
Natumai mu buheri wa afya wasikilizaji wapendwa wa Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Katika makala ya wiki tunachunguza mada ambayo huteka hisia za kila msikilizaji: Ukatili dhidi ya wanawake nchini Ujerumani, nchi yenye watu wengi zaidi katika Umoja wa Ulaya.
Tunachunguza vitendo vya udhalilshaji na ukatili wa majumbani dhidi ya wanawake katika nchi za Ulaya kama vile Ujerumani, na kwa kutegemea takwimu rasmi na ripoti za polisi, makala yetu hii inaonyesha kuwa hata katika nchi zinazodai kulinda haki za wanawake, vitendo vya kuwanyanyasa vingalipo na vinatia wasiwasi, suala ambalo linaathiri sio familia tu, bali pia jamii nzima. Kuhusiana na suala hili, ripoti ya hivi karibuni ya Ofisi ya Polisi ya Uhalifu ya Shirikisho la Ujerumani, BKA imetoa takwimu ambazo ni za kutisha sana.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, mwaka jana pekee, watu 266,000 walikuwa wahanga wa vitendo vya ukatili wa majumbani. Takwimu hiyo inaonyesha ongezeko la asilimia 3.8 ikilinganishwa na mwaka uliopita, na ni rekodi mpya katika historia ya sasa ya Ujerumani.
Takwimu hizi ni sehemu ndogo na ya wazi tu ya vitendo vya ukatili wanavyofanyiwa wanawake huko Ujerumani, kwa sababu utafiti unaonyesha kuwa ni asilimia tano tu ya kesi za ukatili wa majumbani zinazoripotiwa kwa polisi. Hii ina maana kwamba, sehemu kubwa ya uukatili huo bado imefichwa. *****
Karin Prien Waziri wa Familia wa Ujerumani ametahadharisha katika mkutano na waandishi wa habari kwamba katika kila saa moja, wanawake 15 wanakuwa wahanga wa vitendo vya utumiaji mabavu vya waume zao. Kwa maana kwamba, wanawake zaidi ya 360 kila siku hukumbana na vitendo vya unyasasaji nchini humo.
Ukatili wa majumbani hauwaathiri tu wanawake, bali watoto na hata wanaume pia ni wahanga wa vitendo hivyo. Hata hivyo takwimu zinaonyesha kuwa wahanga wengi ni wanawake, yaani karibu asilimia 70 ya waathiriwa wote. Hii ni katika hali ambayo, ukatili ndani ya familia – kati ya wazazi, watoto au wanafamilia kwengine- umeongezeka kwa kiwango cha juu kuliko ukatili wa wenzi wa ndoa, hususan ule unaoathiri watoto wa miaka 6 hadi 14.
Holger Munch, mkuu wa Ofisi ya Polisi ya Jinai ya Ujerumani anasema: “Idadi ya uhalifu dhidi ya wanawake inaongezeka mara kwa mara na tunachokishuhudia ni ncha tu ya barafu.”
Hii ni ncha ya barafu, ndiyo hiyo sehemu ndogo inaripotiwa kwa polisi. Sehemu kubwa ya ukatili wa majumbani bado imefichwa au kunyamaziwa kimya. Hofu, aibu, au utegemezi wa kiuchumi huzuia waathiriwa kuripoti mateso na ukatili wanaokumbana naoa.
Ofisi ya Polisi ya Jinai ya Ujerumani pia imeeleza masuala mbalimbali ya kijamii na kiuchumi kuwa yanachangia ongezeko la ukatili wa majumbani. Mambo hayo ni pamoja na ukosefu wa ajira, kuongezeka uhalifu, uhaba wa makazi na mashinikizo ya kiuchumi.
Hata hivyo, ukatili dhidi ya wanawake sio tu suala la kiuchumi. Mitazamo ya kitamaduni na ya kibaguzi dhidi ya wanawake pia ina nafasi muhimu. Imani za jadi ambazo wakati mwingine hata zinaakisiwa katika vyombo vya habari huwafanya wanawake wengi kunyamaza kimya. *********
Alexander Dobrindt, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Ujerumani amekiri kuwa: “Tunapasa kufanya juhudi kubwa ili kulinda wanawake dhidi ya vitendo vya ukatili.” Matamshi haya yanaonyesha kuwa ukatili wa majumbani ni changamoto ya kitaifa na kiusalama, na si tatizo la kifamilia tu.
Vitendo vya ukatili na utumiaji mabavu vinavyofanyika majumbani pamoja na kuwadhuru moja kwa moja waathiriwa, vina taathiri nyingi za kijamii. Kupungua kwa tija, matatizo ya elimu ya watoto, gharama za matibabu na shinikizo kwenye mfumo wa haki ni baadhi tu ya matokeo ya jambo hili.
Watoto wanaoshuhudia ukatili nyumbani, hata kama hawajadhurika moja kwa moja, lakini hupata matatizo ya kisaikolojia na kitabia, na suala hilo huzidisha uwezekano wa kuendelea kwa mzunguko wa ukatili katika kizazi kijacho. Waathirika wanawake nao, pamoja na madhara ya kimwili na kisaikolojia wanayopata, pia hupoteza fursa nyingi za kiuchumi na kijamii. Vizuizi hivi huathiri uhuru na uwezo wao. *********
Serikali ya Ujerumani imechukua hatua kadha wa kadha ili kukabiliana na mgogoro huu. Mojawapo ya hatua muhimu zaidi ni kuidhinishwa sheria mpya inayowalazimisha wahusika wa ukatili wa majumbani kupachikwa lebo za kielektroniki ya unyanyasaji. Hatua hii imeratibiwa kwa mujibu wa mtindo uliofaulu wa Uhispania na inaruhusu polisi na mahakama kuendelea kuwafuatilia wahusika na vitendo hivyo vya mabavu majumbani, na kuwalinda waathirika.
Wizara ya Masuala ya Familia na Wizara ya Mambo ya Ndani pia zimeweka katika ajenda yao ya kazi programu za elimu na upashaji, kampeni za vyombo vya habari, simu za dharura, mafunzo ya ujuzi wa kukabiliana na vitendo vya mabavu na ushauri wa kisheria.
Pamoja na hayo, weledi wa mambo wanasisitiza kuwa sheria pekee haitoshi. Bali upo umuhimu wa kubadili mitazamo ya kitamaduni, kupatikana msaada wa kijamii, kutoa makazi salama na fursa za kiuchumi kwa wanawake.
Ripoti za ndani zinaonyesha kuwa miji mikubwa ya Ujerumani kama Berlin, Munich na Hamburg ina kiwango cha juu sana cha matukio ya ukatili majumbani. Katika maeneo hayo, mashinikizo ya kiuchumi na uhaba wa nyumba vimezidisha hali ya mivutano katika familia.
Kituo cha Usaidizi mjini Berlin kimearifu kuwa mwaka jana, kilipokea simu za dharura zaidi ya 10,000 zilizopigwa na wanawake. Aghlabu ya wanawake hao wamekuwa wakikabiliwa na ukatili kwa miezi au hata miaka, na wamekaa kimya kwa hofu au kutokana utegemezi. Hii inaonyesha kuwa takwimu hizi rasmi ni sehemu ndogo tu ya uhakika wa mambo, na kwamba sehemu kubwa ya ukatili wa nyumbani bado imefichwa.
************
Vyombo vya habari na asasi za kiraia zina jukumu muhimu katika kupambana dhidi ya vitendo vya ukatili na unyanyasaji. Kutoa taarifa, kuongeza ufahamu wa umma, kuwasaidia waathiriwa na kushinikiza maafisa husika ili kutekeleza sheria, yote haya yanaweza kuzaa matunda na kuwa na taathira.
Wakati huo huo wanaharakati wa kijamii na mashirika yasiyo ya kiserikali nchini Ujerumani yanaendesha kampeni za kupambana na vitendo vya mabavu na ukatili wa majumbani, kutoa mafunzo ya ujuzi wa kujilinda, kuanzisha makazi ya dharura na kutoa ushauri wa kisheria bila malipo.
Mitandao ya kijamii pia imekuwa chombo muhimu cha usaidizi kwa wahanga wa vitendo vya mabavu.. Kupitia mitandao hiyo, wanawake wanaweza kufikia rasilimali wanazohitaji na kufaidika kutokana na uzoefu wa wengine. *********
Pamoja na jitihada zote hizi, changamoto bado zipo; vikwazo vya rasilimali, ukosefu wa maeneo salama, upinzani wa baadhi ya familia kupokea ushauri nasaha, na mitazamo ya kitamaduni vyote vinakwamisha kasi ya kupungua vitendo hivyo vya ukatili.
Ukatili wa majumbani ni jambo chungu na la kweli linaloathiri maisha ya maelfu ya wanawake na watoto. Mnamo mwaka 2024, uvitendo vya ukatili wa majumbani ulisababisha vifo vya watu 286, wanaume walikuwa 95 na wanawake 191 yaani zaidi ya theluthi mbili ya wahanga walikuwa wanawake.
Takwimu hizi za kutisha ni wito unaoiamsha jamii na viongozi husika katika jamii za Ulaya. Nchi hizi hizo za Ulaya, ikiwa ni pamoja na Ujerumani zimekuwa zikijidhihirisha kama watetezi wa haki za wanawake na kwamba zina sheria za juu za kuwalinda na kuwahami.
Hata hivyo, takwimu za ukatili dhidi ya wanawake katika nchi hizo hizo zinavunja rekodi kila mwaka, jambo linaloonyesha namna ukweli wakati mwingine ulivyo mbali na madai yanayotolewa na nchi hizo za Ulaya.
Kwa hiyo, ni wazi kuwa haki za kisheria pekee hazitoshi; bali kubadilisha mitazamo ya kitamaduni, usaidizi halisi wa kijamii na kuchukuliwa hatua za kivitendo ndiyo njia pekee ya kuondokana na janga hili na kuwalinda wanawake ipasavyo.
Makala yetu inaishia hapa kwa leo. Asanteni kwa kutegea sikio. Kwaherini.