Kupitia jukwaa la kimataifa la kifedha la Revolut, lengo ni kuongeza na kurahisisha msaada kwa watu walioko katika safari za uhamiaji. 

Hatua hii inafanya IOM kuwa mdau wa hisani kwenye jukwaa la Revolut, ikiwapa mamilioni ya watumiaji njia rahisi na inayofikika ya kuwaunga mkono watu wanaohama duniani kote.

Kuanzia mwezi huu, watumiaji wa Revolut wataweza kuchangia kazi za IOM moja kwa moja kupitia programu kwa kutoa michango ya mara moja, kuanzisha michango ya mara kwa mara, au kuchagua mpango wa kuzungusha chenji.

Michango itaelekezwa kwa IOM

Michango yote itachakatwa kupitia Prism the Gift Fund, mshirika wa hisani wa IOM nchini Uingereza, kuhakikisha kuwa asilimia 100 ya michango inaelekezwa moja kwa moja kwa IOM.

“Ushirikiano huu na Revolut unalenga kukidhi mahitaji halisi kusaidia watu kupata huduma muhimu na fursa za kujijenga upya, huku tukiongeza uwezo wa jamii na mifumo inayokabiliana na changamoto za uhamishaji,” amesema Amy Pope, Mkurugenzi Mkuu wa IOM.

Ushirikiano huu unalenga kutumia wigo wa fedha za kidijitali kukusanya rasilimali zaidi kwa kazi za IOM katika maeneo kama msaada wa kibinadamu, utawala wa uhamiaji, na maendeleo endelevu. Kwa kuunganisha chaguo za kutoa michango katika miamala ya kila siku ya kifedha, mpango huu unaondoa vikwazo vya kutoa msaada na kuchochea ushiriki wa umma kwa njia endelevu.

IOM hufanya kazi na serikali, wadau na jamii kutoa msaada wa kuokoa maisha, kulinda haki, na kukuza suluhu zinazowanufaisha wahamiaji na jamii zinazowapokea. 

Mtiririko huu mpya wa fedha kutoka kwa watumiaji wa Revolut utasaidia kudumisha juhudi hizi na kuhakikisha rasilimali zinaelekezwa pale zinapohitajika zaidi.

Ushirikiano huu unaakisi mwelekeo unaoongezeka wa ubia kati ya mashirika ya kibinadamu na majukwaa ya fedha za kidijitali, ukionesha jinsi ubunifu unavyoweza kuimarisha mshikamano wa kimataifa katika kukabiliana na changamoto za uhamiaji. 

IOM inatarajia kuendeleza ushirikiano huu na kuchunguza fursa zaidi za kuwaunganisha watu binafsi na taasisi na njia za vitendo za kuunga mkono vipaumbele vya uhamiaji duniani kote.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *