
Marekani imependekeza kwamba Ukraine ijiondoe kutoka eneo la Donetsk mashariki mwa nchi na kuunda “eneo maalum la kiuchumi” katika maeneo ambayo inayadhibiti kwa sasa, Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amesema.
Imechapishwa:
Dakika 3 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Rais Zelensky amebainisha kwamba eneo na udhibiti wa mtambo wa nyuklia wa Zaporizhzhia unabaki kuwa hoja kuu mbili za mzozo katika mpango wa amani uliopendekezwa kwa Ukraine.
Wakati wa mkutano na waandishi wa habari, Rais Zelensky amezungumzia nia ya Marekani ya kukomesha haraka mzozo huo, ugumu wa mazungumzo yanayoendelea, na imani yake kwamba Urusi haina nia ya kukomesha vita.
Ukraine imewasilisha mpango uliosasishwa wa pointi 20 kwa Marekani, pamoja na hati tofauti kuhusu dhamana za usalama na vifungu vya ujenzi wa nchi hiyo, Zelensky amesema.
Pendekezo hili linafuatia wiki kadhaa za shughuli kali za kidiplomasia, ambapo mipango mingi ya amani iliandikwa, kuwekwa sawa, na kurekebishwa na Marekani, Ukraine, Urusi, na viongozi wa Ulaya.
“Hatua ya mwisho ndiyo ngumu zaidi. Kila kitu kinaweza kuanguka kwa sababu nyingi,” Zelensky amesema siku ya Alhamisi.
Urusi inaitaka Ukraine iachilie udhibiti wa takriban 30% ya eneo la Donetsk mashariki mwa Ukraine, ambalo bado inalimiliki. Ukraine inakataa kufanya hivyo, kwa kanuni na kwa hofu ya kuipa Moscow nafasi ya uvamizi wa siku zijazo.
Kulingana na Zelensky, Marekani sasa inafikiria suluhisho linalohusisha uondoaji wa vikosi vya Ukraine kutoka baadhi ya sehemu za Donetsk na kujitolea kutoka kwa vikosi vya Urusi kutoingia katika eneo hilo. Eneo hili litakuwa “eneo maalum la kiuchumi” au “eneo lisilo na kijeshi,” ameelezea.
Hata hivyo, amesisitiza kwamba uondoaji wa upande mmoja wa Ukraine hautakuwa wa haki na kwamba Urusi pia inapaswa kujiondoa kwa umbali sawa.
“Ni nini kitakachoizuia Urusi kusonga mbele? Au kujipenyeza ikiwa imejificha kama raia?” ameuliza.
Zelensky alisema haya yalikuwa “mawazo makubwa sana” na kwamba Ukraine inaweza kukataa pendekezo hilo, huku ikiacha mlango wazi kwa uchaguzi au kura ya maoni ili kuwapa nafasi raia wa Ukraine kuweza kuamua.
Hata hivyo, amekiri kwamba mapigano yataendelea na bado yanaweza kuathiri mustakabali wa mazungumzo: “Mengi yanategemea vikosi vyetu vya kijeshi: wanachoweza kufanya, wapi wanaweza kumzuia adui, wanachoweza kuharibu. Hii inaathiri mpangilio mzima wa shughuli.”
Zelensky amedokeza kwamba usimamizi wa kiwanda cha nyuklia cha Zaporizhzhia ulikuwa suala lingine lenye utata mkubwa.
Kiwanda hiki cha nyuklia, kikubwa zaidi barani Ulaya, kiko mstari wa mbele na kimekuwa chini ya udhibiti wa Urusi tangu mwezi Machi 2022.
Zelensky amesema kwamba suluhisho linalowezekana litakuwa kujiondoa kwa Urusi na kushiriki udhibiti wa kiwanda kati ya Kyiv na Marekani, huku akikiri kwamba maelezo ya makubaliano kama hayo hayakuwa wazi na kwamba Moscow haingeweza kukubaliana nayo.
Rais wa Marekani Donald Trump anaonekana kukasirishwa zaidi na ugumu wa mzozo huo, na Kyiv na washirika wake wana hofu kwamba Marekani inatafuta kulazimisha suluhisho linaloongozwa na Urusi dhidi ya Ukraine.
Zelensky amewaambia waandishi wa habari kwamba, ingawa Marekani inataka vita vikomeshwe haraka, hakuna tarehe ya mwisho iliyowekwa ya makubaliano.
Ukraine, ambayo inalengwa na mashambulizi makubwa ya anga, karibu kila siku, inatoa wito wa kusitishwa kwa mapigano na kusitisha mapigano mara moja kabla ya makubaliano magumu zaidi kufikiwa.
Hata hivyo, Urusi ina nia ya kuchelewesha kusitisha mapigano, huku wanajeshi wake wakiendelea kusonga mbele hatu kwa hatua lakini hakika kwenye mstari wa mbele, na mashambulizi yake yanawachosha raia wa Ukraine.
“Baada ya raundi kadhaa za mazungumzo na Urusi,” Marekani sasa imeungana na Moscow katika msimamo huu, Zelensky amesema.
Maafisa wa Kremlin wamekuwa waangalifu zaidi kuliko wenzao wa Ulaya, Marekani, na Ukraine.
Hata hivyo, Urusi imejitahidi, inapowezekana, kuimarisha hisia kwamba Moscow na Washington zinashiriki matarajio sawa kuhusu masharti ya makubaliano ya amani.
Siku ya Alhamisi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi Sergey Lavrov alisifu juhudi za Donald Trump za kupatanisha na akasema kwamba mkutano wa hivi karibuni huko Kremlin kati ya Rais Vladimir Putin na mjumbe wa Marekani Steve Witkoff umeondoa kutoelewana kati ya pande hizo mbili.
Waziri pia alifutilia mbali mapendekezo yanayodia kwamba Kyiv inaweza kunufaika na dhamana za usalama katika mfumo wa wanajeshi wa kigeni waliopo Ukraine.