
Akizungumza kwenye kikao cha Baraza la Usalama kuhusu hali nchini Ukraine mjini New York Marekani amesema “Mwaka 2025 umekuwa mmoja wa miaka yenye vifo vingi zaidi kwa watu wa Ukraine, licha ya matumaini madogo yanayotokana na kurejea kwa juhudi za kidiplomasia,”
Bi. Gotoh Amesema idadi ya vifo na majeruhi kwa raia imeongezeka kwa asilimia 24 kati ya Januari na Novemba ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka 2024, huku Shirikisho la Urusi likiongeza mashambulizi ya anga kote Ukraine.
Tangu uvamizi mkubwa na kamili wa Urusi kuanza Februari 2022, Ofisi ya Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa OHCHR, imethibitisha kwamba raia 14,775 wa Ukraine, wakiwemo watoto 755, wameuawa, na wengine 39,322, wakiwemo watoto 2,416, wamejeruhiwa.
Idadi halisi ya waathirika huenda ni kubwa zaidi
“Hizi ni takwimu zilizothibitishwa tu. Idadi halisi huenda ni kubwa zaidi,” amesema.
Akirejea kwamba mashambulizi dhidi ya raia na miundombinu yao ni marufuku chini ya sheria za kimataifa “kama tulivyosisitiza katika taarifa zetu zote” ameongeza kuwa “mashambulizi hayo hayakubaliki na lazima yakome popote yanapotokea”.
Ameeleza pia matukio kadhaa yanayoashiria “hatua nyingine hatari katika mzunguko wa sasa wa kuongeza mvutano, ikiwemo madai ya ukiukaji wa anga za nchi kadhaa za Ulaya, matukio ya hivi karibuni yanayohusisha meli na miundombinu ya bandari katika Bahari Nyeusi, na mashambulizi yanayoendelea karibu na kinu cha nyuklia cha Zaporizhzhia.”
Mnepo mkubwa wa watu wa Ukraine
Katika hali hii, Gotoh amesema watu wa Ukraine “sio tu wameonesha mnepo wa kushangaza kukabiliana na madhara ya vita, bali pia dhamira ya kujenga mustakabali wa amani, demokrasia na ustawi kwa nchi yao.”
Akitaja matumaini kwamba juhudi za kidiplomasia zinazoongozwa na Marekani zinaweza kusaidia kumaliza vita kupitia mazungumzo, amesisitiza kuwa kupungua kwa mapigano kutasaidia kuokoa maisha ya raia na kuimarisha kasi ya mazungumzo hayo.
“Tunazitaka pande zote kujihusisha kikamilifu na kusaidia mchakato jumuishi wa kidiplomasia kwa lengo la amani ya haki, ya kudumu na ya kina,” amesema.
Waukraine wako katika giza totoro: OCHA Msuya
Watu wa Ukraine wako chini ya moto Mkubwa wa vita na wako gizani. Wanahitaji ulinzi wa kweli na si huruma tu amesema Joyce Msuya Naibu Mratibu wa Umoja wa Mataifa wa Misaada ya Kibinadamu na Masuala ya Dharura (OCHA)
Ameongeza kuwa “Watu wa Ukraine hawana fursa ya kusubiri hali kuwa bora”. Amesisitiza kuwa wanakabili baridi kali katika msimu wao wa nne wa baridi tangu vita vianze, “wakiwa gizabi na chini ya mashambulizi.”
Anasema wanachohitaji kutoka kwa Baraza “si huruma tu, bali hatua madhubuti za kupunguza madhara na kulinda kazi ya kibinadamu inayowezesha maisha yao kuendelea.”
Ameendelea kusema kuwa “Hatua zenu katika wiki zijazo zitaamua kama msimu huu wa baridi utakuwa tena sura nyingine ya mateso yanayoweza kuzuilika au wakati ambao Baraza linasaidia kuyazuia”
Amewasihi wajumbe wa Baraza kutumia ushawishi wao kuhakikisha mambo matatu:
- Sheria za vita zinaheshimiwa ili kuwalinda raia;
- Msaada wa kibinadamu unawafikia watu bila hatari na bila vikwazo;
- Operesheni za kibinadamu zinapata ufadhili unaohitajika kukidhi mahitaji ya dharura.
Akitoa mifano, amesema kwamba katika wiki mbili tangu taarifa ya mwisho, mashambulizi ya makombora na ndege zisizo na rubani au drone kote Ukraine yameendelea kuua na kujeruhi raia, kuharibu nyumba, na kuharibu vibaya miundombinu ya nishati wakati wa hali ya baridi kali.
Ameonya kuwa pengo la ufadhili linaathiri sana hatua za msaada, kwani ni asilimia 65 tu ya mpango wa msaada wa baridi wa dola milioni 278 umefadhiliwa, na hivyo kulazimisha kupunguza huduma za kupashia joto, msaada wa fedha taslimu, huduma za afya ya akili na programu za ulinzi.
Kwa watu milioni 10.8 wanaotarajiwa kuhitaji msaada mwaka 2026, “hata upungufu mdogo unawaacha maelfu bila msaada wanaohitaji ili kuendelea kuishi,” amesema bi Msuya.
Sura mpya ya kutisha ya majeraha
Shirika la Usalama wa Binadamu na Uondoaji wa Mabomu limetoa tahadhari kuhusu sura mpya ya kutisha ya majeraha nchini Ukraine.
“Kile nilichoshuhudia Ukraine kinaashiria sura mpya ya kutisha katika mabadiliko ya majeraha kutokana na mabomu ya kutegwa ardhini,” amesema Tomaž Lovrenčič, Mkurugenzi wa ITF Enhancing Human Security.
Mabomu ya ardhini na sasa mabomu ya kutupwa na droni kutoka angani yanaunda “mashamba ya mabomu angani, na kuwa na athari mbaya za kibinadamu kwa kuwa mabomu hayo yanapiga usoni, kichwani, mikononi na miguuni, na kusababisha majeraha ya muda mrefu yanayobadili maisha.”
ameisimulia ziara yake ya hivi karibuni Ukraine ambako alikutana na manusura waliopata ulemavu wa sehemu za juu za mwili, kukatwa viungo, kupoteza uwezo wa kusikia na msongo mkubwa wamawazo.
Aamesisitiza kuwa mabomu kutoka kwenye droni ni “holela na ni ya kudhalilisha utu na mara nyingi magumu zaidi kutibu kuliko mabomu ya ardhini ya kawaida”.
Waathiriwa wengi wanakabiliwa na maisha ya kutengwa kijamii, kiuchumi na kimwili bila msaada wa kudumu wa kimataifa.
Ameitaka jamii ya kimataifa, ikiwemo Baraza la Usalama, kuchukua hatua katika vipaumbele vitatu:
- Kuongeza kwa kiwango kikubwa shughuli za kuondoa na kutegua mabomu, ikiwa ni pamoja na uwekezaji katika teknolojia mpya;
- Kutambua msaada kwa waathiriwa na vifaa vya viungo bandia kuwa “nguzo kuu, si jambo la kufikiria mwishoni”;
- Kusisitiza chini ya sheria za kimataifa za kibinadamu kwamba matumizi ya silaha zisizobaguzi na mashambulizi dhidi ya raia lazima yakome.
Ametoa wito pia kwa washirika kutoa msaada wa ugawanaji mzigo, akionya kuwa Ukraine inaweza kuwa “mfano wa kusikitisha katika migogoro ya baadaye iwapo dunia haitachukua hatua za kutosha”.
Amemalizia kwa wito wa mshikamano unaotokana na “heshima, haki na matumaini ili Waukraine waweze kujenga upya maisha na jamii zao.”