
Dar es Salaam. Timu ya Wanawake ya Tanzania chini ya umri wa miaka 15, imetwaa ubingwa wa mashindano ya kuwania kufuzu Fainali za African Schools Football Championship kanda ya CECAFA baada ya leo kuibuka na ushindi wa mikwaju ya penalti 5-4 dhidi ya wenyeji Ethiopia huko jijini Addis Ababa.
Mechi hiyo ililazimika kuamriwa kwa mikwaju ya penalti baada ya dakika 90 za kawaida kumalizika kwa sare tasa.
Matokeo hayo yameifanya timu hiyo kuzoa kitita cha Dola 100,000 kutoka Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF).
Ethiopia ambayo imemaliza katika nafasi ya pili, imejihakikishia kitita cha Dola 75,000 na Uganda iliyomaliza katika nafasi ya tatu imepata Dola 50,000.
Kwa upande wa wanaume, Tanzania imemaliza katika nafasi ya tatu baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 na hivyo imepata kitita cha Dola 50,000.
Bingwa kwa upande wa wanaume ni Uganda na mshindi wa pili ni Ethiopia.
Ikumbukwe timu tatu zilizomaliza katika nafasi za juu kwa wanaume na tatu zilizoongoza upande wa wanawake, zinafuzu kucheza mashindano ya Afrika.
Ikumbukwe Tanzania ni bingwa wa kihistoria wa mashindano ya African Football Schools Championship upande wa wanaume ikiwa imetwaa taji mara mbili.
Kwa upande wa wanawake, Tanzania imetwaa taji hilo mara moja.