
Angalau watu 74, wengi wao wakiwa raia, wameuawa na 83 kujeruhiwa kutokana na mapigano ya karibuni mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa na mratibu wa misaada wa Umoja wa Mataifa nchini humo jioni ya Jumatatu.
Mapigano kati ya vikosi vya DRC na waasi wa M23 kati ya Desemba 2 na 7, yalijumuisha matumizi ya silaha nzito na mashambulizi ya maroketi katika maeneo yenye watu wengi, yaliathiri wilaya za Uvira, Walungu, Mwenga, Shabunda, Kabare, Fizi, na Kalehe, katika mkoa wa Kivu Kusini.
Taarifa mpya inaonyesha kuwa mapigano haya pia yamesababisha zaidi ya watu 200,000 kukimbia makwao tangu Desemba 2, huku maelfu wengine wakikimbilia nchi jirani, ikiwemo Burundi na Rwanda.
Hayo yanajiri katika mkoa ambao tayari una idadi ya watu milioni 1.2 waliokimbia makwao, kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa.
Katika taarifa, mratibu wa misaada wa Umoja wa Mataifa nchini DRC, Bruno Lemarquis, aliitaka kulindwa mara moja idadi ya watu wa kiraia.
Mapigano haya hata yamezuia misaada ya matibabu. Lemarquis aliziomba pande zote za mzozo kuheshimu majukumu yao chini ya sheria za kimataifa za kibinadamu.
Taarifa ya Umoja wa Mataifa imetolewa baada ya Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Félix Tshisekedi, kuituhumu Rwanda kwa kukiuka makubaliano ya ‘amani’ yaliyosimamiwa na Marekani na kutiwa saini wiki iliyopita mjini Washington DC.
Makubaliano hayo, yaliyosimamiwa na Rais Donald Trump, yamekosolewa vikali na wachambuzi wengi wanaosema yamelenga zaidi kurahisisha uhamishaji wa madini adimu kutoka mashariki mwa DRC kuliko kuleta amani ya kweli katika eneo hilo. Trump mwenyewe amesema baada ya mapatano hayo makampuni ya kiteknolojia ya Marekani yataweza kuchimba madini ya DRC, jambo linaloweka wazi nia yake ya kupora madini ya nchi hiyo.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Burundi, Edouard Bizimana, ametuhumu Rwanda kwa kuendeleza “harakati za kuvuruga usalama” mpakani na DRC. Amesisitiza kuwa majeshi ya Burundi yaliyotumwa mashariki mwa DRC hayataondoka hadi “jukumu lao litakapokamilika kikamilifu.” Takribani askari 15,000 wa Burundi wameripotiwa kuwa mashariki mwa DRC wakisaidia jeshi la nchi hiyo kupambana na waasi.