Dar es Salaam. Wanawake na vijana wanaohudumu kwenye biashara ndogo za chakula maarufu kama mama lishe na baba lishe wametajwa kuwa miongoni mwa wanufaika wakubwa wa mpango mpya wa kuwawezesha kiuchumi baada ya Benki ya Stanbic Tanzania, kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo la Ujerumani (GIZ), kuzindua rasmi programu ya RISE Mama Lishe.

Mpango huo, unaolenga kuwafikia wajasiriamali 2,000 katika mikoa ya Arusha, Dar es Salaam, Dodoma, Kilimanjaro na Tanga, utajikita katika kutoa mafunzo ya biashara, upatikanaji wa huduma za kifedha, matumizi ya nishati safi ya kupikia pamoja na ushauri wa kisheria ili kuboresha mazingira ya biashara zao.

Uzinduzi wa programu hiyo umefanyika jijini Dar es Salaam katika kituo cha Stanbic Biashara Incubator, ambako wafanyabiashara 96 kutoka Coco Beach wamehitimu mafunzo ya majaribio yaliyolenga kutathmini mbinu mpya za ufundishaji.

Katika mafunzo hayo ya siku nne, washiriki wamepata elimu ya upangaji bei, usimamizi wa fedha, huduma kwa wateja, ujasiriamali, usafi wa chakula, utunzaji wa kumbukumbu na matumizi ya mitandao ya kijamii kutangaza bidhaa. Masuala hayo yaliyotajwa kama vikwazo vikubwa kwa walaji wengi wa kipato cha chini.

Tatu Ally, anayeuza vinywaji na maji ya nazi Coco Beach, amesema mafunzo hayo yamebadili mtazamo wake wa biashara.

“Nimejifunza kupanga bei kwa faida, kutunza kumbukumbu na kuwahudumia wateja kwa ujasiri zaidi. Mauzo yanaongezeka na sasa napanua biashara,” amesema.

Ayoub Mabrouck, muuzaji wa ubuyu, alisema mafunzo yamemwongezea mbinu za uzalishaji na masoko.

“Nimetumia mitandao ya kijamii kutangaza bidhaa. Ubora umeongezeka, uzalishaji unaongezeka na mpango huu umetupa dira ya muda mrefu,” amesema.

Katika kuongeza tija kwa biashara hizo, Stanbic imekabidhi majiko 100 yenye ufanisi wa nishati kwa wahitimu wa mafunzo. Majiko hayo yanadaiwa kupunguza matumizi ya mkaa na kuni, gharama za uendeshaji pamoja na moshi unaoweza kuhatarisha afya.

Mkuu wa Stanbic Biashara, Kai Mollel akizungumza na wahitimu wa mafunzo ya mpango wa Rise Mamalise uliondaliwa na Benki ya Stanbic na GIZ.

Hatua hiyo inaenda sambamba na malengo ya Taifa ya kufikia upishi safi ifikapo 2032, pamoja na kupunguza athari za tabianchi.

Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Biashara za Kati wa Stanbic, Stephen Mpuya, alisema mpango huo ni sehemu ya jitihada za benki kuweka wanawake na vijana katikati ya ukuaji wa uchumi.

“Mama Lishe wanapoboreshwa, kaya zinapata kipato bora na jamii inanufaika. Tunawapa mafunzo, majiko salama na huduma za kifedha ili wakue kwa uthabiti,” alisema.

Kwa upande wake, Awadh Milasi kutoka GIZ amesema Mama Lishe ni kundi muhimu katika mnyororo wa uchumi, hivyo wanahitaji ujuzi na zana sahihi za kukua.

“Tunawapa mafunzo ya vitendo na zana salama za kupikia, huku tukilinda mazingira kupitia majiko bora,” alisema.

Mkurugenzi wa Mafunzo wa SIDO, George Kasinga, amesema ushiriki wa taasisi hiyo una hakikisha mafunzo yanahusisha changamoto halisi za wajasiriamali.

“Tunataka Mama Lishe waondoke na ujuzi wanaoweza kuanza kutumia kesho,” amesema.

Kwa mujibu wa waandaaji, utekelezaji wa mpango utaanza jijini Dar es Salaam kupitia vipindi saba vya mafunzo katika Stanbic Biashara Incubator kabla ya kuhamia Arusha, Kilimanjaro, Tanga na Dodoma. Madarasa yataendeshwa jioni ili kuwaruhusu Mama Lishe kuendelea na shughuli zao.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *