Dar es Salaam. Msanii mahiri wa muziki wa kizazi kipya Amini Mwinyimkuu, ambaye amewahi kutamba na wimbo unaokwenda kwa jina la Robo Saa, amesema mashabiki wake wasubiri kazi zake mpya kali zinakuja.
Akizungumza na Mwananchi, Amini alisema amekuwa kimya kwa muda mrefu, kutokana na sababu mbalimbali ikiwa ni pamoja na kusoma mwelekeo wa muziki kutoka kwa wasanii wapya.
Amini alisema mara baada ya kukamilisha harakati zake hizo, kwa sasa ameanza maandalizi ya kuanza kujitangaza upya kwa kuja na tungo zake mpya ambapo kwa sasa anaendelea kuzirekodi.
“Sipendi kuongea kwa sasa kwa kuwa sijakamilisha yale ambayo, ninayafanya, lakini napenda kuwajulisha mashabiki wangu kwamba nipo na nakuja na kazi mpya, nilikuwa nikisoma nyakati.”
Amini alielezea uzoefu alionao katika fani hiyo, utampa nafasi ya kufanya kazi zilizo na kiwango cha juu, kutokana na kipaji kikubwa cha kisanii alionacho katika muziki huo.
Aidha, akizungumzia hali ya muziki huo nchini kwa sasa, alisema sanaa imebadilika katika sehemu mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kuingia kwa wasanii wenye vipaji vikubwa kitu ambacho kimesaidia kuleta ushindani.
Amini aliwahi kutamba na vibao vyake kama Ni Wewe, Asante na Bado Robo Saa.