
Mbeya. Kocha Mkuu wa Mbeya City, Mecky Maxime ameanza kazi ya kusuka upya timu hiyo ambapo amependekeza kusajiliwa kwa wachezaji watano katika dirisha dogo lijalo la usajili.
Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano ya Mbeya City, John Jerome amesema tayari wamepokea ripoti ya Maxime kuhusu mahitaji yake ya usajili na uongozi wa timu hiyo umeanza kuifanyia kazi.
“Amehitaji kuongeza nguvu maeneo matatu, beki, kiungo na straika. Lakini amewataja mastaa anaowataka na sisi uongozi tunafanyia kazi ripoti hiyo ili kufikia malengo.
“Ni kweli wachezaji wanaohitajika wote wana mikataba na timu zao. Kinachoenda kufanyika ni kuvunja kibubu kuwapata nyota hao ambao tunaamini wataturejeshea heshima yetu kuanzia mechi zijazo,” alisema Jerome.
Habari kutoka chanzo cha uhakika ndani ya Mbeya City, zimefichua kwa gazeti hili kuwa miongoni mwa wachezaji ambao Maxime anawahitaji ni Ladack Chasambi na Awesu Awesu wa Simba.
Inaripotiwa kwamba uongozi wa Mbeya City umeanza kufanya mawasiliano na Simba ili kuwapata wachezaji hao kwa mkopo kwa vile mikataba yao ya kuitumikia Simba inaendelea hadi msimu ujao.
Mbeya City inashika nafasi ya 13 katika msimamo wa Ligi Kuu ikiwa na pointi nane ambazo imekusanya katika michezo 10, ikishinda miwili, kutoka sare mbili na kupoteza mechi sita.