Marekani. Staa wa Hollywood, Idris Elba (53), amesema kwamba ana mpango wa kuachana na uigizaji katika siku za usoni ili kujikita katika uongozaji wa filamu, kazi ambayo anaona inamfaa zaidi kwa wakati huu.
Elba ametoa kauli hiyo hivi karibu huko Jeddah, Saudi Arabia aliposhiriki kipindi cha maswali na majibu kwenye tamasha la kimataifa la filamu la Red Sea.
Mwigizaji huyo mwenye asili ya Sierra Leone, katika tamasha hilo aliwasilisha filamu yake mpya, Dust To Dreams’ ambayo ni kazi yake ya kwanza kiuongozaji tangu alipofanya filamu ya Yardie (2018).
Alisema kuwa licha ya kufurahia uigizaji, sasa anataka kutumia uzoefu wake kwenye eneo la uongozaji, hatua ambayo anategemea mashabiki wake wataipokea vizuri.
“Natumaini mashabiki wangu hawatanikasirikia… Hatimaye baada ya muda mrefu nataka kujikita katika uongozaji filamu kwa asilimia 100,” alisema Elba na kuongeza.
“Nimekuwa nikiigiza kwa muda mrefu, na bado ninaipenda kazi hiyo, lakini uongozaji unanipa fursa ya kutumia uwezo wangu mwingine na kuwa sehemu ya uzalishaji filamu kwa njia tofauti,” alieleza.
Hata hivyo, kwa mujibu wa The Hollywood Reporter, bado atarudi kwenye uigizaji akiendelea kucheza uhusika wake maarufu wa DCI John Luther. Ikumbukwe kuwa Elba amecheza nafasi ya ofisa huyo wa Uingereza tangu mwaka 2010.
Filamu mpya ya Luther inatarajiwa kuanza kurekodiwa mnamo Februari 2025, ikiwa ni baada ya Luther: The Fallen Sun (2023) kufanya vizuri.
Akiendelea kuelezea mipango yake, Elba alithibitisha kuwa filamu yake inayofuata akiwa kama mwongozaji ‘This Is How It Goes’, inatokana na tamthilia ya Neil LaBute (2005).
Filamu hiyo ilirekodiwa nchini Ghana na utayarishaji wake ulikamilika wiki iliyopita. Elba amesema amebadilisha hadithi ya awali na kuja na yake ila inayofanana na ile ya mwanzo.
“Tamthilia ya awali inamhusu mwanaume mweusi aliyemuoa mwanamke mzungu, kisha mwanaume mzungu anahamia nyumbani kwao, na inachunguza kinachotokea kwenye ndoa yao,” ameeleza.
“Nilinunua haki za filamu hiyo na nikabadili hadithi. Sasa ni mwanaume mzungu anayemuoa mwanamke mweusi, na mwanaume mweusi anakuja kuishi kwenye nyumba yao. Ni mtihani wa ndoa, uaminifu na masuala ya rangi,” alisema.
Elba ambaye ana zaidi ya kazi 130 za uigizaji, hapo awali kupitia Podcast ya Good Hang, alisema kwamba uigizaji kwake ni kama neema na si kazi ngumu kama watu wengi wanavyodhani.
“Kwa hiyo ninapopata nafasi ya kufanya kazi na wewe, au kuwa kwenye seti, sihisi kama kazi. Watu wengine wanasema, ‘Unajichosha sana,’ lakini kwangu si kazi ngumu kwa kiwango hicho,” alieleza.
Miongoni mwa filamu maarufu alizocheza Elba ni pamoja na The Jungle Book, The Wire, Hobbs & Shaw, Beasts of No Nation, The Harder They Fall, Luther, The Suicide Squad, Star Treak Beyond, Beast n.k.