Kamishna Türk, ametoa onyo hilo kufuatia kuripotiwa vifo vya zaidi ya watu 269 kutokana na mashambulizi tangu mwishoni mwa mwezi Oktoba 2025.

Türk ameongeza kuwa raia wengi wanashikiliwa kwa tuhuma za “kushirikiana” na upande pinzani, huku pia kukiongezeka hotuba za chuki zinazochochea machafuko zaidi.

Hali ikoje?

Taarifa kutoka Geneva Uswisi imeeleza kuwa tangu tarehe 25 Oktoba, baada ya RSF kuuteka mji wa Bara, Ofisi ya Haki za Binadamu ya UN imeorodhesha vifo vya angalau raia 269 kutokana na mashambulizi ya angani, mabomu ya ardhini na mauaji ya kiholela. Idadi hiyo huenda ikawa kubwa zaidi kutokana na kukatika kwa mawasiliano na intaneti, jambo linalozuia taarifa sahihi kupatikana.

Ripoti zinaonesha pia ulipizaji kisasi, ukamatwaji holela, utekaji, ukatili wa kingono na ulazimishaji wa watu ikiwemo watoto kulazimishwa kujiunga na makundi ya kivita.

Kwa majuma ya hivi karibuni, mashambulizi kadhaa yameripotiwa, ikiwemo shambulio la ndege zisizo na rubani la RSF tarehe 3 mwezi Novemba katika mji wa El Obeid lililoua takribani watu 45, wengi wao wanawake, na shambulio la anga la SAF tarehe 29 Novemba katika eneo la Kauda lililosababisha vifo vya takriban watu 48.

Mapigano mazito yanaendelea katika majimbo yote matatu ya Kordofan, na kusababisha vifo na majeruhi zaidi.

Miji ya Kadugli na Dilling imezingirwa na RSF pamoja na SPLM-N, huku El Obeid nayo ikiwa imezungukwa kwa kiasi kikubwa.

Hali ya kibinadamu

Hali ya kibinadamu inaelezwa kuwa ni mbaya sana, njaa imethibitishwa huko Kadugli na hatari ya njaa ikiongezeka Dilling, huku pande zote zikizuia misaada ya kibinadamu kufika kwa walio hatarini.

Zaidi ya watu 45,000 wamelazimika kukimbia makazi yao mwezi uliopita, wakitafuta usalama ndani au nje ya Kordofan.

Kamishna Türk amezitaka pande zote katika mzozo nchini Sudan kusitisha mapigano mara moja, kuruhusu misaada ya dharura, kulinda wahudumu wa kibinadamu na kurejesha mawasiliano ili taarifa muhimu ziweze kuwafikia raia.

Ametoa wito kwa nchi zenye ushawishi kuingilia kati, kusitisha mtiririko wa silaha na kusaidia kumaliza mapigano. “Hatuwezi kuruhusu Kordofan kuwa mwendelezo wa maafa tuliyoyaona El Fasher. Vita lazima vikome sasa,” alisema Mkuu huyo wa Haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *