Tiba asilia inajumuisha mbinu na maarifa kutoka katika muktadha mbalimbali ya kihistoria na kitamaduni, ambayo ilikuwepo kabla ya tiba ya kisasa (biomedicine) na mifumo ya kawaida ya kitabibu.

Nchi wanachama wengi wa WHO zinaripoti kuwa kati ya asilimia 40 hadi 90 ya wakazi wao kwa sasa hutumia tiba asilia.

Haya ni kwa mujibu wa Dkt. Shyama Kuruvilla, mkurugenzi wa kituo cha dunia cha tiba asilia, kilichoanzishwa mwaka 2022 na WHO ili kutumia ipasavyo uwezo wa mifumo hii katika huduma za afya na ustawi wa jamii.

Kwa kuwa nusu ya watu duniani hawana huduma za msingi za afya, tiba asilia mara nyingi huwa ndiyo huduma ya karibu zaidi au pekee inayopatikana kwa watu wengi,” amesema Kuruvilla katika mkutano wa waandishi wa habari wa mtandaoni uliofanyika Jumatano, kuelekea Mkutano wa Dunia wa WHO kuhusu tiba asilia utakaofanyika baadaye mwezi huu.

Kwa watu wengine wengi, tiba asilia ni chaguo wanaloipendelea kwa sababu ni ya kibinafsi na ya mtazamo mpana. Inaendana na tamaduni na mazingira ya maisha, na inaunga mkono ustawi wa jumla wa mtu, badala ya kutibu dalili za ugonjwa fulani pekee,” Kuruvilla ameongeza.

Tiba asilia ni nini?

Kwa mujibu wa WHO, tiba asilia inajumuisha mbinu na maarifa yanayotokana na muktadha mbalimbali ya kihistoria na kitamaduni, na ambayo yalikuwepo kabla ya tiba ya kisasa na mifumo ya kawaida ya kitabibu.

Tiba asilia husisitiza matumizi ya tiba zinazotokana na maumbile na mbinu za jumla na za kibinafsi zinazolenga kurejesha uwiano kati ya akili, mwili na mazingira.

Kuruvilla amesema kuwa mahitaji ya tiba asilia duniani yanaongezeka kutokana na kuongezeka kwa magonjwa sugu, changamoto za afya ya akili, msongo wa mawazo, na hamu ya kupata huduma za afya zenye maana zaidi.

Ameongeza pia kuwa, licha ya matumizi yake makubwa na mahitaji yanayoongezeka, chini ya asilimia moja ya ufadhili wa utafiti wa afya duniani kwa sasa unaelekezwa kwenye tiba asilia.

Nini kitatokea katika mkutano huo?

Mkutano wa pili wa dunia kuhusu tiba asilia utafanyika kuanzia tarehe 17 hadi 19 Desemba na utawakutanisha watunga sera, waganga wa tiba asilia, wanasayansi na viongozi wa jamii za asili kutoka kote duniani.

Mkutano huo utafanyika New Delhi, India, na pia kwa njia ya mtandaoni.

Washiriki watajadili namna ya kutekeleza mkakati wa kimataifa wa tiba asilia hadi mwaka 2034, unaolenga kuendeleza tiba asilia, tiba mbadala na tiba shirikishi zinazotegemea ushahidi wa kisayansi, pamoja na kutoa miongozo kuhusu udhibiti na ushirikiano wa wadau mbalimbali.

Mkutano wa Dunia unalenga kuweka mazingira na ushirikiano unaohitajika ili tiba asilia iweze kuchangia kwa kiwango kikubwa ustawi wa watu wote na sayari yetu,” Kuruvilla amehitimisha.

Wakati huohuo, WHO inazindua maktaba ya kimataifa ya tiba asilia  jukwaa la kwanza la kidijitali la aina yake lenye zaidi ya rekodi za kisayansi milioni 1.6 kuhusu tiba asilia pamoja na mtandao wa takwimu za tiba asilia na mfumo wa maarifa ya kiasili, Bioanuwai na Afya, miongoni mwa mipango mingine.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *