Tarehe 10 Desemva wiki hii, Ofisi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa OHCHR itaungana na dunia kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Haki za binadamu ikikumbuka kupitishwa kwa azimio la tamko la haki za binadamu UDHR mwaka 1948. Je maadhimisho ya mwaka huu yanajikita na nini? Na kwa nini ni muhimu?  Seifu Magango Msemaji wa Ofisi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa anafafanua  akizungumza na Idhaa hii ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa.

Akizungumzia kuhusu  azimio la tamko hilo la haki za binadamu Magango amesema “Mwaka huu ni maadhimisho ya miaka 77 ya Azimio hilo UDHR. Kaulimbiu ya mwaka 2025 ni Haki za Binadamu, Msingi wa Kila Siku, inasisitiza kwamba haki za binadamu si kanuni za mbali, bali ndiyo nguzo za kila siku zinazowawezesha watu binafsi na jamii kuishi kwa usalama, utu na uhuru. Kaulimbiu ya Siku ya Haki za Binadamu mwaka huu ni, Haki za Binadamu, Msingi wa Kila Siku.”

Kwa nini kaulimbui hii na nini umuhimu wake?

Akijibu swahili hilo msemaji huyo wa haki za binadamu anafunguka “Katika kipindi hiki cha misukosuko, ambamo wengi wanahisi ongezeko la hali ya kutokuwa na uhakika, kukata tamaa na kutengwa, lengo letu ni kuthibitisha tena thamani ya kudumu ya haki za binadamu. Kupitia kampeni hii, tutawaunganisha tena watu na haki za binadamu kwa kuonesha jinsi zinavyoathiri maisha yetu ya kila siku, mara nyingi kwa njia ambazo huenda hatuzitambui. Kampeni itasisitiza kwamba haki za binadamu ni chanya, za msingi na zinaweza kupatikana. Haki za binadamu ndizo dira yetu katika nyakati zenye misukosuko  hutuelekeza na kututuliza wakati wa sintofahamu,”

Mwaka huu wa 2025, misingi yenyewe ya haki za binadamu imewekwa kwenye mizani tumeshuhudia changamoto lukuki ikiwemo barani Afrika. Nini unadhani kimechochea zaidi hali hiyo?

“Kutokuwepo kwa usawa kunazidi kuongezeka, migogoro inazidi kushika kasi, dharura ya tabianchi inazidi kuwa mbaya, na baadhi wanaunda na kujaribu kuongeza migawanyiko ndani ya jamii na kati ya nchi. Lakini hatupaswi kukata tamaa,Tunahitaji mshikamano zaidi na haki zaidi za binadamu ili kukabiliana na changamoto za sasa. Ni muhimu kuendelea kutetea haki zetu za msingi.”

Kampeni ya mwaka huu ambayo Haki za binadamu ni Msingi wa Kila inaangazia vipengele viwili vinavyohusiana vya haki za binadamu: Mosi upekee wa kuanzishwa kwake kama moja ya ahadi za kimataifa zilizoathiri dunia kwa kiasi kikubwa, na pili uwepo wake wa kila siku, wa lazima, ulioshikana na maisha yetu.Kwa nini hili ni muhimu sana?

Seif amesema “Kilicho cha kiufundi kinakuwa halisi tunapotambua kwamba matendo ya kila siku kutumia muda na familia, kusoma habari, kutembea kwa uhuru, kunywa maji safi, au kufurahia mlo yanawezekana kutokana na utekelezaji wa haki za binadamu.

Tamko la kimataifa la haki za binadamu

Credit : Rorie Katz (UNPA stamp designer)

Tamko la kimataifa la haki za binadamu

Ameongeza kuwa “Misingi hii imewekwe katika Azimio la Haki za Binadamu (UDHR) haki ya kuwa na kiwango cha maisha kinachofaa (Kifungu cha 25), kinachohakikisha chakula, mahitaji ya msingi na mazingira yenye afya; haki ya uhuru wa maoni na kujieleza (Kifungu cha 19), inayohakikisha upatikanaji wa taarifa; haki ya elimu (Kifungu cha 26), inayowezesha uelewa na maamuzi sahihi; na haki ya kupumzika na burudani (Kifungu cha 24), inayotoa muda wa ustawi na kuunganika na wengine. Hata hivyo, vitendo hivi rahisi havipatikani kila mahali.

Sasa nini kifanyike ili kuhakikisha kaulimbiu ya mwaka huu inakuwa hali halisi katika jamii na maisha ya kila mtu  duniani?

Amesisitiza kuwa “Kwa kuziba pengo kati ya kanuni za haki za binadamu na uzoefu wa kila siku, kampeni ya Msingi wa Kila Siku inalenga kuongeza uelewa, kuhamasisha ujasiri na kuhimiza hatua za pamoja. Zaidi ya kuhimiza tafakari, kampeni inatoa nafasi kwa watu kushiriki kile wanachokiona kuwa muhimu katika maisha yao ya kila siku, na kufanya dhana ya muunganiko kuwa halisi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *