
Mwaka 2025 unaashiria uzinduzi wa Ripoti ya tatu ya Viashiria ya GCR, ambayo inajengwa juu ya maarifa na uzoefu kutoka katika matoleo yaliyopita. Ripoti hii inatumia takwimu kutoka viashiria 16 vya GCR kutoa uchambuzi wa kina wa maendeleo yaliyofikiwa pamoja na changamoto zinazoendelea kuathiri utekelezaji wa mkataba huo wa kimataifa.
Aidha, ripoti inatoa mifano yenye ushahidi inayoonesha namna Mkataba wa Kimataifa wa Wakimbizi umechangia kuboresha mwitikio wa masuala ya wakimbizi katika maeneo mbalimbali duniani. Matokeo ya ripoti hii yanatarajiwa kuwa mchango muhimu katika Tathmini ya Maendeleo ya Jukwaa la Kimataifa la Wakimbizi, inayofanyika kuanzia leo tarehe 15 hadi 17 Desemba 2025.
Kwa mtazamo wa jumla, ripoti inaonesha maendeleo katika utekelezaji wa malengo yote manne ya GCR, na kusisitiza athari chanya za juhudi za pamoja kati ya serikali, mashirika ya kimataifa na wadau wengine.
Wakati huo huo, inaeleza kuwa upatikanaji wa takwimu unaendelea kuboreshwa, hali inayowezesha uundaji wa sera zenye ushahidi na ufanisi zaidi. Hata hivyo, ripoti inaonya kuwa mafanikio haya yako hatarini kutokana na kupungua kwa ufadhili na kudhoofika kwa mshikamano wa kimataifa.
Akizungumzia umuhimu wa kuendeleza juhudi hizi, Kamishna Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Wakimbizi (UNHCR), Filippo Grandi, amesema:
“Tunapoelekea kwenye Tathmini ya Maendeleo ya Jukwaa la Kimataifa la Wakimbizi mwezi huu Desemba 2025, ni muhimu kuendeleza msukumo uliopo na kuthibitisha upya dhamira yetu ya pamoja kwa misingi ya Mkataba wa Kimataifa wa Wakimbizi. Hakuna anayepaswa kudhani kuwa hili ni jambo rahisi. Lakini pia hatupaswi kukata tamaa.”
Fursa za suluhisho katika nchi za dunia ya tatu
Katika eneo la upatikanaji wa suluhisho kwa wakimbizi katika nchi za tatu, ripoti inaonesha mafanikio ya awali. Mwaka 2024, idadi ya wakimbizi waliopatiwa hifadhi kupitia mpango wa kuhamishiwa na kuishi upya ilizidi malengo ya mwaka. Ingawa mwaka 2025 ulishuhudia kushuka kwa kasi kwa idadi hiyo, kwa ujumla njia mbadala na za ziada zimeendelea kuongezeka. Kati ya mwaka 2016 hadi 2023, jumla ya nchi 38 zilitoa vibali kwa zaidi ya wakimbizi milioni 1.7 kupitia njia hizi.
Kurejea kwa usalama na heshima
Kwa upande wa kurejea kwa wakimbizi katika nchi zao za asili, ripoti inaonesha kuwa ufadhili kwa ajili ya wanaorejea uliongezeka kwa asilimia 6 kati ya mwaka 2020 na 2023. Hata hivyo, kiwango hiki bado kiko chini sana ikilinganishwa na mahitaji halisi, hasa kutokana na ongezeko kubwa la idadi ya wanaorejea.
Takwimu zinaonesha kuwa ni asilimia 3.5 tu ya Msaada Rasmi wa Maendeleo (ODA) unaohusiana na hali za wakimbizi uliwafikia wanaorejea, huku juhudi za ujenzi wa amani na maendeleo zikiendelea kukabiliwa na upungufu mkubwa wa ufadhili.
Kwa ujumla, Ripoti ya Viashiria ya GCR ya 2025 inatuma ujumbe wazi: licha ya mafanikio yaliyopatikana, bado kuna safari ndefu mbele. Mafanikio ya kweli yatategemea mshikamano wa kimataifa, ufadhili endelevu, na dhamira ya pamoja ya kuhakikisha wakimbizi wanapata ulinzi, suluhisho na maisha yenye heshima.