
Kwa mujibu wa Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi UNHCR, kurejea kwa mapigano katika eneo hili la mashariki mwa DRC kumesababisha ongezeko kubwa la wakimbizi wa Congo wanaoingia Burundi kupitia kituo cha mpakani cha Buganda tangu tarehe 5 Desemba.
“Wakimbizi wanaowasili wanaendelea kuingia Burundi. Maelfu ya familia zinazokimbia vurugu huko Kivu Kusini zinavuka maeneo ya vinamasi ya Mto Rusizi na pia zinafika kupitia Ziwa Tanganyika huko Rumonge, mara nyingi baada ya safari hatarishi,” imethibitisha ofisi ya UNHCR nchini Burundi kupitia mtandao wake wa kijamii wa X.
Shirika hilo la wakimbizi limesema mgogoro wa kibinadamu sasa unaambatana pia na wasiwasi wa kiusalama. Jumanne iliyopita, Burundi iliamua kufunga mpaka wake na DRC, baada ya kundi la M23 linaloungwa mkono na jeshi la Rwanda kuingia Uvira.
Wakimbizi 1000 watinga nchini Rwanda
Kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto UNICEF, kufuatia kuwasili kwa wingi kwa wakimbizi wa Congo nchini Burundi, waliokimbia mapigano makali huko Kivu Kusini, hususan katika maeneo ya Kamanyola, Luvungi na Katogota, “hali ya usalama imezorota kwa kiasi kikubwa tangu wiki iliyopita.”
Tathmini za awali zinaonesha “kiwango cha juu cha hatari na udhaifu miongoni mwa watu wapya wanaowasili hususan wale waliojeruhiwa wakati wa mapigano.”
Eneo la muda la mapokezi limeanzishwa karibu na Buganda, eneo lililo karibu na mpaka wa DRC, ili kuwahifadhi na kuwasaidia watu walioathirika.
Mbali na maelfu ya wakimbizi waliosajiliwa nchini Burundi, Rwanda pia inaripoti “ongezeko la wastani lakini linaloonekana la idadi ya wanaowasili kati ya tarehe 3 na 7 Desemba, ambapo takriban watu 1,000 waliingia kupitia kituo cha mpakani cha Bugarama kusini-magharibi mwa nchi hiyo.”
Zaidi ya watu 500,000 wamekuwa wakimbizi wa ndani nchini DRC
Ndani ya DRC, ahirika hilo la watoto linasema vurugu zimesababisha ufurushwaji mkubwa wa watu. Tangu tarehe 1 Desemba, zaidi ya watu 500,000, wakiwemo watoto 104,000, wamekimbia makazi yao mapya katika jimbo la Kivu Kusini, na ufurushwaji zaidi unatarajiwa kadri mapigano yanavyoenea katika maeneo mengine.
UNICEF inaripoti kuwa “ukiukwaji mkubwa wa haki dhidi ya watoto umeripotiwa, ikiwa ni pamoja na kuuawa kwa wanafunzi wanne katika shambulio la bomu huko Kaziba Walungu na kujeruhiwa kwa wanafunzi sita kwa risasi huko Walungu, Kabare na Bukavu”.
Mitandao ya ulinzi ya ndani pia imeripoti matukio mengine ya utekaji nyara na vifo vya raia, lakini bado hakuna takwimu zilizothibitishwa.
Aidha, kurejea kwa mapigano katika majimbo ya mashariki kumesababisha zaidi ya wanafunzi 390,000 kukosa masomo.
Kwa mujibu wa UNICEF, zaidi ya shule 1,200 sawa na asilimia 15 bado zimefungwa kutokana na mzozo huo. “Angalau shule saba na ofisi moja ya usimamizi wa elimu zimeshambuliwa au kuchukuliwa, na madarasa yameharibiwa au kubomolewa.”