
Taarifa ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Duniani, WHO iliyotolewa leo Lubumbashi, DRC inasema chanjo ya surua ya (monovalent) itabadilishwa na chanjo mseto ya surua-rubella (MR) katika ratiba ya chanjo za kawaida, huku kampeni za kufidia zikiwa zimepangwa ili kuziba mapungufu ya kinga miongoni mwa watoto na vijana dhidi ya magonjwa haya mawili. Utekelezaji wa chanjo ya MR na kampeni za kufidia utafanyika hatua kwa hatua kulingana na makundi ya majimbo.
Kundi la kwanza, linalojumuisha majimbo saba, Bas-Uélé, Haut-Katanga, Haut-Lomami, Haut-Uélé, Ituri, Lualaba na Tanganyika litaendesha kampeni hiyo kuanzia Novemba 27 hadi Desemba 1, 2025.
“Utangulizi wa chanjo ya surua na rubela ni hatua muhimu kwa afya ya watoto na unatupeleka karibu na jitihada zetu za pamoja kuhakikisha kuwa hakuna mtoto anayeteseka au kufa kutokana na magonjwa haya yanayoweza kuzuilika,” anasema Dkt. Mohamed Janabi, Mkurugenzi wa WHO kanda ya Afrika.
Zaidi ya watoto milioni 7 walio chini ya umri wa miaka mitano wako hatarini
Wahudumu wa afya watatoa chanjo kupitia vituo maalumu na maeneo ya muda, ili kuhakikisha hata watoto wanaoishi katika maeneo magumu kufikiwa na yaliyoathiriwa na migogoro wanapata huduma.
Mamlaka za afya za Congo zinatoa wito kwa wazazi na viongozi wa jamii kuhakikisha hakuna mtoto anayesalia nyuma.
“Kampeni hii ni hatua muhimu kuelekea kutokomeza surua na rubella nchini mwetu,” anasema Dkt. Roger Kamba, Waziri wa Afya ya Umma wa DRC.
Mabadiliko kutoka chanjo moja ya surua kwenda chanjo ya MR yanasaidiwa na wadau kadhaa, wakiwemo Muungano wa Chanjo (Gavi), Taasisi ya Gates, Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Duniani (WHO), Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) na Vituo vya Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa Marekani (CDC).
DRC imekumbwa na milipuko ya mara kwa mara ya surua, ikionesha umuhimu wa haraka wa hatua hii. Zaidi ya watoto milioni 7 wenye umri chini ya miaka mitano wako hatarini kwa sasa. Mbali na kuziba mapengo ya chanjo, utangulizi wa chanjo ya MR pia utasaidia kupunguza mzigo wa ugonjwa wa rubella ya kuzaliwa (congenital rubella syndrome) na unatarajiwa kuliweka taifa kwenye mkondo wa kutokomeza surua na rubela.