
Hivi sasa Umoja wa Mataifa unajiandaa kwa uchaguzi na uteuzi wa Katibu Mkuu mpya mwaka 2026. Je mchakato huo unafanyaje kazi?, na kwa nini ni muhimu zaidi sasa kuliko hapo awali?.
Hatua ya 1: Uteuzi unafunguliwa
Takriban mwaka mmoja kabla ya kipindi cha Katibu Mkuu wa sasa kumalizika, marais wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na Baraza Kuu hutoa barua ya pamoja wakizihimiza Nchi Wanachama kutaja wagombea.
Kila mtu aliyepewa msaada na nchi inaweza kuwania kiti hicho, kawaida ni rais wa zamani, waziri wa mambo ya kigeni au afisa wa ngazi ya juu.
Mwaka 2016, kwa mara ya kwanza, wagombea walichapisha wasifu wao na taarifa za maono yao mtandaoni, hatua kubwa kuelekea uwazi katika mchakato ambao kwa muda mrefu ulikuwa umefichwa.
Hatua ya 2: Orodha fupi ya Baraza la Usalama
Shindano halisi linaanza ndani ya Baraza la Usalama lenye wanachama 15. Ndani ya milango iliyofungwa, wajumbe hufanya mfululizo wa “kura za majaribio,” wakitaja kila mgombea kama kuunga mkono, kupinga au kutokuwa na maoni.
Wanachama watano wa Kudumu ambao ni Marekani, Urusi, China, Ufaransa na Uingereza hutumia fomu za rangi ili wengine waweze kuona iwapo mwanachama wa kundi hilo lijulikanalo kama P5 anapinga. “ Kura moja ya Hapana kutoka kwa yeyote kati yao inaweza kumaliza kampeni ya mgombea”.
Baada ya duru kadhaa mfano ilichukua duru sita mwaka 2016, mgombea mmoja kawaida huchaguliwa bila kura ya turufu au veto ya P5.
Ndipo Baraza linafanya kura rasmi kupendekeza mtu huyo kwa Baraza Kuu.
Hatua ya 3: Uidhinishaji wa mgombea Baraza Kuu
Kutoka hapo, Baraza Kuu lenye wanachama 193 linapiga kura kumteua mgombea aliyewasilishwa na Baraza la Usalama, kawaida kwa kupiga makofi, ikimaanisha pongezi badala ya kuhesabu majina.
Katibu Mkuu anahudumu kwa kipindi cha miaka mitano, kinachoweza kuongezwa mara moja kwa miaka mitano mingine, desturi ambayo imewahi kuvunjwa mara moja tu katika historia ya Umoja wa Mataifa.
Mchakato huu unaonesha usawa wa nguvu wa Umoja wa Mataifa: kila nchi ina sauti, lakini hakuna anayepata kazi bila idhini ya wanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama au P5.
Kanuni ambazo hazijaandikwa
Kiasi kikubwa cha kile kinachobainisha matokeo hakijaandikwa, lakini kinaunda kila hatua
• Hakuna raia wa nchi zenye nguvu kubwa: Hakuna raia wa nchi tano wachachama wa kudumu wa baraza la Usalama P5, ambaye amewahi kuwa Katibu Mkuu, kwani itachukuliwa kama upendeleo.
• Mzunguko wa Kijiografia: Kazi hii kwa siri hubadilishwa au kuzunguka kati ya kanda za ndunia dunia. Baada ya Mwafrika Kofi Annan, alikuja Masia Ban Ki-moon, kisha Myuropa António Guterres. Wengi wanatarajia Katibu Mkuu anayefuata atoke Amerika ya Kusini.
• Desturi ya Vipindi Viwili: Wengi wa Makatibu Wakuu wanahudumu vipindi viwili iwapo wataendeleza uhusiano mzuri na nguvu kuu. Mmoja tu ambaye ni Boutros Boutros-Ghali alikosa kipindi cha pili baada ya Marekani kutumia kura ya turufu , veto mwaka 1996.
Mageuzi na mustakbali wa UN
Kwa miongo kadhaa, uteuzi wa Katibu Mkuu ulikuwa mchakato wa siri kati ya nguvu kuu. Hali hiyo ilianza kubadilika mwaka 2015 na kampeni ya “1 kwa Bilioni 7,” iliyopiga msasa kwa uteuzi wazi, kuweka orodha za wagombea kwa umma na kusikilizwa mbele ya Baraza Kuu.
Shindano la 2016 lilikuwa la uwazi zaidi katika historia ya Umoja wa Mataifa. Wagombea walikabiliwa na vikao vya maswali na majibu hadharani, pamoja na kushirikiana na vyombo vya habari na mashirika ya kiraia.
Kwa kuwa kipindi cha pili cha Guterres kinamalizika mwaka 2026 kwani alianza kipindi chake cha pili Januari 1, 2022, mchakato ujao utafanyika chini ya uangalizi mkubwa zaidi.
Wagombea lazima wachapishe taarifa za maono, wafichue wafadhili wa kampeni zao na waache kazi yoyote ya Umoja wa Mataifa ili kuepuka mgongano wa maslahi.
Kuna pia msukumo unaoongezeka wa mara ya kwanza katika historia: kumchagua mwanamke. Baada ya miongo minane na wanaume tisa, wanadiplomasia, wanaharakati wengi wanasema ni wakati kwa uongozi wa Umoja wa Mataifa kuakisi maadili yake ya usawa na uwakilishi.
Ni nani ambaye ameshajitokeza kuwania kiti hicho?
Wakati mbio za kumpta mkuu mpya wa Umoja wa Mataifa ndio zimeanza tu, wagombea watatu tayari wamejitokeza, kila mmoja akileta uzoefu na mtindo tofauti.
Michelle Bachelet wa Chile, mara mbili alichaguliwa kuwa Rais wa taifa hilo na baadaye mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa
Rebeca Grynspan wa Costa Rica, makamu wa rais wa zamani wa taifa hilo na sasa Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la Biashara na Maendeleo UNCTAD
Na Rafael Mariano Grossi wa Argentina, mkuu wa muda mrefu wa Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki IAEA.
Uteuzi zaidi unatarajiwa kadri Nchi wanachama wanavyopima hali ya kisiasa huko New York kabla ya kuanza rasmi kwa mchakato.
Kwa nini ni muhimu
Katiba ya Umoja wa Mataifa inamwita Katibu Mkuu “afisa mkuu wa kiutawala wa shirika”. Kwenye vitendo, jukumu hilo linachanganya diplomasia, uongozi na mamlaka ya kimaadili “sehemu sawa za Mwanadiplomasia na mchechemuzi, mtumishi wa umma na Mkurugenzi Mtendaji,” kama Umoja wa Mataifa unavyofafanua.
Na ingawa Katibu Mkuu si rais wa dunia, ushawishi wake ni mkubwa kuanzia kuhamasisha misaada ya kibinadamu hadi upatanishi wa mizozo na kuwawajibisha wenye nguvu. Kuhakikisha kwamba mwanadiplomasia mkuu wa kimataifa anachaguliwa kwa uwazi na kwa haki si tu usimamizi wa mpangilio bali ni demokrasia kwenye jukwaa la kimataifa.
Lini Katibu Mkuu mpya ataanza kazi?
Endapo mchakato wa uchaguzi utaenda kama ulivyopangwa Katibu Mkuu anayefuata wa Umoja wa Mataifa anatarajiwa kuanza kazi tarehe 1 Januari 2027. Katibu Mkuu wa sasa, António Guterres, atamaliza awamu yake ya pili ya miaka mitano tarehe 31 Desemba 2026.