Dar es Salaam Ikiwa ni mfuatiliaji wa mitandao ya kijamii hususan kwa wapenzi wa muziki wa singeli utakuwa umekutana na mwanamuziki machachari K Zungu.  Msanii anayekuja kwa kasi kupitia muziki wa singeli.

Akizungumza na Mwananchi, K Zungu ameeleza safari yake ya kimuziki mpaka kufikia alipo sasa huku akifichua kuwa alianza tangu alipokuwa darasa la sita.

“Safari yangu ya muziki nilianza nikiwa mdogo tu, nilikuwa darasa la sita, niliimba huku nasoma, nilikuwa napata shavu la kuimba katika sherehe hizi za vigodoro, harusi na sherehe mbalimbali zilizokuwa zinafanyika mitaani. Nakumbuka nilivyofika darasa la saba kukatangazwa Singeli Search ilikuwa inaitwa Singeli Movement iliyokuwa inasimamiwa na Meneja Abas.

“Tulikuwa wasanii sikosei zaidi ya 50. Mungu akabariki nikaingia robo fainali, ikaja fainali na nikashinda, wakaniambia tunaenda Dar es Salaam tukirudi tunakuchukua. Kipindi hicho nilikuwa Muheza, Tanga basi kweli wakarudi kuja kunichukua na hiyo ndio safari yangu ya muziki ilipoanzia,”amesema Zungu.

Kupitia wimbo wake alioachia ‘Kuna Wakati’ msanii huyu anasema, umempatia mafanikio na ujasiri wa kupanda jukwaa lolote.
 
“Kupitia wimbo huo wasanii wakubwa wamekuwa wakinitafuta akiwamo Jaiva, Chino, Dulla Makabila, Mzee wa Bwax, umenifanya nitambulike hata nikienda sehemu yoyote najulikana. Mbali na hayo nimepata nakala kwenye Air Tanzania, kwa sababu kwenye ndege hiyo kuna kitabu ambacho kinaelezea mambo mbalimbali kuhusu Tanzania wameelezea pia kuhusu muziki wa Singeli na katika toleo hilo mimi pia nimeandikwa,”amesema. 

Aidha ameongezea kwa kueleza “Idea ya ‘Kuna Wakati’ niseme tu imeletwa na Mungu. Kwasababu kuna siku Mzee wa Bwax alikuja studio kurekodi, basi wakati wameplay beat mimi nikawa naimba kama masihara. Wakaanza kuniambia mbona nzuri hiyo ngoja nikuchukue clip basi wimbo huo ukaanzia hapo. Nikaurekebisha kidogo na ndio huo ambao watu wanatamba.” 

Hata hivyo ameeleza licha ya ulemavu wa ngozi alionao anashukuru hajawahi kunyanyapaliwa na mtu yeyote huku akiweka wazi kuwa ameamua kujitosa kwenye Singeli ili kuwaonesha watu kuwa na wao wanaweza kufanya makubwa kama binadamu wengine.

“Nikiwa kama ambassador wa watu wenye ulemavu wa ngozi ‘Albinims’ unajua sisi bila kujipambania hakuna mtu wa kutupambania. Mimi naamua nifanye kuonesha kwamba tunaweza kwahiyo mashabiki zangu sapoti kubwa ninayohitaji ili niweze kusogea kwenye muziki wangu ni kusikiliza kazi zangu na kufuatilia mitandao yangu ya kijamii hususani YouTube.”

“Jambo jingine japo nina Meneja Abass lakini tunatoa nafasi kwa watu ambao wanataka kutia mkono kwenye kipaji changu ili niweze kukua zaidi. Ninauwezo wa kuimba nyimbo zozote ukiachana na singeli ikiwamo Hip Hop na Bongo Fleva hivyo kikubwa Watanzania wanisapoti tu.”

Mbali na hayo Zungu ameweka wazi kuwa kwa sasa anatamani kufanya kolabo na mastaa wakubwa akiwamo Diamond, Dulla Makabila, Yammy pamoja na Vanilla akieleza kuwa akifanikiwa kufanya kazi na wasanii hao basi anaamini itakuwa ni tiketi yake ya kutoboa kimuziki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *