
Lengo la mafunzo hayo limekuwa kuwatahadharisha vijana kuwa makini wanapotumia mitandao ya kijamii, hususan katika kipindi hiki ambacho nchi nyingi zinaghubikwa na chaguzi, ili kuepuka kueneza taarifa za uongo na kauli za chuki.
Miongoni mwa waliohudhuria mafunzo hayo yaliyojikita na ulinzi wa data na matumizi salama ya mitandao, ni Melissa Kasili, mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Masuala ya Ufundi cha Kenya au Technical University of Kenya kilichoko jijini Nairobi, anasema maisha ya vijana yako mitandaoni, lakini mara nyingi hukutana na kauli za chuki na taarifa potofu
“Kama vijana, tunatumia muda mwingi sana kwenye mitandao ya kijamii. Lakini tunapokuwa humo, mara nyingi tunakutana na jumbe za chuki na taarifa ambazo hatujui kama ni za kweli, na wakati mwingine tunazisambaza bila kuthibitisha.”
Melissa anasema mafunzo haya na mijadala waliyokuwa nayo imewakumbusha vijana umuhimu wa kuwajibika wanapochapisha au kusambaza taarifa mtandaoni.
“Leo tumekumbushwa kwamba ni kosa kusambaza taarifa bila uhakika. Kuna propaganda nyingi zinaenea, na kama vijana tunapaswa kuwa waangalifu ili tusije tukawa vyombo vya kusambaza chuki, hasa dhidi ya wanawake, na hasa wakati huu wa kuelekea uchaguzi.”
Anahimiza vijana wenzake kutumia mitandao kama jukwaa la kueneza ujumbe chanya, haki za binadamu na mshikamano.
“Tunapaswa kusambaza upendo na haki za binadamu. Njia mojawapo ya kujilinda ni kuhakiki taarifa, kuangalia chanzo chake, na kufuatilia vyombo vya habari vinavyoheshimika. Ukikosa kuthibitisha chanzo, mara nyingi taarifa hizo huwa si za kweli.”
Dhamira kuu ya mafunzo na mjadaIa huo ni kuwajengea vijana uwezo wa kutambua taarifa sahihi, kulinda data zao binafsi na kutumia mitandao ya kijamii kwa njia inayochangia amani, mshikamano na kulinda haki za binadamu katika jamii.