
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, “idadi ya raia wasiopungua 1,013 wameuawa kati ya tarehe 11 na 13 Aprili, katika kile kilichoelezwa kuwa ni mfumo thabiti wa ukiukwaji mkubwa wa sheria za kimataifa za kibinadamu na ukiukaji wa wazi wa haki za binadamu za kimataifa.”
Mauaji ya raia na watu kufurushwa
Ripoti imeeleza kuwa kati ya waliouawa, watu 319 wameuawa kinyume cha sheria, ama ndani ya kambi au walipokuwa wakijaribu kukimbia.
Baadhi yao wameuawa majumbani mwao wakati wa msako wa nyumba kwa nyumba uliofanywa na RSF, huku wengine wameuawa katika soko kuu, shule, vituo vya afya na misikiti.
Kufuatia mashambulizi hayo, zaidi ya wakazi 400,000 wamekimbia makazi yao kwa mara nyingine, na kuacha kambi hiyo ikiwa tupu.
Akisimulia tukio hilo, kiongozi mmoja wa jamii aliyenusurika amesema kuwa wapiganaji wawili wa RSF wameingiza bunduki zao kupitia matundu madogo ya dirisha la chumba walikokuwa wamejificha wanaume 10, kisha wamefyatua risasi kiholela, na kuua wanane wao papo hapo.
Kwa upande mwingine, mwanamke mmoja aliyerejea kambini siku iliyofuata kumtafuta mwanawe wa miaka 15 aliyepotea amesema
“Kambi imekuwa tupu. Nimeona miili ya watu ikiwa imesambaa barabarani. Kulikuwa na kuku, punda na kondoo pekee wakizunguka.”
Ameongeza kuwa hakumkuta mwanawe siku hiyo.
Onyo la UN: Uhalifu wa kivita unaweza kuwa umetendeka
Akizungumza kutokea Geneva, Uswisi Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Binadamu, Volker Türk, amesema mauaji ya makusudi ya raia au watu walioko nje ya mapigano “yanaweza kufikia kiwango cha uhalifu wa kivita wa mauaji.”
Amehimiza kufanyika kwa uchunguzi huru, wa kina na wenye ufanisi, na kuwawajibisha wote waliohusika kupitia taratibu za haki.
Mbali na mauaji, ripoti hiyo pia imebaini mifumo ya ukatili wa kingono unaohusiana na mzozo. Angalau manusura 104 wakiwemo wanawake 75, wasichana 26 na wavulana watatu, wengi wao kutoka kabila la Zaghawa wamekumbwa na vitendo vya kutisha vya ukatili wa kingono, vikiwemo ubakaji, ubakaji wa makundi na utumwa wa kingono, wakati wa shambulio hilo na katika njia za kutorokea nje ya kambi.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, “ukatili wa kingono umeonekana kutumiwa kwa makusudi kama silaha ya kueneza hofu ndani ya jamii.”
Kambi yazingirwa, njaa yatumiwa kama silaha
Ripoti pia imeeleza kuwa katika miezi iliyotangulia shambulio hilo la RSF limezuia kabisa kuingizwa kwa chakula, maji, mafuta na mahitaji mengine muhimu, huku likiwashambulia kwa utaratibu wale waliokuwa wakijaribu kupeleka misaada.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, watu 26 wamekamatwa na kuripotiwa kuuawa katika barabara kati ya Zamzam na Tawila, ikielezwa kuwa ni onyo kwa yeyote aliyekuwa akijaribu kuingiza chakula kambini.
Kutokana na hali hiyo, familia nyingi zimelazimika kuwalisha watoto chakula cha mifugo, ikiwemo maganda ya karanga.
Wito wa hatua za haraka za kimataifa
Akitoa tathmini yake, Türk amesema mifumo hiyo ya ukiukwaji wa haki “inaendana na kile ambacho Ofisi yake imekuwa ikikiripoti mara kwa mara, ikiwemo wakati wa kutwaliwa kwa El Fasher na RSF mwishoni mwa Oktoba.
Ameongeza kuwa, “matokeo ya ripoti hii ni ukumbusho mwingine mzito wa haja ya kuchukua hatua za haraka kukomesha mizunguko ya ukatili na kuhakikisha haki na fidia kwa waathirika. Dunia haiwezi kukaa kimya huku ukatili wa aina hii ukiendelea kushamiri nchini Sudan.”
Kamishna Mkuu huyo amezitaka nchi zote, hususan zenye ushawishi katika mgogoro huo, kuchukua hatua za haraka kuzuia uhalifu wa kimataifa, ikiwemo kusitisha usambazaji, uuzaji au uhamishaji wa silaha zinazoendelea kuchochea mzozo huo.
Aidha, amehimiza juhudi endelevu za kidiplomasia kuelekea kusitishwa kwa mapigano na kupatikana kwa suluhu ya kudumu ya mgogoro huo, Darfur, Kordofan na maeneo mengine ya Sudan.
Ripoti hiyo imetokana na ufuatiliaji wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Haki za Binadamu, ikiwemo mahojiano yaliyofanywa mnamo mwezi Julai, 2025 na manusura na mashahidi 155 walioko mashariki mwa Chad.