Nigeria. Mwanamuziki kutoka Nigeria, Sarah Oyinkansola ‘Ayra Starr’ amesema amehamia kwa muda Marekani kwa ajili ya kukamilisha shughuli zake za kumuziki akiwa humo.
Mwanadada huyo alianza muziki mwaka 2019 kwa kufanya kava za wasanii wengine na mwisho ni mwa mwaka huo akatoa ngoma yake rasmi iitayo ‘Damage’ iliyoanza kumpa umaarufu mkubwa.
Akizungumza na kituo cha redio cha Hot 93.7FM Ayra alikiri kuhamia New York, jambo ambalo linaashiria sura mpya katika maisha yake binafsi na taaluma yake ya muziki.
“Nimehamia New York rasmi ndani ya miezi miwili, lakini mimi siku zote nipo hapa kwa kiroho, muda niliokaa hapa umekuwa na maana kubwa kwangu,” amesema Ayra Starr na kuongeza;
“Najihisi hivyo, New York inanikumbusha Lagos sana kwa sababu ya vaibu lake, watu wamechangamka na kuna Wanigeria wengi hapa, kuna pia wakazi wengi wa Kiafrika, kwa hivyo najisikia kama nyumbani.”
Ayra aliyepo chini ya lebo ya Mavin Records inayowasimamia wasanii wakubwa Nigeria kama Rema, amekuwa miongoni mwa wasanii wanaofanya vizuri nchini humo.
Wimbo wake wa Commas alioutoa mwaka 2024 ulimpa umaarufu mkubwa duniani, ukafanya uingie kwenye tuzo kubwa kama Grammy ingawa haukuchukua tuzo.