Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Seyed Abbas Araghchi amekutana na kufanya mazungumzo na mwenzake wa Oman Badr Al-Busaidi mjini Muscat Jumapili jioni na kujadili masuala mbalimbai yakiwemo ya uhusiano wa pande mbili na matukio muhimu ya kikanda.

Mazungumzo ya wanadiplomasia hao wa ngazi ya juu wa Iran na Oman yanasisitiza kuendelea mawasiliano ya kidiplomasia ya Tehran kwa mataifa jirani huku kukiwa na mvutano unaoongezeka wa kikanda, mashambulizi yanayoendelea ya Israel dhidi ya Gaza, na ukosefu wa utulivu katika Asia Magharibi. Oman kihistoria imekuwa na jukumu la upatanishi kati ya Iran na pande za Magharibi na za kikanda hususan katika masuala ya nyuklia na usalama.

Araghchi, ambaye ametembelea Muscat kama sehemu ya mashauriano ya mara kwa mara ya Iran na majirani zake, ameshukuru juhudi za kidiplomasia za Oman na mipango kuhusu suala la nyuklia la Iran. Pia alibainisha matukio ya hivi karibuni katika uwanja huo, akielezea dhamira ya Tehran ya ushirikiano mzuri wakati wa kutetea maslahi yake ya kitaifa.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Oman Badr Al-Busaidi alieleza tena utayarifu wa Muscat wa kudumisha mazungumzo na ushirikiano na Tehran, akisisitiza umuhimu wa utatuzi wa amani wa migogoro ya kikanda na kuendelea kwa ushirikiano wa kiuchumi kati ya nchi hizo mbili.

Oman inasalia kuwa mmoja wa washirika wakuu wa kidiplomasia wa Iran katika Ghuba ya Uajemi na mara nyingi hutumika kama mpatanishi mtulivu katika mizozo ya kikanda na mawasiliano ya moja kwa moja ya Iran na madola ya Magharibi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *