
Dar es Salaam. Wakati beki wa kulia Yao Kouassi akirejea uwanjani muda mfupi kabla ya kufunguliwa kwa dirisha dogo la usajili Tanzania, uongozi wa Yanga umewapa watu wawili kibarua cha kuamua kama beki huyo aingizwe katika usajili wao au la.
Beki huyo hayupo katika orodha ya nyota 12 wa kigeni wa Yanga ambao walisajiliwa katika dirisha kubwa la usajili kabla ya msimu kuanza lakini linaweza kuingizwa katika dirisha dogo ikiwa mchezaji mmoja wa kigeni atapunguzwa.
Ofisa Habari wa Yanga, Ally Kamwe amewataja watu hao kuwa ni Kocha Mkuu, Pedro Goncalves na Kocha wa Utimamu wa miili, Chyna Mokaila.
“Kwasi Attohoula Yao tunachosubiri sasa hivi ni ripoti kutoka kwa kocha wa utimamu wa mwili. Mchezaji ambaye ametoka kwenye majeraha ni ngumu mno kumakadiria kwamba akishapona atarudi. Ikituambia kwamba mchezaji huyu amekamilika kwa asilimia mia, mwalimu atakuwa na namna yake ya kumchunguza Yao kuangalia ubora wake umefika wapi.
“Halafu yeye anatugea sisi mapendekezo yake kwamba sasa hivi mnaweza kumuingiza kwenye usajili, nitamtumia. Amefika kwenye kiwango anachohitaji yeye tumuingize kwenye usajili au tumuache aendelee kufanya naye mazoezi au tumtoe kwa mkopo apate muda wa kucheza. Yote yanaweza kutokea hayo,” amesema Kamwe.
Katika hatua nyingine, Kamwe amesema kuwa tayari wameanza kufanyia kazi ripoti ya usajili wa dirisha dogo ambao ametamba kuwa wataukamilisha mapema.
“Dirisha dogo litafunguliwa mwezi wa kwanza. Mashabiki wetu, wanachama wetu wamekuwa wakiuliza sana kuhusu dirisha dogo la usajili. Kimuundo, Yanga inafanyia kazi ripoti ya benchi la ufundi. Kimuundo, ripoti ya usajili anayo mwalimu Pedro.
“Kuiweka hiyo sawa, tayari ripoti yake ameshaiwasilisha katika ofisi ya Mtendaji Mkuu. Ameshawasilisha maeneo ambayo anahisi tunatakiwa tuyaboreshe na wachezaji ambao anaamini tunatakiwa tuwatoe kwa mkopo wakapate changamoto sehemu nyingine.
“Uzuri sisi hatusajili kwa mihemko. Kama nafasi ipo, taratibu zinaturuhusu, mchezaji huyo labda tushazungumza naye ameshasaini mkataba wa awali, tutamuingiza tu kwenye usajili,” amesema Kamwe.
Kamwe pia amefichua kwamba wachezaji wawili wa timu hiyo ambao wanakabiliwa na majeraha, Clement Mzize na Mudathir Yahya, watarejea uwanjani mwishoni mwa Januari.