Jamaica. Muziki  wa reggae umepata pigo jingine. Baada ya kudondoka magwiji kadhaa wa miondoko hiyo maarufu duniani kama Bob Marley, Peter Tosh, Gregory Isaacs, Lucky Dube, Bunny Wailer wiki hii tena gwiji mwingine, Jimmy Cliff, naye ameumaliza mwendo.

Mwanamuziki huyo mkongwe wa reggae na ikoni ya utamaduni wa Jamaica, Jimmy Cliff, aliyekuwa na sauti ya kipekee na mchango mkubwa katika tasnia ya filamu, alifariki dunia Jumatatu akiwa na miaka 81.

Taarifa ya kifo cha gwiji huyo ilitolewa na mkewe Jumatatu iliyopita kupitia mitandao ya kijamii.

“Kwa huzuni kubwa ninapenda kuuwataarifu kwamba mume wangu, Jimmy Cliff, ameaga dunia kutokana na mshtuko uliofuatiwa na nimonia,” alisema Latifa Chambers katika taarifa iliyochapishwa kwenye akaunti ya Instagram ya Cliff.

“Naishukuru familia yake, marafiki, wasanii na wafanyakazi wenzake ambao wameshiriki safari yake naye. Kwa mashabiki wake duniani kote jueni kuwa msaada wenu ulikuwa nguvu katika kazi yake. Jimmy, mpenzi wangu pumzika kwa amani. Nitafuata matakwa yako,” iliongeza taarifa ya Latifa, huku watoto wa Jimmy ambao ni Lilty na Aken wakitia saini zao.

Waziri Mkuu wa Jamaica, Andrew Holness, alimwita Cliff, “shujaa wa kweli wa utamaduni ambaye muziki wake ulibeba moyo wa taifa letu. Jimmy Cliff alisimulia hadithi yetu kwa uaminifu na moyo.

“Muziki wake uliwakomboa watu katika nyakati ngumu, ulihamasisha vizazi, na ulichangia kuunda heshima ya kimataifa ambayo utamaduni wa Jamaika unafurahia leo hii. Tunatoa shukrani kwa maisha yake, mchango wake, na kiburi alicholeta kwa Jamaica. Tembea salama, Jimmy Cliff. Urithi wako unaendelea katika kila kona ya kisiwa chetu na mioyoni mwa watu wa Jamaica.”

PIGO KUBWA

Kifo cha Jimmy Cliff ni pigo kubwa kwa muziki wa reggae na ulimwengu wa muziki kwa ujumla, kwani ni wazi umepoteza mmoja wa watu walio hodari zaidi katika kutumia fursa.

Wale wasio na huruma wangeweza kumwita mtu wa bahati tu, lakini tangu mwanzo kabisa, palikuwa na mambo machache sana ambayo hangeyajaribu kama aliona yanaweza kumsaidia yeye mwenyewe au kuisaidia muziki.

Kifo chake kilileta simanzi kubwa katika ulimwengu wa muziki, kwani alibaki kuwa mmoja wa wanamapinduzi wa reggae walioisukuma muziki huo kufika hadhi ya kimataifa, na kimetokea wakati mashabiki wapenzi wa miondoko hiyo wakiendelea kuwalilia na kuwambuka magwiji kadhaa wa reggae waliofariki dunia kwa vipindi tofauti.

Kwa wanaokumbuka, miaka 18 iliyopita, Lucky Dube, aliyetamba na miondoko hiyo huko Afrika Kusini, alikumbwa na mautio Oktoba 2007 kwa kuuwawa na majambazi akiwa jijini Johannesburg.

Mei 11, 1981, gwiji Bob Marley naye alikumbwa na mauti kwa kilichoelezwa saratani iliyoanzisha katika kidole, achilia mbali Gregory Isaacs aliyeaga dunia Oktoba 2010 na Bunny Wailer, yeye alikumbwa na mauti Machi 2021 baada ya kuugua kwa muda, bila kumsahau Peter Tosh aliyefariki Septemba 1987.

Hivyo kufariki dunia kwa Jimmy Cliff ni pigo jingine kwa wanazi wa reggae, japo huyu ameondoka akiwa amekuwa humvi ya kutosha tofauti na kina Dube na Marley, waliokuwa hawajafikisha hata umri wa mkongwe huyo aliyezaliwa na kupewa jina la James Chambers.

ALIKOANZIA

Jimmy alizaliwa Julai 30, 1944, huko Somerton District, St. James, Jamaica, akifahamika kama James Chambers, akiwa ni mtoto wa pili kati ya tisa, na akiwa na kijana mdogo wa miaka 12 tu, alianza kuonyesha mapenzi makubwa kwa muziki, na alianza kuandika nyimbo.

Akiwa na miaka 14, aliamua kuachana na jina lake halisi na kujipachika la Jimmy Cliff; wakati huo baba yake akimhamishia Kingston, Jamaica, na mzuka wa moyo na mapenzi ya muziki wa reggae. Huko ndipo alikutana na kumshawishi Leslie Kong, Mchina Mjamaika aliyemiliki duka lililochanganya aiskrimu, duka la rekodi na vipodozi, linaloitwa Beverley’s, na kuanzisha lebo yake mwenyewe.

Leslie Kong alimsaidia kurekodi nyimbo zake za kwanza za Dearest Beverley na Hurricane Hattie.

Nyimbo hizo zilimfanya atambulike katika tasnia ya muziki ya Jamaica na kupanda pia kimataifa katika miaka ya 1960 na 1970, ambayo ilikuwa kipindi cha ukuaji wake mkubwa wa kimuziki.

“Niliandika wimbo uitwao Dearest Beverley na kumwimbia dukani siku iliyofuata. Aliupenda sana sauti yangu… akaniuliza anawezaje kuingia kwenye utengenezaji wa rekodi. Mimi nilijua wanamuziki, studio, nilijua biashara. Kwa hiyo ningeweza kumsaidia,” alinukuliwa.

Chini ya uongozi wa Kong na Cliff, Beverley’s ikawa lebo iliyofanikiwa na yenye ushawishi mkubwa.

ATUA LONDON

Baada ya kutamba sana Jamaica, Jimmy alihamia London, England, ambapo alijifunza mitindo mipya ya muziki wa kimataifa; hili lilimsaidia kuleta mchanganyiko wa reggae na pop uliompa umaarufu duniani.

Alisisitiza mara nyingi kwamba hatua hii ilimsaidia kukua kama mtunzi na ilimruhusu kupeleka muziki wa Jamaica katika uwanja wa kimataifa bila kupoteza asili yake.

Pia alijitosa katika ulimwengu wa filamu, na mwaka 1972 alicheza kazi iitwayo The Harder They Come. Hii ilikuwa moja ya mafanikio yake makubwa, akiigiza kama Ivanhoe Martin katika filamu hiyo iliyoongozwa na Perry Henzell.

Filamu hiyo ilimfanya awe nyota wa kimataifa na ilimsaidia kueneza reggae duniani na kuhifadhi pia jina lake katika historia ya utamaduni wa Jamaica. Wimbo wa The Harder They Come na vibao vingine alivyoimba katika filamu hiyo zilibaki kuwa alama ya reggae hadi leo, akiwa mtunzi, mwimbaji na mcharaza magitaa.

KAZI ZA MOTO

Jimmy anakumbukwa kwa kazi zake murua alizowahi kuzitoa enzi za uhai wake, ambazo ni mamia ya nyimbo na albamu. Lakini baadhi ya nyimbo na albamu zake maarufu zaidi za gwiji huyo ni: The Harder They Come, Miss Jamaica, Struggling Man, Brave Warrior, Give Thanks, Black Magic, The Power and the Glory, Many Rivers to Cross, You Can Get It If You Really Want, Wonderful World, Beautiful People, Sitting in Limbo na I Can See Clearly Now (toleo la filamu Cool Runnings).

Albamu zake maarufu ni pamoja na Harder They Come (Soundtrack), Jimmy Cliff, Struggling Man, Rebirth (2012), huku akitaka tuzo mbalimbali za kitaifa na kimataifa zikiwamo Rock and Roll Hall of Fame (2010), aliingizwa kama msanii mahiri wa reggae duniani. Alishinda Grammy kupitia albamu Rebirth (2012), National Honours za Jamaica, Order of Merit (OM) ambayo ni heshima ya juu inayotolewa kwa wasanii wakubwa wa Jamaica, na Order of Distinction.

Pia amewahi kutwaa tuzo za heshima mbalimbali duniani kutokana na mchango wake katika reggae na utamaduni wa Jamaica, na albamu yake ya mwisho kuiachia ni Refugees ya mwaka 2022.

URITHI ALIOACHA

Jimmy Cliff aliacha muziki wenye ujumbe wa matumaini, mapambano na uthabiti, mchango mkubwa katika kuusambaza reggae duniani, sambamba na filamu iliyogeuka kuwa hadithi ya vizazi vya wasanii wa Caribbean na ushawishi mkubwa kwa wasanii kama Bob Marley, Peter Tosh, Burning Spear na wengine.

Mwamba huyo aliyekuwa memba wa harakati za Rastafari alikuwa mkristo kabla ya kubadili dini na kuwa Mwislam, japo mwaka 2013 katika mahojiano alisema hayupo katika harakati zozote za kidini kwa vile anaamini katika ulimwengu wa sayansi.

Enzi za uhai wake alibahatika kuoa na kujaaliwa watoto watatu: Lilty, Odessa (ambaye ndiye wa mwisho) na Nabiyah Be, ambaye ni muigizaji na mwanamuziki kama alivyokuwa gwiji huyo. Nabiyah Be ameigiza filamu ya Black Panther. Mtoto wa kiume wa pekee wa gwiji huyo ni Aken.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *