Kwa mujibu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu na Misaada ya Dharura OCHA, watu 107,000 wamekimbia makazi yao katika wiki za hivi karibuni, na kufanya idadi ya waliokimbia katika miezi minne iliyopita kufikia 330,000.

Hawakuwa na muda wa kupona kabla ya kulazimika tena kukimbia, kutokana na mashambulizi au hofu ya mashambulizi, amesema Paola Emerson, Mkuu wa OCHA nchini Msumbiji.

Mtaalamu huyo mkongwe wa masuala ya kibinadamu ameeleza kuwa ghasia zimekuwa zikilazimisha familia kuhama mara kadhaa wanapokabiliwa na wiki za mashambulizi mfululizo.

Hili ni jambo lisilo la kawaida, ikilinganishwa na mbinu za awali za mashambulizi ya ghafla na kutoweka yaliyoshuhudiwa wakati ghasia zilipoanza kaskazini mwa Cabo Delgado mwaka 2017.

Takwimu za Umoja wa Mataifa zinaonesha kuwa mzozo huu pamoja na misukosuko ya tabianchi sasa vimesababisha zaidi ya watu 600,000 kukimbia makazi yao, huku karibu watu tisa kati ya kumi waliokimbia ghasia wakiwa tayari wamekimbia angalau mara moja mwaka huu.

Familia zimekusanyika kaskazini mwa Msumbiji Mkoa wa Nampula, baada ya kukimbia ghasia.

© UNHCR/Isadora Zoni

Familia zimekusanyika kaskazini mwa Msumbiji Mkoa wa Nampula, baada ya kukimbia ghasia.

Kupigwa na vimbunga

Bi. Emerson ameongeza kuwa wimbi hili jipya la mashambulizi limevuruga kwa kiasi kikubwa jamii ambazo tayari zimeathiriwa na vimbunga vitatu mwaka 2025.

Idadi kubwa ni watoto ambayo ni asilimia 67,” amesema Bi. Emerson. “Kuna hofu kubwa za ulinzi, zikiwemo taarifa za ukatili wa kijinsia na watoto waliotenganishwa na familia au walioko peke yao.”

Familia nyingi sasa zinahifadhiwa katika jamii zinazowapokea ambazo zimefurika watu, maeneo ya wazi au shule zilizoharibiwa, ambako mitihani imevurugika katika wilaya kadhaa.

Ugawaji wa msaada uko chini sana ya mahitaji, afisa huyo wa Umoja wa Mataifa ameongeza, hukukukiwa na karibu asilimia 40 tu ya watu wanaopokea msaada mdogo wa chakula, katikati ya upungufu mkubwa wa bidhaa”.

Bi. Emerson ameonya kuwa mapungufu katika msaada tayari yanazisukuma baadhi ya familia kurejea katika maeneo yasiyo salama bila taarifa za kutosha kuhusu endapo hali imetulia”.

Ukatili Mkubwa ukijumuisha watu kukatwa vichwa

Mashirika ya Umoja wa Mataifa yametoa maonyo kadhaa wiki hii. Jumanne, Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi UNHCR, lilisema raia wameripoti mashambulizi ya usiku, nyumba kuchomwa moto na mauaji ya kukatwa vichwa wakati makundi yenye silaha yalipoingia katika wilaya ambazo hapo awali hazikuathirika.

Shirika hilo lilionya kuhusu uhaba mkubwa wa rasilimali, likisema hatua zilizopo sasa ni  “hafifu”.

Shirika la Umoja wa Mataifa la Watoto UNICEF, limeongeza leo kuwa watoto wanasukumwa hadi kikomo cha ustahimilivu.

Limeonya kuhusu viwango vya “kushtua vya watu kukimbia makazi na ongezeko la ukiukaji mkubwa wa haki za watoto, ikiwemo utekaji na uandikishwaji katika makundi yenye silaha”.

Shirika hilo limesema huduma muhimu za afya, elimu, maji na ulinzi zinaelemewa na mahitaji, wakati msimu wa vimbunga ukitarajiwa kuwa mkali zaidi.

Wito wa ufadhili wa dharura

Wadau wa misaada wametoa wito wa ufadhili wa haraka ili kuzuia hali kuzorota zaidi, wakionya kuwa bila msaada wa haraka, mgogoro utakua, na familia zinaweza kulazimika kukimbia tena ndani ya wiki chache zijazo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *