India. Gwiji wa filamu za kidosi amedondoka. Ndiyo, Dharmendra aliiaga dunia jana asubuhi, huku akiacha kilio kwa familia, ndugu jamaa na mashabiki wa filamu waliozishuhudia kazi zake kuanzia miaka ya 1960 hadi alipokumbwa na mauti.

Dharmendra aliyetamba na filamu kama Sholay, Loha na Ram Balram, alikumbwa na mauti akijiandaa kusherehekea miaka 90 ya kuzaliwa kwake Desemba 8, kwani alizaliwa tarehe hiyo mwaka 1935, lakini akijiandaa pia uzunduzi wa filamu ya Ikkis iliyopangwa kuachiwa Krismasi.

Maisha binafsi ya Dharmendra, hususan ndoa zake, yalibaki kuwa jambo la kuwavutia umma na vyombo vya habari kwa miongo kadhaa.

DHAR 02

.

Akiwa na kazi iliyodumu zaidi ya miaka 60 na zaidi ya filamu 300, Dharmendra alisifiwa kama “He-Man” wa asili wa Bollywood na mmoja wa alama zake kubwa zaidi za filamu.

Licha ya kazi yake kubwa, maisha yake ya binafsi, hususan ndoa zake yalivutia sana umma.

DHAR 01

NDOA YA KWANZA NA PRAKASH KAUR

Enzi za uhai wake, Dharmendra alifunga ndoa ya kwanza na Prakash Kaur mwaka 1954, wakati alikuwa na umri wa miaka 19 pekee, muda mrefu kabla hajaingia katika tasnia ya filamu.

Wawili hao walipata watoto wanne, wakiwamo  wa kiume wawili, Sunny Deol na Bobby Deol, ambao wote ni waigizaji mashuhuri na wasichana wawili, Vijeta na Ajeeta.

Alipoanza kucheza filamu mwaka 1960 kupitia Dil Bhi Tera Hum Bhi Tere, tayari alikuwa ameoa na alikuwa baba wa mtoto wa kwanza, Sunny.

Kadri miaka ilivyosonga, Dharmendra aligeuka kuwa mmoja wa nyota wakubwa wa filamu za Kihindi, akiwa na kazi kama Phool Aur Patthar, Sholay, Chupke Chupke, Mera Gaon Mera Desh na Dharam Veer.

STA 01
STA 01

HADITHI YA MAPENZI NA HEMA MALINI

Ilipofika miaka ya 1970, ukaribu wake na mwigizaji wa kike, Hema Malini ulianza kugonga vichwa vya habari.

Wawili hao walicheza pamoja katika filamu kadhaa, ikiwemo Seeta Aur Geeta, Raja Jani, Jugnu, na Sholay. Uhusiano wao wa katika skrini uligeuka kuwa uhusiano wa kimapenzi katika maisha halisi.

Mwaka 1980, Dharmendra alimuoa Hema Malini huku bado akiwa katika ndoa ya kisheria na Prakash Kaur.

Ndoa hiyo na Hema Malin ilizua utata, huku ripoti zikidai Dharmendra na bibie huyo walisilimu ili kufunga ndoa chini ya Sheria ya Kiislamu inayoruhusu ndoa ya wake wengi.

Hatua hiyo ilisemekana kuchukuliwa ili kukwepa Sheria ya Ndoa ya Kihindu, ambayo inaruhusu ndoa ya mke mmoja pekee. Hata hivyo, Dharmendra na Hema Malini walikanusha hadharani madai ya kubadili dini.

Mke wa kwanza, Prakash Kaur, hakuwahi kutalikiwa na aliendelea kuishi na Dharmendra na watoto wao. Aliwahi kumtetea hadharani mumewe. Katika mahojiano ya mwaka 1981 na Stardust, Prakash alisema:

“Kwa nini mume wangu tu? Mwanamume yeyote angeweza kumpendelea Hema kuliko mimi,” alinukuliwa Prakash na kuongeza;

“Wawezaje kumuita mume wangu mtu anayetembea na wanawake, ilhali nusu ya tasnia hii wanafanya hivyo? Huenda si mume bora, ingawa ni mzuri kwangu, lakini bila shaka ni baba bora. Watoto wake wanampenda sana. Hajawahi kuwatelekeza.”

DHARMENDA Pict

KUHUSU MKE MWENZIE

Akizungumzia Hema Malini, Prakash alisema: “Ninaelewa anachopitia. Ana watu wa dunia kukabiliana nao, jamaa na marafiki. Lakini kama ningekuwa katika nafasi yake, nisingefanya alivyofanya. Kama mwanamke namwelewa, lakini kama mke na mama sikubaliani naye.”

Alisisitiza tena Dharmendra ndiye mwanamume wa kwanza na wa mwisho katika maisha yake na angeendelea kumheshimu kama baba wa watoto wao.

STA 02

FAMILIA PACHA

Katika ndoa na Hema Malini, gwiji huyo wa filamu yaani Dharmendra alipata binti wawili, Esha Deol na Ahana Deol. Kwa miaka mingi, familia hizi mbili ziliishi kwa mpangilio wa kipekee: Dharmendra aliendelea kuishi na Prakash Kaur na watoto wao, huku Hema Malini na binti zao wakiishi sehemu tofauti Mumbai.

Dharmendra alikuwa akiwatembelea mara kwa mara, ingawa familia hizo mbili ziliendelea kuishi maisha yao kwa kujitegemea.

Hadi mauti yamememfika, Dharmendra ameacha wake wawili yaani Prakash Kaur na Hema Malini pamoja na watoto sita ambao ni; Sunny, Bobby, Vijeta, Ajeeta, Esha na Ahana sambamba na hazina kubwa ya filamu alizocheza enzi za uhai wake akishirikisha na magwiji wenzake kadhaa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *