
Picha kutoka kituo cha matibabu cha Al-Shifa zinaonesha majengo yaliyoanguka, shoroba zilizoteketea kwa moto na miundombinu iliyosambaratika, taswira ya uharibifu uliolazimisha hospitali hiyo kufanya kazi kwa sehemu ndogo tu ya uwezo wake.
Akiwa amesimama katikati ya vifusi, Mwakilishi wa UNFPA Palestina eneo linalokaliwa Kimabavu na Israel Nestor Owomuhangi, amesema mnepo wa wahudumu wa afya wa Gaza unaendelea kuhamasisha juhudi za shirika hilo.
“Hii ilikuwa moja ya hospitali kubwa zaidi za uzazi katika Ukanda wa Gaza, na leo, kama unavyoona nyuma yangu, yote ni magofu. Lakini bado inasimama, bado inafanya kazi,” amesema Owomuhangi.
Ameongeza kuwa licha ya uharibifu mkubwa, wahudumu wa afya wanaendelea kutoa huduma bora kwa wanawake na wasichana katika mazingira magumu.
UNFPA: Hatujawahi kuondoka Gaza
Owomuhangi amesisitiza kuwa dhamira ya UNFPA imeendelea tangu siku za mwanzo za mapigano.
“UNFPA imekuwa pamoja na watu wa Ukanda wa Gaza tangu mwanzo wa vita, na hatujawahi kuondoka,” amesema.
“Tunaendelea kusaidia vituo 22 vya afya, vikiwemo hospitali tano kubwa kama Al-Shifa.”
Kwa mujibu wa UNFPA, msaada wake umewezesha takribani kujifungua kwa wanawake 130, ambapo asilimia 98 ya watoto bado wanazaliwa katika vituo vya afya licha ya mfumo wa afya kuporomoka kwa kiasi kikubwa.
Hata hivyo, wakina mama 18 sasa wanajifungua nje ya vituo vya afya, hali ambayo shirika linaonya kuwa ni hatari kwa mama na mtoto.
Wakunga wako msitari wa mbele wa mapambano
Ili kuzuia ongezeko la kujifungua katika mazingira hatarishi, UNFPA inawapeleka wakunga wengi zaidi katika Ukanda wa Gaza.
“Kwa sasa, wakunga 175 wamesambazwa katika Ukanda wa Gaza,” amesema Owomuhangi akiongeza kuwa
“Tunaendelea kuleta vifaa vya matibabu na mahitaji muhimu. Tutaendelea kuleta dawa kutoka duniani kote hadi tufikie asilimia 100 ya wanawake kujifungua salama ndani ya Gaza.”
Kuendeleza huduma za afya za Gaza
Licha ya uharibifu mkubwa katika Hospitali ya Al-Shifa, hospitali hiyo bado inaendelea kufanya kazi kwa kiasi, ikitoa huduma muhimu za afya ya uzazi na huduma nyingine za matibabu.
Msaada wa UNFPA unajumuisha utoaji wa dawa, vifaa vya matibabu, mahitaji ya afya ya msingi na msaada wa kuendelea kuendesha vituo vinavyokabiliwa na changamoto.
Mabango katika eneo la hospitali yanaonesha ujumbe wa kuunga mkono wanawake wa Palestina ishara inayoonekana ya uwepo endelevu wa shirika hilo.
Kulinda afya ya wanawake na wasichana
Juhudi zinazoendelea za UNFPA zinalenga kulinda afya ya uzazi katika moja ya nyakati ngumu zaidi kuwahi kushuhudiwa katika Ukanda wa Gaza.
Owomuhangi ametoa wito wa kuendelezwa kwa msaada na mshikamano wa kimataifa ili kuhakikisha huduma hizi zinaendelea kuwepo.