Ujenzi wa barabara ya Iringa kuelekea Hifadhi ya Taifa ya Ruaha umetajwa kuwa kichocheo cha kuimarisha shughuli za utalii ndani ya hifadhi hiyo, huku ukifungua fursa za kiuchumi kwa wananchi wanaoishi pembezoni mwa Ruaha.
Miundombinu hiyo inatarajiwa kuongeza urahisi wa ufikikaji, kuvutia wawekezaji na kuongeza mzunguko wa fedha katika jamii zinazozunguka hifadhi.
Wananchi wa Kijiji cha Kidodi Mkoani Iringa wamesema maboresho ya barabara hiyo kwa kiwango cha Lami ni hatua inayowapa matumaini mapya ya kunufaika na utalii, ikiwemo kuwekeza katika biashara za vyakula vya asili, mavazi ya kitamaduni na bidhaa za urembo zinazotambulisha utamaduni wa eneo hilo.
Kwa upande wake, Afisa Uhifadhi Mkuu – Kitengo cha Utalii katika Hifadhi ya Taifa Ruaha, Amina Rashid, amesema ujenzi wa barabara hiyo utarahisisha upatikanaji wa huduma za utalii, kuongeza idadi ya watalii wanaotembelea Ruaha na kuvutia wawekezaji zaidi kuwekeza katika shughuli za uhifadhi na utalii.
#StarTvUpdate