
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jioni hii ya Ijumaa ya tarehe 19 Desemba 2025 na Stéphane Dujarric, Msemaji wa Katibu Mkuu, mfanyakazi huyo, Bol Rhoch Mayol Kuot, raia wa Sudan Kusini aliyekuwa akifanya kazi kama Msaidizi wa Lugha katika UNMISS, alikamatwa kwa nguvu na maafisa wa usalama karibu na mji wa Wau katika jimbo la Western Bahr el Ghazal tarehe 15 Desemba. Baadaye akauawa akiwa mikononi mwa waliomteka.
Katibu Mkuu ameitaka Serikali ya Sudan Kusini “itumie juhudi zozote” kuhakikisha kwamba wale wote waliohusika na uhalifu huo wanatambuliwa haraka na kuwajibishwa ipasavyo. Amesisitiza umuhimu wa kulinda wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa na kuheshimu utawala wa sheria.
Bwana Guterres pia ametuma salamu zake za rambirambi zake za dhati kwa familia na wapendwa wa marehemu Kuot, na kuthibitisha tena dhamira ya Umoja wa Mataifa ya kutoa msaada wote unaowezekana katika kipindi hiki kigumu sana.
UNMISS ina jukumu la kulinda raia, kuunga mkono utekelezaji wa mchakato wa amani wa Sudan Kusini na kusaidia kuweka mazingira yanayowezesha utoaji wa misaada ya kibinadamu kote nchini. Mauaji hayo yameibua upya wasiwasi kuhusu usalama wa wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa wanaofanya kazi katika nchi hiyo inayokabiliwa na migogoro.
Nayo UNMISS imesisitiza uchunguzi kupitia taarifa ya kulaani tukio hilo waliyoitoa leo mjni Juba.
“Tumesikitishwa sana na kumpoteza mwenzetu,” amesema Anita Kiki Gbeho, Afisa Msimamizi wa UNMISS.
“Vitendo kama hivi vya kuua wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa havikubaliki kabisa. Tunatoa wito wa kufanyika mara moja uchunguzi wa kina ili kubaini mazingira ya kukamatwa kwake na kifo chake, na kuhakikisha anapatiwa haki yeye na familia yake. Usalama na ulinzi wa wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa lazima viheshimiwe wakati wote,” amesema Anita Kiki Gbeho.
Ujumbe huo pia umetuma salamu za rambirambi kwa familia, marafiki na wafanyakazi wenzake wa marehemu, ukimuelezea kama mfanyakazi mwenye kujituma wa timu ya Umoja wa Mataifa aliyekuwa na dhamira ya dhati ya kuhudumia watu wa Sudan Kusini.