Tanzania imeandika historia kwa kupata ushindi wa kwanza kwenye Fainali za Kombe la Dunia la mchezo wa Futsal baada ya kuichapa New Zealand kwa mabao 4-2 leo huko Philippines.
Ushindi huo umekuja ikiwa ni siku tatu baada ya Tanzania kupokea kichapo cha mabao 10-0 katika mechi ya kwanza dhidi ya Ureno.
Katika mchezo wa leo, mabao ya Tanzania yamepachikwa na Mary Siyame aliyefunga matatu na lingine moja limewekwa kimiani na Winfrida Mathias.
Ushindi wa leo umeweka hai matumaini ya Tanzania kuingia hatua inayofuata ya mashindano hayo huku ukiifanya New Zealand kuaga rasmi.
Tanzania sasa inahitaji ushindi katika mchezo wa mwisho dhidi ya Japan ili iweze kuingia katika hatua ya robo fainali kutokea kundi C.
Ikumbukwe hii ni mara ya kwanza kwa Tanzania kushiriki Fainali za Kombe la Dunia za mchezo wa Futsal ambazo pia zinafanyika kwa mara ya kwanza.
Tanzania ilikata tiketi ya kushiriki Fainali za Kombe la Dunia la Futsal baada ya kumaliza katika nafasi ya pili ya katika Fainali za Mataifa ya Afrika kwa mchezo huo.
Katika fainali hizo za Afrika ambazo zilifanyika Aprili 22 hadi Aprili 30 mwaka huu, wenyeji Morocco walitwaa ubingwa kwa kuifunga Tanzania kwa mabao 3-2 katika mechi ya Fainali.