Ugonjwa huu wa vimelea unaosababishwa na mbu unaweza kuzuilika na kutibika, imesema ripoti hiyo lakini bado ni tishio kubwa la afya duniani ukiua mamia ya maelfu ya watu, wengi wao wakiwa watoto wadogo na wanawake wajawazito, hususan Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara.

Taarifa ya hivi karibuni ya WHO inaonesha maendeleo makubwa tangu mwaka 2000, hatua za kinga zimeokoa takribani maisha ya watu milioni 14 duniani kote katika kipindi cha miaka 25 iliyopita, na nchi 47 zimethibitishwa kutokuwa na malaria kabisa.

Hata hivyo, malaria bado ni tatizo hatari. Kwa mujibu wa ripoti kulikuwa na zaidi ya visa milioni 280 vya malaria na vifo zaidi ya 600,000 mwaka 2024, huku asilimia 95 ya visa hivyo vikirekodiwa katika ukanda wa Afrika vingi katika nchi 11 tu.

Usugu wa dawa waongezeka

Ripoti hiyo inasema kikwazo kikubwa katika kutokomeza malaria ni suala la usugu wa dawa, ambalo limepewa sura maalum katika ripoti ya mwaka huu, nchi nane zimeripoti usugu uliothibitishwa au unaoshukiwa wa dawa za kutibu malaria, ikiwemo artemisinin, moja ya tiba inayopendekezwa na WHO.

Ili kukabiliana na hili, ripoti inapendekeza nchi kuepuka kutegemea dawa moja tu na badala yake kuboresha udhibiti, ufuatiliaji na mifumo ya afya.

Upungufu wa ufadhili katika eneo lenye migogoro, ukosefu wa usawa wa kudhibiti mabadiliko ya taianchi na mifumo dhaifu ya afya ni sababu nyingine muhimu. Imesema ripoti hiyo

Takribani dola bilioni 3.9 ziliwekezwa katika kukabiliana na malaria mwaka 2024, chini ya nusu ya lengo lililowekwa na WHO.

Ripoti inaonesha kuwa Msaada wa Maendeleo kutoka nchi tajiri ODA, umeshuka kwa karibu asilimia 21.

Bila uwekezaji zaidi, waandishi wa ripoti wanatahadharisha kuwa kuna hatari ya kuibuka tena kwa mlipuko mkubwa usiodhibitika.

Taa nyekundu zinawaka zikiashiria hatari

“Malaria bado ni ugonjwa unaoweza kuzuilika na kutibika, lakini hilo huenda lisidumu milele,” ameonya Dkt. Martin Fitchet, Mkurugenzi Mtendaji wa Medicines for Malaria Venture, shirika lisilo la hisani linaloongoza katika ukuzaji wa dawa mpya za kutibu malaria, wakati wa mkutano wa WHO kuwasilisha ripoti hiyo.

Ameongeza kuwa “Ni lazima tuchukue hatua sasa kuongeza wigo na uratibu wa ufuatiliaji ili tusitembee gizani, na kuwekeza kwa ujasiri, katika ubunifu wa dawa za kizazi kijacho ili vimelea visituzidi kasi.”

Dkt. Fitchet amekumbusha madhara yaliyosababishwa na usugu wa dawa ya chloroquine katika miaka ya 1980 na 1990.

Hali hiyo ilisababisha janga la kibinadamu, na kupoteza maisha ya mamilioni ya watu, hasa watoto.

“Leo tunaona kupitia ripoti hii kwamba taa nyekundu zinawaka tena, huku ongezeko la mabadiliko sugu likiripotiwa barani Afrika. Tunahitaji kuhakikisha tunadumisha uimara na ufanisi wa dawa tulizonazo sasa.” Amesema

“Lakini ushindi wa muda mrefu katika vita dhidi ya malaria unategemea utengenezaji wa dawa za kizazi kijacho za kutibu malaria.”

Ameongeza kuwa “ugumu na ukubwa wa changamoto tunayokabili hauwezi kushughulikiwa na chombo kimoja au taasisi moja.”

Amehitimisha kwa kutoa wito wa ushirikiano unaovuka sekta nzima ya afya ya binadamu, ukijumuisha “sekta ya viwanda, mashirika ya afya ya kimataifa, vyuo vikuu, madaktari, watafiti, mashirika ya kiraia, jamii na wafadhili.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *