
Yanga haina muda wa kupoteza baada ya jana kutua Dar na kuchukua ndege kuifuata JS Kabylie ya Algeria kwenye mchezo wa pili wa Makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika huku kocha mkuu wa timu hiyo Pedro Pedro Goncalves akisema wanatawashtua wapinzani wao
Huu ni mchezo wa pili wa Yanga wa hatua ya makundi baada ya kufanikiwa kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya AS FA Rabat ya Morocco na kushika nafasi ya pili kwenye kundi lake nyuma ya Al Ahly ya Misri ambayo iliichapa Kabylie mabao 4-1.
Kocha Pedro ambaye hana sasa kwenye michezo mitatu hajapoteza hata mmoja amesema kuwa wakati wanawafuata JS Kabylie, hawaendi kujihami bali wanakwenda kutafuta ushindi kwenye mchezo huo wa pili ili kujiweka sehemu nzuri kufuzu robo fainali.
Goncalves alisema hautakuwa mchezo rahisi kwa kuwa wenyeji wao wametoka kupoteza lakini pia ubora wao lakini wamejipanga kuanza na msako wa pointi na kama itashindikana basi iwe kupata pointi moja.
“Tumewaona wapinzani wetu ni timu nzuri, siku zote ni vigumu kufanya vizuri ugenini lakini nafurahia aina ya wachezaji wa timu yangu tutajipanga kufanya vizuri,”alisema Goncalves.
“Hatuendi kujilinda tunakwenda kutafuta ushindi kama mechi zingine na kama ikishindikana basi tupate pointi moja, tutakuwa makini kuhakikisha hatufanyi makosa kuwaruhusu wapate bao kirahisi.
Aidha Goncalves aliongeza hatua ya timu yake kuondoka mapema ni kutaka kuzoea hali ya hewa na kuwapa mapumziko mazuri wachezaji wake kwa kuwa safari yao itawalazimu kutumia siku mbili kabla ya kufika.
“Tumeondoka mapema ni kweli lakini fikiria tutakuwa na siku mbili kufika eneo ambalo tutacheza mchezo wetu faida yake ni kwamba wachezaji watakuwa na muda wa kupumzika.
“Watazoea pia hali ya hewa ya kule hapa Tanzania ni joto sana na kule kuna baridi, nadhani uongozi umefanya juhudi nzuri kuwahi kwenda kule.”
Hii ni mara ya nne mfululizo Yanga inafuzu hatua ya makundi ya michuano ya CAF ambapo msimu uliopita timu hiyo iliishia kwenye hatua hiyo jambo ambalo kwa sasa hawataki litokee.