Akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva kwa njia ya video kutoka katika eneo lililoharibiwa vibaya na vita huko Gaza, Meneja wa Mawasiliano wa UNICEF Tess Ingram amesema kuwa takriban watoto 165 wameripotiwa kufa, vifo vya maumivu, ambavyo vingezuilika vinavyohusiana na utapiamlo wakati wa vita kati ya wapiganaji wa Hamas na Israel.
Msichana mdogo huko Gaza anachunguzwa utapiamlo.
Ameendelea kusema kuwa Janga lisilotambulika sana ni njaa kali miongoni mwa wanawake wajawazito na wanaonyonyesha na athari mbaya ya mnyororo wa ukosefu huu wa lishe bora kwa maelfu ya watoto wachanga.
“Katika hospitali za Gaza nimekutana na watoto wachanga kadhaa waliokuwa na uzito wa chini ya kilo moja, vifua vyao vidogo vikivuta hewa kwa nguvu ili kuendelea kuishi,” amesema Bi. Ingram.
Kuzaliwa katika mazingira hatari
Bi. Ingram ameeleza kwamba watoto wanaozaliwa na uzito mdogo wako kwenye hatari ya kufa kwa kiwango cha mara 20 zaidi kuliko wale wanaozaliwa na uzito wa kawaida.
Msemaji huyo wa UNICEF meibainisha kuwa kabla ya vita mwaka 2022, wastani wa watoto 250 kwa mwezi sawa na asilimia tano walizaliwa wakiwa na uzito chini ya kilo 2.5 kulingana na Wizara ya Afya ya Gaza.
Katika nusu ya kwanza ya mwaka 2025, hata kama kulikuwa na watoto wachache waliozaliwa, kiwango hicho kilipanda hadi asilimia 10 ya watoto wote, yani takribani watoto 300 kwa mwezi, na kufikia 460 kwa mwezi katika miezi mitatu kabla ya kusitishwa kwa mapigano.
Hiyo ni sawa na watoto 15 kwa siku karibu mara mbili ya kiwango cha kabla ya vita.
“Uzito mdogo wakati wa kuzaliwa mara nyingi unasababishwa na lishe duni ya mama, msongo wa mawazo wa mama na ukosefu wa huduma za kliniki,” Bi. Ingram ameeleza.
“Katika Ukanda wa Gaza, tunashuhudia mambo yote matatu, na hatua za kusaidia haziendi kwa kasi inayohitajika wala kwa kiwango kinachohitajika.”
Mkunga kutoka Khan Younis akiwasaidia wanawake wajawazito kutoka kwa hema aliloweka katika eneo la Mawasi.
Hali halisi ya athari za vita
Msemaji huyo ameongeza kuwa mwezi Oktoba pekee, wanawake 8,300 wajawazito na wanaonyonyesha walilazwa kwa matibabu ya utapiamlo mkali, “katika eneo ambalo awali hakukuwa na utapiamlo wa aina hii miongoni mwa kundi hili kabla ya Oktoba 2023.”
Ameongeza kuwa “Mtindo huu ni onyo zito na huenda ukasababisha watoto wachanga wenye uzito mdogo kuzaliwa katika Ukanda wa Gaza kwa miezi ijayo. Hili bado halijaisha.”
Umoja wa Mataifa unakabiliana na hii mbaya kwa kubadilisha mashine za joto, mashine za kupumulia na vifaa vingine vya kuokoa maisha vilivyoharibiwa wakati wa mapigano.
UNICEF pia imetoa virutubisho kwa makumi ya maelfu ya wanawake wajawazito na wanaonyonyesha ili kuzuia utapiamlo, kuchunguza watoto wadogo kwa utapiamlo mkali na kuwaingiza kwenye matibabu.
Lakini ili kuboresha hatua, msaada zaidi unahitajika kuingia haraka katika Ukanda wa Gaza.
Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu na misaada ya Dharura OCHA imesema Jumatatu wiki hii kwamba “vikwazo vya kudumu kufikia walio hatarini zaidi ni pamoja na ukosefu wa usalama, changamoto za ukaguzi wa forodha, ucheleweshaji na kukataliwa kwa shehena mipakani”.
Timu za misaada pia zimesema njia zilizopo za kusafirisha misaada ndani ya Ukanda wa Gaza ni chache sana.
Mwanamke akiwa na watoto wake kaskazini mwa Gaza anasema “maisha ya hapa ni magumu na ya kusikitisha.”
Wito kuhusu mpaka wa Rafah
Kufungua mpaka wa Rafah kusini mwa Gaza kunaweza kusaidia kuongeza idadi ya malori ya misaada na kupunguza idadi ya watoto wenye utapiamlo, amesema Bi. Ingram.
“Tunahitaji kuona aina zote za misaada zikiingia, hasa chakula chenye lishe kupitia njia za kibiashara pia,” ameongeza, akisisitiza kuwa masoko ya ndani yanahitaji kujazwa bidhaa zaidi za kibiashara ili bei ishuke na bidhaa kama matunda, mboga, nyama na maziwa familia ziweze kumudu.
Msemaji wa UNICEF amesisitiza kuwa kusitishwa kwa mapigano kwa miezi miwili “kunapaswa kutoa usalama kwa familia, si hasara zaidi,” akisema kuwa zaidi ya watoto 70 wameuawa tangu tarehe 10 Oktoba.
“Vizazi vya familia, wakiwemo wanaozaliwa sasa wakati wa kusitishwa kwa vita hivi, vimebadilika milele kutokana na kile walichofanyiwa,” amesema Bi. Ingram, akisisitiza kuwa anaona na kusikia athari za vizazi vya vita kwa mama na watoto “karibu kila siku hospitalini, katika kliniki za lishe, na kwenye mahema ya familia. Ni kitu ambacho hakionekani kama damu na majeraha, lakini kiko kila mahali,”
Bi. Ingram amesisitiza kuwa athari za mnyororo kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto, madhara ya utapiamlo, msongo wa mawazo na kukoseshwa makazi kwa wanawake wajawazito na watoto wao yalipaswa na yangeweza kuzuilika.
“Hakuna mtoto anayepaswa kuchafuliwa na vita kabla hata kabla ya kupumua mara ya kwanza,” amesema, “akionesha ukweli mchungu wa mgogoro na vizuizi vya misaada vinavyowekwa na Israel, ambavyo vimesababisha upungufu wa vifaa hospitalini na kuwaletea njaa na msongo wa mawazo akina mama.”
Amehitimisha tarifa yake akisema “Maumivu na machungu mengi sana yangeweza kuepukika kama sheria za kimataifa za kibinadamu zingeheshimiwa”