Balozi wa Iran nchini Kenya amesema kuwa uhusiano kati ya Tehran na Nairobi umeingia katika hatua mpya.
Ali Gholampour, balozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nchini Kenya ameashiria kufanyika kwa duru ya saba ya Kamisheni ya Ushirikiano wa Pamoja wa Iran na Kenya baada ya kupita muongo mmoja na kusisitiza kuwa, uhusiano kati ya Tehran na Nairobi umeingia katika hatua mpya.
Alieleza kuwa, kufanyika kwa mkutano wa kamisheni hiyo kuwa ni “maendeleo makubwa” katika uhusiano kati ya nchi hizo mbili na kusema: “Katika ushirikiano wa pande mbili, uhusiano wa kisiasa, kibiashara na kiutamaduni uko kwenye ajenda.”
Akizungumzia uhusiano wa kiuchumi kati ya Iran na Kenya, Gholampour alibainisha: Wafanyabiashara wa Iran wanaweza kufanya kazi katika uwanja wa kusafirisha nje bidhaa za viwandani, hospitali, dawa, kilimo na vifaa vya ujenzi, na mkabala wake, inawezekana kuagiza bidhaa za kilimo za Kenya, ikiwa ni pamoja na kahawa, maua, chai na nyama fresh, kwa Iran.
Aliongeza: “Tulijaribu kuongeza uagizaji wa nyama fresh kutoka Kenya hadi Iran.” Vile vile ametaja ushirikiano wa kitamaduni na kusema: “filamu za mfululizo za Kiirani hurushwa hewani kwenye kanali za televisheni za Kenya.”
Akiashiria kutwaa ubingwa wa timu ya taifa ya Iran ya taekwondo katika michuano ya dunia iliyofanyika nchini Kenya, Gholampour aliyaona mafanikio hayo kuwa ya “muhimu sana” na kusema: “Mafanikio haya ya kimichezo yanatoa taswira bora ya nchi yetu mbele ya propaganda chafu.”
Ushahidi uliopo unaonyesha kuwa, uhusiano kati ya Iran na Kenya umeingia katika hatua mpya, na mabadiliko haya yanaonekana katika nyanja za kisiasa, kiuchumi, kiutamaduni na hata kimichezo.
Uhusiano kati ya Iran na Kenya una historia ndefu, kuanzia miaka ya 1970. Baada ya misukosuko mingi, ikiwa ni pamoja na kukatika kwa mahusiano mwaka 1977 na kuanza tena mwaka 1982, nchi hizi mbili zimejaribu kila mara kuboresha kiwango cha mahusiano yao.

Katika miaka ya hivi karibuni, mahusiano haya yameonekana zaidi katika nyanja za biashara na utamaduni. Kenya, ikiwa ni moja ya nchi muhimu katika Afrika Mashariki, ina nafasi maalum katika diplomasia ya Iran katika bara la Afrika. Iran, kwa kuzingatia uwezo wake wa kiuchumi na kisayansi, inafuatilia kupanua ushirikiano na nchi za Afrika, ikiwemo Kenya.
Katika miezi ya hivi karibuni, kumekuwa na dalili za wazi kwamba uhusiano kati ya Tehran na Nairobi unaingia katika hatua mpya, ikiwa ni pamoja na mkutano kati ya balozi wa Iran nchini Kenya na Spika wa Bunge la nchi hiyo mwezi Machi 2025, ambapo msisitizo uliwekwa katika kuimarisha ushirikiano wa Mabunge, kuyafanya amilifu makundi ya kirafiki, na kupanua uhusiano wa kibiashara.
Mkutano huo pia umefungua njia ya ushirikiano katika Mkutano wa Iran na Afrika unaolenga kuimarisha uhusiano wa kiuchumi na kisiasa kati ya Iran na nchi za Afrika. Mikutano kama hiyo inaonyesha kwamba, diplomasia ya bunge na maingiliano ya moja kwa moja kati ya vyombo vya sheria vya nchi hizo mbili ni wenzo wa kuimarisha uhusiano.
Kwa upande mwingine, kufanyika duru ya saba ya Kamisheni ya Ushirikiano ya Pamoja ya Iran na Kenya baada ya kusitishwa kwa muongo mmoja ni ishara muhimu ya kuanza awamu mpya ya uhusiano kati ya nchi hizo mbili. Tume imechunguza maeneo ya ushirikiano katika nyanja za kisiasa, kibiashara na kitamaduni na kufikia makubaliano mapya.
Katika nyanja ya kiuchumi, Iran inataka kusafirisha bidhaa za viwandani, hospitali, dawa, vifaa vya kilimo na ujenzi nchini Kenya, na mkabala wake imeongeza uagizaji wa bidhaa za kilimo za Kenya kama vile kahawa, chai, maua na nyama fresh nchini Iran. Ubadilishanaji huu wa bidhaa unaweza kusaidia kuingiza anuwai ya bidhaa katika masoko ya nchi zote mbili na kuinua uhusiano wa kiuchumi kutoka kiwango kidogo hadi endelevu zaidi.

Katika nyanja ya kitamaduni, uhusiano kati ya Iran na Kenya pia umeingia katika hatua mpya. Kurushwa hewani filamu za mfululizo za Kiirani katika kanali za televisheni za Kenya ni mfano wa ushirikiano huu wa kiutamaduni unaoweza kuleta ufahamu bora wa utamaduni na jamii ya Iran miongoni mwa watu wa Kenya.
Mbali na kuimarisha uhusiano wa kitamaduni, hatua hizo zitasaidia kuboresha taswira ya Iran katika maoni ya umma wa Kiafrika. Ushirikiano wa michezo, kama vile uwepo wa timu za Iran katika Mashindano ya Dunia ya Taekwondo nchini Kenya, pia unaonyesha uwezo mpya katika uhusiano kati ya nchi hizo mbili.
Kwa mukhtasari, inaweza kusemwa kwamba, uhusiano kati ya Iran na Kenya sasa unaelekea kwenye hatua mpya, yenye sifa ya kupanuka kwa ushirikiano wa pande nyingi, kuimarisha uhusiano wa bunge, kuendeleza mabadilishano ya kiuchumi, na kuimarisha maingiliano ya kitamaduni na michezo.
Mchakato huu sio tu kwamba unachangia maslahi ya pamoja ya nchi hizo mbili, lakini pia unaweza kuwa mfano wa kuigwa kwa uhusiano wa Iran na nchi nyingine za Kiafrika. Ikiwa njia hii itafuatiliwa kwa umakini, uhusiano kati ya Tehran na Nairobi unaweza kuinuliwa hadi kiwango cha kimkakati na kuunganisha nafasi ya Iran katika ukanda wa Afrika Mashariki.