Ripoti hiyo iliyopewa jina la chukua hatua sasa kukomesha ukatili dhidi ya wanawake, imebaini kuwa asilimia 41 ya wanawake wameripoti kushambuliwa pia nje ya mtandao kutokana na matusi na manyanyaso ya kidijitali.

Ripoti hiyo mpya iliyotolewa leo Geneva,Uswisi imetayarishwa na Tume ya Ulaya na programu ya UN Women, kwa ushirikiano na watafiti wa TheNerve, City St George’s Chuo Kikuu cha London, Kituo cha Kimataifa cha waandishi wa habari, na kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni  UNESCO.

Ripoti inaonya kuwa ukatili huu unawaondoa wanawake kwenye majukwaa ya mtandaoni na kutishia demokrasia. UN Women inatoa wito kuwepo kwa sheria imara, uwajibikaji kwa kampuni za teknolojia, na ulinzi zaidi kwa wanawake wanaoongoza mijadala ya umma.

Imesema “Bila hatua madhubuti, ukatili wa mtandaoni unahatarisha kuwafukuza wanawake kutoka majukwaa ya kidijitali, na hivyo kudhoofisha demokrasia na uhuru wa kujieleza”.

Ukatili mtandaoni umevuka mipaka

Kwa mujibu wa ripoti ukatili wa mtandaoni sasa unavuka mipaka ya mtandao, wanawake wanne kati ya kumi walioulizwa pia wameripoti kushambuliwa au kudhuriwa nje ya mtandao kutokana na ukatili wa mtandaoni.

Ripoti inabainisha kuwa asilimia 70 ya wanawake walioulizwa wamewahi kukumbwa na ukatili wa mtandaoni katika utekelezaji wa majukumu yao. Aidha, asilimia 41 ya waliojibu wameripoti madhara ya moja kwa moja nje ya mtandao yanayohusiana na ukatili huo wa mtandaoni.

Kwa waandishi wanawake, ripoti inasema uhusiano kati ya ukatili wa mtandaoni na madhara ya nje ya mtandao umeongezeka, kutoka asilimia 20 mwaka 2020 hadi 42 katika utafiti wa mwaka huu.

“Takwimu hizi zinathibitisha kuwa ukatili wa kidijitali si wa kubuni ni ukatili halisi wenye madhara ya kweli katika maisha ya wanawake. Wanawake wanaosimama kutetea haki zetu, wanaoripoti habari au wanaoongoza vuguvugu za kijamii wanalengwa na mashambulizi yanayolenga kuwaaibisha, kuwanyamazisha na kuwatenga kutoka katika mijadala ya umma. Kwa kiwango kinachoongezeka, mashambulizi haya hayamalizikii kwenye skrini  yanafika hadi milangoni mwao. Hatupaswi kuruhusu majukwaa ya mtandaoni kuwa sehemu za vitisho vinavyowanyamazisha wanawake na kudhoofisha demokrasia.” amesema Sarah Hendricks, mkurugenzi wa sera, programu na idara ya masuala ya serikali za nchi wanachama, wa UN Women

Ukatili dhidi ya wanawake unaongezeka zama za AI

Ripoti inaendelea kusema kuwa Takwimu hizi zinaonesha kwamba katika zama za matumizi mabaya ya AI na kuongezeka kwa mifumo kandamizi, ukatili wa mtandaoni dhidi ya wanawake katika maeneo ya umma unaongezeka. Lakini jambo la kutisha zaidi ni ushahidi kuwa madhara ya nje ya mtandao wanayopata waandishi wanawake kutokana na ukatili wa mtandaoni yameongezeka maradufu tangu 2020  ambapo asilimia 42 ya washiriki wa utafiti wa 2025 wametaja mwelekeo huu hatari na wa kutisha,” amesema Profesa Julie Posetti, mkuu wa utafiti na Mkurugenzi wa Information Integrity Initiative ya TheNerve.

Ripoti pia inaonesha kuwa karibu mwanamke mmoja kati ya wanne walioulizwa watetezi wa haki za binadamu, wanaharakati na waandishi wa Habari amepitia ukatili wa mtandaoni unaosaidiwa na teknolojia ya AI, kama vile picha bandia (deepfake) na maudhui yaliyobadilishwa.

Waandishi na watangazaji wa umma kama vile watayarishaji wa maudhui mtandaoni na washawishi, wanaojikita kwenye masuala ya haki za binadamu ndio wanaokumbwa zaidi na ukatili huo, kwa asilimia 30.

Ripoti hii inatolewa wakati dunia inamaliza Siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia, kampeni ambayo mwaka huu imeangazia ukatili wa mtandaoni. Inatoa wito wa sheria na sera madhubuti za kukabili ukatili unaotumia teknolojia, uwajibikaji kwa makampuni ya teknolojia, usalama na msaada kwa watetezi wa haki na waandishi wanawake, pamoja na uwekezaji katika utafiti na takwimu ili kuunda sera zenye ushahidi.

UN Women itafunga kampeni ya Siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia kwa kuzindua mkakati wa shirika wa kuzuia na kukabili ukatili dhidi ya wanawake unaotumia teknolojia.

Mkakati huo utaangazia kuimarisha uwajibikaji, kuziba mapengo ya ushahidi na takwimu, kuharakisha hatua za kuzuia na hatua zinazomweka mhanga katikati, pamoja na kujenga uimara na kuongeza nguvu za vuguvugu za haki za wanawake na viongozi wanawake.

Kuhusu ACT

Programu ya uhamasishaji, kujenga ushirikiano na kuleta mabadiliko yah atua za kijinsia (ACT) ni ushirikiano wa kimkakati kati ya Tume ya Ulaya na UN Women kama viongozi wenza wa Muungano dhidi ya Ukatili wa Kijinsia (GBV), kwa ushirikiano na Mfuko wa Umoja wa Mataifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake.

Ajenda ya pamoja ya ACT inatoa kipaumbele kwa sauti za vuguvugu za kupigania haki za wanawake na kutoa mfumo wa pamoja wa ushirikiano unaolenga vipaumbele, mikakati na hatua za pamoja.

Kuhusu UN Women

UN Women ipo ili kuendeleza haki za wanawake, usawa wa kijinsia na uwezeshaji wa wanawake na wasichana. Kama chombo kikuu cha Umoja wa Mataifa kuhusu usawa wa kijinsia, tunabadilisha sheria, taasisi, tabia za kijamii na huduma ili kupunguza pengo la kijinsia na kujenga dunia iliyo sawa kwa wanawake na wasichana.

Tunahakikisha haki za wanawake na wasichana zipo katikati ya maendeleo ya dunia kila wakati, kila mahali. Kwa sababu usawa wa kijinsia si tu kile tunachokifanya, ndicho tulicho.

Kuhusu Information Integrity Initiative

Information Integrity Initiative ni mradi mpya wa TheNerve, maabara ya uchunguzi wa kimitandao iliyoanzishwa na mshindi wa Tuzo ya Nobel, Maria Ressa.

Mradi huu unaongoza utafiti unaolenga hatua katika makutano ya jinsia, upotoshaji wa taarifa, uhuru wa kujieleza na vyombo vya habari vinavyolinda maslahi ya umma.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *