Msemaji wa Umoja wa Mataifa , Stéphane Dujarric, ameviambia vyombo vya habari hii leo kwenye Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York Marekani kuwa Katibu Mkuu amempongeza Rais wa Marekani Donald Trump kwa jukumu lake katika mchakato huu na pia kumpongeza Rais Félix Tshisekedi wa DRC na Rais Paul Kagame wa Rwanda kwa kufanikisha hatua hii muhimu.”

Dujarric amesema “Katibu Mkuu ameashiria kuwa makubaliano haya ni hatua muhimu katika kurejesha uaminifu kati ya DRC na Rwanda na katika kuendeleza juhudi za amani ya kudumu katika eneo la mashariki mwa DRC,”.

Mchango wa mchakato wa Doha

Katibu Mkuu pia amebainisha maendeleo makubwa yaliyofikiwa chini ya mchakato wa Doha na juhudi zinazosimamiwa na Muungano wa Afrika.

Amezihimiza pande zote kuheshimu ahadi walizozichukua, ikiwa ni pamoja na kuzingatia usitishwaji wa kudumu wa mapigano kama ilivyoagizwa na azimio la Baraza la Usalama  namba 2773 (2025).

Akimalizia, Dujarric amesisitiza kuwa Umoja wa Mataifa, ikiwa ni pamoja na Mpango wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini  DRC (MONUSCO), “uko tayari kuendelea kusaidia juhudi zote kuelekea amani na utulivu wa kudumu nchini DRC na Ukanda mzima.”

Makubaliano ya Washington yanawakilisha mafanikio makubwa ya kidiplomasia yanayolenga kumaliza mzozo wa miongo kadhaa kati ya nchi hizi mbili, hasa katika mashariki mwa DRC ambapo migogoro ya muda mrefu imekuwa chanzo cha kutokuwa na utulivu wa kikanda.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *