Dar es Salaam. Mwimbaji wa Afrobeats kutokea Nigeria, Tems (31), kwa mara nyingine tena ameshika nafasi ya kwanza katika chati ya Billboard Mainstream R&B/Hip-Hop Airplay ikiwa ni mara yake ya nne, rekodi inayothibitisha mafanikio ya kazi zake nchini Marekani.
Tems, mshindi wa tuzo za Grammy mara mbili, amerudi tena namba moja kupitia wimbo wake ‘What You Need’ kutoka katika Extended Playlist (EP) yake ya tatu, Love Is a Kingdom (2025).
Wimbo huo umepanda kutoka nafasi ya pili hadi kuwa namba moja, hatua inayoonyesha kuwa ndio wimbo uliochezwa zaidi kwenye vituo vikubwa vya redio vya R&B/Hip-Hop nchini Marekani kuanzia Juni 19 hadi 25.
Hiyo ni kwa mujibu wa kampuni ya uchambuzi wa data za burudani Marekani, Luminate ambayo hukusanya taarifa kutoka kwa watoa huduma zaidi ya 500 duniani, kisha kuzihakiki na kuzitumia kupima umaarufu wa nyimbo na wasanii.
Kwa miaka mingi, Luminate ndio chanzo kikubwa cha takwimu zinazotumika kutengeneza chati nyingi za Billboard.
Wimbo huo wa Tems (What You Need), uliotolewa na kusambazwa kupitia lebo ya Since 93/RCA Records, umeshika nafasi hiyo ya kwanza kwa kuupiku wimbo wa Rick Ross, French Montana na Max B ‘Minks in Miami’ ambao umeporoka hadi nafasi ya tano.
Mwaka 2021, ndipo Tems alishika nafasi ya kwanza katika chati ya Billboard Mainstream R&B/Hip-Hop Airplay kwa mara ya kwanza kupitia wimbo aliyoshirikishwa na Wizkid ‘Essence’ uliokaa namba moja kwa wiki 10.
Aliendelea na moto huo mwaka 2022, ambapo kolabo yake na Future na Drake ‘Wait for U’ ulishika nafasi ya kwanza kwa wiki 16, vilevile wimbo wake mwenyewe ‘Free Mind’ kutoka katika EP yake ya kwanza, For Broken Ears (2022), ambao ulitawala nafasi hiyo kwa wiki mbili.
Mbali na hilo, wimbo wa ‘What You Need’ imepanda kutoka nafasi ya 23 hadi ya 16 kwenye chati ya Adult R&B Airplay na kushinda tuzo ya Greatest Gainer kama wimbo uliopata ongezeko kubwa zaidi la usikilizwaji kwa wiki hiyo.
Kutokana na mafanikio yake kwenye chati za Mainstream R&B/Hip-Hop na Adult R&B, wimbo huo umeendelea kushika nafasi ya tatu kwenye chati ya R&B/Hip-Hop Airplay, huku ukiongeza idadi ya wasikilizaji wake kwa asilimia 12 ambao ni sawa na milioni 13.1.
Mafanikio hayo pia yameusaidia wimbo huo kupanda kwenye chati ya Radio Songs ambayo hujumuisha aina zote za muziki, ukitoka nafasi ya 39 hadi ya 32 ukiwa na wasikilizaji milioni 16.
Mbali na wimbo huo, Tems ameendelea kufanya vizuri Marekani kupitia wimbo, Raindance (2025) alioshirikishwa na Dave, rapa kutokea Uingereza. Wimbo huo umeendelea kupanda juu kwenye chati mbalimbali ikiwamo Rap Airplay, Rhythmic Airplay na R&B/Hip-Hop Airplay.
Mafanikio ya Tems yamekuja baada ya hapo awali waimbaji wakubwa wa kike duniani kama Rihanna na Beyonce kuonyesha kukubali kipaji chake.
Ikumbukwe Tems ambaye hivi karibuni ametumbuiza katika tuzo za BET nchini Marekani, ameshiriki kuandika wimbo wa Rihanna, Lift Me Up (2022) ambao ulitumika katika filamu, Black Panher2: Wakanda Foreve. Vilevile amefanya hivyo katika wimbo wa Beyonce ‘Move’ kutoka katika albamu yake ya saba, Renaissance (2022).