
Katika ujumbe mahususi kwa ajili ya maadhimisho haya ya kwanza ya Siku ya Kimataifa ya Usafiri Endelevu kwa maana ya njia za usafiri zinazozingatia mazingira, Guterres anaelezea usafiri kama “mfumo wa mzunguko wa damu wa dunia,” unaowezesha biashara, kuunganisha jamii, na kuendeleza ajira. Hata hivyo, anasisitiza kuwa mfumo huohuo sasa ni kichocheo kikubwa cha ongezeko la joto duniani.
“Sekta ya usafiri inawajibika kwa takribani robo ya uzalishaji wote wa gesi chafu,” anasema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na kuongeza kuwa asilimia 91 ya nishati inayotumika katika usafiri wa barabara, baharini na angani bado inatokana na mafuta ya kisukuku, jambo linalofanya “kuwa miongoni mwa maeneo magumu zaidi kupunguza hewa ukaa.”
Licha ya changamoto hiyo kubwa, Bwana Guterres anaonesha matumaini kwamba suluhu zipo na kwamba mataifa yanapaswa kuchukua hatua mara moja.
“Ninaamini binadamu tuna uwezo wa kuvunja utegemezi wetu kwa mafuta ya kisukuku yanayoharibu tabianchi,” anasema Guterres, akizitaka serikali kuwekeza katika “mifumo ya usafiri thabiti, yenye ufanisi na yenye kiwango kidogo cha hewa ukaa, inayozingatia vyanzo bunifu vya nishati jadidifu.”
Anataja maendeleo ya kiteknolojia na sera zinazoweza kuharakisha mabadiliko hayo, ikiwemo magari ya umeme na ya kutumia nishati ya jua, mafuta mbadala kwa usafiri wa anga, uwekezaji mkubwa katika usafiri wa umma unaozingatia utunzaji wa mazingira, bei ya kaboni na ruzuku kwa nishati zenye utoaji mdogo wa hewa chafuzi.
Guterres anasisitiza kwamba usafiri endelevu ni nguzo muhimu ya kufikia malengo ya kimataifa ya tabianchi na kulinda mustakabali wa sayari. Anahitimisha akisisitiza, “Hakuna muda wa kupoteza. Tuchukue hatua sasa.”
Katika ripoti yake ya mwaka 2016, Kikundi cha Ushauri cha Ngazi ya Juu cha Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kilifafanua usafiri endelevu kama “utoa ji wa huduma na miundombinu ya usafrishaji wa watu na bidhaa unaokuza maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo kwa namna iliyo salama, nafuu, inayoweza kufikiwa na wote, yenye ufanisi na ustahimilivu, huku ikipunguza utoaji wa hewa ukaa na uchafuzi mwingine pamoja na madhara ya kimazingira.”
Mwaka 2023, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilitangaza Muongo wa Kwanza Kabisa wa Usafiri Endelevu wa Umoja wa Mataifa, ambao utaanza mwaka 2026.
Uzinduzi wa Muongo wa Usafiri Endelevu utafanyika tarehe 10 mwezi ujao yaani Desemba mwaka huu wa 2025, hapa katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa, New York, Marekani.