Manchester, England. Erling Haaland ameendelea kuwasha moto baada ya kuandika historia mpya kwenye Ligi Kuu England kwa kufikisha idadi ya mabao 100 ndani ya mechi 111 tu, na hivyo kuivunja rekodi ya muda mrefu iliyokuwa ikishikiliwa na Alan Shearer.

Straika huyo wa Manchester City alifunga bao hilo dakika ya 17 pale Craven Cottage, akipiga shuti kali ambalo lilimwacha golikipa, Bernd Leno bila cha kufanya katika mchezo wa Ligi Kuu England uliopigwa usiku wa jana dhidi ya Fulham.

Bao hilo lilimrudisha nyuma Shearer, aliyewahi kuhitaji mechi 124 kufikisha mabao 100 katika miaka ya 1990. Awali mambo yalionekana kuwa magumu kwa Haaland baada ya kupenya ngome ya Fulham na kukosa nafasi ya kuandika bao la mapema.

Hata hivyo, alivyopata nafasi ya pili alipachika bao na kuthibitisha tena kwa nini amekuwa tishio lisilozuilika tangu atue Etihad akitokea Borussia Dortmund Julai 2022.

Kwa kufikisha mabao hayo, nyota huyo raia wa Norway sasa amewapita masupastaa kama Thierry Henry aliyewahi kufikisha idadi ya mabao 100 katika mechi 141, Sergio Aguero (147) na Mohamed Salah (162), lakini Haaland amekuwa mchezaji wa kwanza aliyewahi kufikisha idadi ya mabao 100 kwa haraka zaidi katika historia ya EPL.

Bao hilo alilofunga usiku wa jana Jumanne, Desemba 2, 2025 pia limemfanya aendelee kuongoza chati ya wafungaji msimu huu akiwa na mabao 15, akiwaacha Igor Thiago wa Brentford mwenye mabao 11 na Danny Welbeck wa Brighton mwenye mabao saba.

Tangu awasili City, Haaland amlivunja rekodi ya kupachika mabao mengi kwenye msimu mmoja wa EPL akifanya hivyo msimu wa 2022/2023 alipofunga jumla ya mabao 36 na kuvunja rekodi ya Mo Salah ya mabao 32 katika msimu wa mechi 38 wa 2017/2018.

Huu msimu umekuwa muendelezo wa ubora wake, kwani kabla hajafikisha miaka 26 tayari amejikusanyia mafanikio kibao, akiongoza mabao katika ngazi ya klabu na timu ya taifa ndani ya mwaka 2025.

Baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 5-4 kikosi cha Pep Guardiola kimezidi kuiongezea presha Arsenal kikibakiza tofauti ya pointi mbili licha ya kuwa na mchezo mmoja zaidi ya vinara hao ambao leo watavaana Brentford.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *