Mkutano huu unatarajiwa kutangaza mipango mipya mikubwa ya kisayansi na ahadi za kimataifa zitakazosaidia kuharakisha utekelezaji wa Mkakati wa Kimataifa wa WHO wa Tiba Asili 2025–2034.
Mkakati huo unaweka msisitizo kwenye kuimarisha ushahidi wa kisayansi, kuboresha mifumo ya udhibiti, kuunganisha tiba asili katika mifumo ya afya, kuimarisha ushirikiano, pamoja na kushirikisha jamii kikamilifu.
Jamii na familia katika Ukanda wa Pasifiki Magharibi hutumia dawa asilia na nyongeza kwa kiasi kikubwa kwa matatizo mbalimbali ya kiafya, kuanzia magonjwa madogo hadi magonjwa yanayotishia maisha.
Nafasi ya tiba asili katika huduma za afya
Tiba za asili au dawa za mitishamba zinajumuisha mifumo iliyorasimishwa na isiyorasimishwa ambayo ilikuwepo kabla ya tiba za kisasa na imeendelea kubadilika kulingana na mahitaji ya nyakati za sasa.
WHO inasema kwa watu wengi duniani, tiba asili bado ni chanzo kikuu cha huduma za afya kutokana na upatikanaji wake wa karibu, gharama nafuu, na ulinganifu wake na tamaduni na mazingira yao ya kijamii.
Kwa wengine wengi zaidi, tiba asili ni chaguo linalopendelewa kwa kuwa ni la kibinafsi zaidi na linaonekana kuwa la asili. Takribani asilimia 90 ya Nchi Wanachama wa WHO ambazo ni nchi 170 kati ya 194 zinaripoti kuwa kati ya asilimia 40 hadi 90 ya wananchi wao hutumia tiba za asili.
Akizungumza katika ufunguzi wa mkutano huo, mjini New Delhi, nchini India Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dk. Tedros Adhanom Ghebreyesus, amesema shirika hilo limejizatiti kuunganisha hekima ya maelfu ya miaka na nguvu ya sayansi na teknolojia za kisasa ili kufanikisha dira ya “afya kwa wote.”
“Kwa kushirikiana kwa uwajibikaji, maadili na usawa, na kwa kutumia ubunifu kuanzia akili mnemba hadi jenomiki, tunaweza kufungua uwezo wa tiba asili kutoa suluhisho salama, bora na endelevu za afya kwa kila jamii na kwa sayari yetu,” amesema Dk. Tedros.
Maandalizi ya maagizo ya tiba asili katika kliniki ya dawa za jadi za Kichina huko Simao, mkoa wa Yunnan, Uchina.
Kuimarisha ushahidi, udhibiti na ujumuishaji katika mifumo ya afya
Katika kipindi ambacho mifumo ya afya duniani inakabiliwa na changamoto kubwa, takribani nusu ya watu wote duniani ambao ni watu bilioni 4.6 hawana upatikanaji wa huduma muhimu za afya. Aidha, zaidi ya watu bilioni 2 wanakumbwa na mzigo wa kifedha wanapojaribu kupata huduma za afya. limesema shirika hilo la afya duniani.
Kwa muktadha huo WHO inasema, ujumuishaji wa tiba asili katika mifumo ya afya ni muhimu katika kupanua upatikanaji wa huduma, kuongeza chaguo za matibabu nafuu na yanayomlenga mtu, pamoja na kusukuma mbele ajenda ya Afya kwa Wote (UHC), ili kila mtu apate huduma anazohitaji bila kuingia katika matatizo ya kifedha.
Limeongeza kuwa ushahidi unaojitokeza unaonesha kuwa kuunganisha tiba asili katika mifumo ya afya kunaweza kupunguza gharama na kuboresha matokeo ya kiafya. Aidha, mbinu hizi huweka mkazo kwenye kinga na uendelezaji wa afya, jambo linalochangia manufaa mapana zaidi, ikiwemo matumizi sahihi ya dawa za antibiotiki.
Hata hivyo, WHO inasisitiza kuwa ujumuishaji wenye mafanikio unahitaji sayansi thabiti, viwango vya kimataifa vya ubora na usalama, pamoja na mifumo madhubuti ya udhibiti.
“Ni lazima tutumie uthabiti ule ule wa kisayansi katika kutathmini na kuthibitisha tiba za kisasa na tiba asili, huku tukiheshimu bioanuai, upekee wa tamaduni na kanuni za kimaadili,” amesema Dk. Sylvie Briand, Mwanasayansi Mkuu wa WHO.
Ameongeza kuwa ushirikiano wa kimataifa na matumizi ya teknolojia za zenye uwezo mkubwa kama akili mnemba AI, jenomiki, biolojia ya mifumo, sayansi ya neva na uchambuzi wa kina wa takwimu vinaweza kubadilisha namna dunia inavyochunguza na kutumia tiba asili.
Ubunifu, uwekezaji na manufaa endelevu
WHO imesema Tiba asili ni mhimili wa sekta zinazokua kwa kasi duniani, ikiwemo sekta ya dawa za mitishamba. Kwa ujumla, dawa zote za tiba asili, pamoja na zaidi ya nusu ya dawa za kisasa za kibaolojia, zinatokana na rasilimali za asili, ambazo bado ni chanzo muhimu cha ugunduzi wa dawa mpya.
Dkt. Shyama Kuruvilla, Mkurugenzi a.i. wa Kituo cha Tiba Asilia Duniani cha WHO.
Jamii za asili duniani zinalinda takribani asilimia 40 ya bioanuai ya dunia, licha ya kuwa ni asilimia 6 tu ya idadi ya watu duniani. Hivyo basi, kuendeleza tiba asili kunahitaji pia kushughulikia haki za jamii za asili, biashara ya haki, na masuala ya mgawanyo wa manufaa.
Pamoja na matumizi yake makubwa na mchango wake katika uhifadhi wa rasilimali za asili kwa afya na ustawi, chini ya asilimia 1 ya fedha zote za utafiti wa afya duniani hutengwa kwa ajili ya tiba asili.
Ili kuziba pengo hilo la maarifa na utafiti, WHO imezindua Maktaba ya Kimataifa ya Tiba Asili ya kwanza ya aina yake yenye zaidi ya rekodi za kisayansi milioni 1.6, zikijumuisha tafiti, sera, kanuni na makusanyo ya mada mbalimbali kuhusu matumizi ya tiba asili.
Maktaba hiyo imeandaliwa kufuatia wito wa Wakuu wa Nchi katika mikutano ya G20 na BRICS mnamo mwaka 2023, na inalenga pia kutoa upatikanaji wa haki wa machapisho ya kitaaluma kwa taasisi za nchi zenye kipato cha chini kupitia mpango wa Research4Life. Aidha, inasaidia nchi kurekodi tiba asili kwa kulinda haki miliki na kujenga uwezo wa kisayansi kwa ajili ya kuendeleza ubunifu.
“Kuendeleza tiba asili ni wajibu wa kisayansi, kimaadili na kimazingira,” amesema Dk. Shyama Kuruvilla, Kaimu Mkurugenzi wa Kituo cha Kimataifa cha WHO cha Tiba Asili. “Mkutano huu wa Dunia unaweka msingi wa ushirikiano unaohitajika ili tiba asili ichangie kwa kiwango kikubwa ustawi wa watu wote na sayari.”
Mkutano huu wa kimataifa, unaofanyika kuanzia leo tarehe 17 hadi 19 Desemba 2025 jijini New Delhi, unatarajiwa pia kutangaza ahadi mpya kutoka kwa serikali na wadau wengine, sambamba na wito wa kuanzishwa kwa muungano wa kimataifa utakaoshughulikia mapungufu ya kimfumo na kuharakisha utekelezaji wa Mkakati wa Kimataifa wa Tiba Asili kwa kiwango kikubwa.