Rais Masoud Pezeshkian wa Iran amevitaja vitendo vya Marekani dhidi ya Venezuela kuwa ni uzushi hatari unaotishia amani na usalama wa dunia.
Katika mazungumzo yao ya simu jioni ya Jumanne wiki hii, Rais Pezeshkian na mwenzake wa Venezuela, Nicolas Maduro walibadilishana mawazo kuhusu ushirikiano wa pande mbili na kujadili matukio ya hivi karibuni katika eneo la Karibi. Rais Masoud Pezeshkian wa Iran amekosoa na kulaani waziwazi vitendo haramu vya Marekani katika eneo la Karibi, akisema: “Kitendo cha serikali ya Marekani cha kutuma meli za kivita huko Karibi na pwani ya Venezuela, kwa visingizio vya uwongo, ni haramu, ukiukaji wa sheria za kimataifa na ni uzushi hatari unaotishia amani na usalama wa dunia.” Amesisitiza kuwa Jamhuri ya Kislamu inalaani vikali vitendo hivyo.
Rais Pezeshkian amesema: “Iran inaiona Venezuela kama rafiki na mshirika wa kweli na inaiunga mkono katika hali zote, hasa katika hali nyeti ya sasa.”
Kwa upande wake, Rais wa Venezuela ameashiria mvutano unaoendelea katika eneo la Karibi na kusema, vitendo vya Marekani ni “vya uchochezi, visivyo vya lazima na kinyume na Mkataba wa Umoja wa Mataifa.” Amesema: “Madai ya uongo ya Marekani dhidi ya watu watukufu wa Venezuela yamepingwa na maoni ya umma duniani, na hata ndani ya Marekani kwenyewe…”
Rais Maduro ameisisitiza haja ya kuwepo umoja, mshikamano na azma ya watu wa Venezuela ya kutetea amani, uhuru na kukabiliana na uongo wa Marekani, na kusema: “Nina uhakika kwamba watu wa Venezuela hii leo wana nguvu na umoja zaidi kuliko ilivyokuwa hapo awali, na wanajiandaa zaidi kila siku kwa ajili ya kudumisha amani na kupata ushindi; tutaendelea na njia ya ustawi na maendeleo.”
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekuwa ikilaani sera za kujichukulia maamuzi ya upande mmoja na kuingilia kati masuala ya nchi nyingine za Marekani dhidi ya nchi huru na zinazojitawala na kuziona kuwa ni kinyume na kanuni za sheria za kimataifa na Mkataba wa Umoja wa Mataifa. Katika muktadha huu, sera za Washington dhidi ya Venezuela, hasa kutuma wanajeshi karibu na nchi hiyo katika Bahari ya Karibi, na tishio la mashambulizi ya kijeshi ya nchi kavu dhidi ya Venezuela, zinatambuliwa na Jamhuri ya Kiislamu kuwa ni ukiukaji wa wazi wa mamlaka ya kitaifa ya nchi huru na uzushi hatari unaotishia amani na usalama wa dunia. Tehran inaamini kwamba, vitisho vya kijeshi, vikwazo vya kiuchumi, mashinikizo ya kisiasa na majaribio ya kubadilisha utawala kutoka nje haviwezi kutatatua matatizo ya ndani ya Venezuela, bali kinyume chake, vitazidisha mgogoro wa binadamu na ukosefu wa utulivu wa kikanda.
Kwa mtazamo wa Iran, Marekani, ikitumia dhana za haki za binadamu na demokrasia kama chombo, inataka kudhibiti rasilimali za nishati za Amerika Kusini na kuimarisha nafasi yake kijiografia na kisiasa. Venezuela, ikiwa moja ya nchi zenye akiba kubwa zaidi ya mafuta duniani, imekuwa ikilengwa kwa sera za utawala wa Washington. Mtazamo wa sasa wa Washington kuhusu Venezuela unafanana na mienendo ya Marekani katika eneo la Magharibi mwa Asia, ambayo, chini ya kaulimbiu ya kuunga mkono uhuru na haki za binadamu, inafuatilia maslahi yake haramu ya kiuchumi na kisiasa. Sera kama hiyo siyo tu kwamba si halali, lakini pia inadhoofisha sana imani ya mataifa ya dunia kwa mfumo wa kimataifa.
Iran pia inasisitiza kwamba vikwazo vya kiuchumi dhidi ya Venezuela, kama vilivyo vikwazo ambavyo Iran yenyewe inakabiliana navyo kwa miaka mingi, vinasababisha madhara makubwa kwa raia wa kawaida. Vikwazo hivi vinawazuia watu kupata dawa, chakula na mahitaji ya msingi, na hatimaye kuzidisha mgogoro wa binadamu. Hatua za aina hii ni mfano wa wazi wa “adhabu ya pamoja,” ambayo imepigwa marufuku kwa mujibu wa sheria za kimataifa. Kwa msingi huo, Tehran inapingi sera hizo na kuziona kama tishio kwa dhamiri ya mwanadamu na kanuni za maadili za dunia.
Katika ngazi ya kisiasa, Iran inaamini kwamba jaribio la Marekani la kutaka kuondoa madarakani serikali nchini Venezuela kwa kutumia nguvu linakiuka kanuni ya kutoingilia mambo ya ndani ya nchi nyingine. Kanuni hii ni mojawapo ya misingi ya mahusiano ya kimataifa, na kuipuuza kunaweza kusababisha kuporomoka kwa mfumo wa kimataifa.
Wakati huo huo, Tehran inasisitiza umuhimu wa kuwepo mshikamano miongoni mwa nchi huru na zinazojitawala katika kukabiliana na sera za kujichukulia maamuzi ya upande mmoja za Marekani. Ushirikiano miongoni mwa mataifa na serikali ambazo ni wahanga wa vikwazo na mashinikizo ya kigeni unaweza kuwa njia nzuri ya kukabiliana na mwenendo huu hatari. Katika miaka ya hivi karibuni, Iran na Venezuela zimekuwa na uhusiano wa karibu, na ushirikiano huo ni nembo ya Muqawama na kusimama kidete dhidi ya tawala za kigeni. Miungano kama hiyo inaonyesha kwamba nchi mbalimbali zinaweza kukabiliana na mashinikizo ya nje kwa kutegemea uwezo wao wa ndani na ushirikiano wa pande zote.
Mwishoni tunasema kuwa, mtazamo wa Iran kuhusu mienendo ya Marekani dhidi ya Venezuela unategemea kanuni kwamba usalama na amani ya dunia vinaweza kulindwa wakati nchi zote zinafuata kanuni za sheria za kimataifa, kuheshimu mamlaka ya kitaifa ya kujitawala na kutoingilia mambo ya ndani ya nchi nyingine. Iran pia inaonya kwamba kuendelea sera za Marekani za kujichukulia maamuzi ya upande mmoja, hasa tishio la mashambulizi ya kijeshi dhidi ya nchi hiyo yenye utajiri wa mafuta ya Amerika Kusini, kutazidisha ukosefu wa amani na utulivu katika eneo la Karibi na Amerika Kusini kwa ujumla. Jambo hilo pia linaweza kuwa mfano mbaya na hatari kwa maeneo mengine ya dunia. Uzushi huu, ikiwa hautadhibitiwa, unaweza kusababisha ukosefu wa utulivu na kuwa tishio kubwa kwa amani na usalama wa kimataifa.