Wachezaji wa zamani wa Manchester United, Roy Keane na Gary Neville, wamewashutumu vikali mabeki wa klabu hiyo, Diogo Dalot na Leny Yoro, baada ya timu hiyo kupoteza ugenini dhidi ya Aston Villa katika mchezo wa Ligi Kuu England uliochezwa jana Jumapili, Desemba 21, 2025.

Manchester United ilikubali kipigo hicho baada ya Morgan Rogers kufunga mabao mawili yaliyoiwezesha Aston Villa kupata ushindi wa 10 mfululizo msimu huu, ushindi uliomaliza rekodi ya United kutofungwa ugenini Villa Park tangu mwaka 1995.

Akichambua mchezo huo kupitia, Keane amesema baadhi ya wachezaji wa United hawakuonyesha kupambana na kujituma ipasavyo, akimlenga zaidi Dalot.

“Unaweza kuwa na kipaji kikubwa kiasi gani, lakini lazima ujitume. Kuna wachezaji wengi, kama Dalot, ambao hawajitumi vya kutosha kwa ajili ya timu,” amesema Keane.

Keane aliongeza kuwa uzembe wa Dalot na Yoro ulichangia moja kwa moja mabao yaliyofungwa na Rogers, akisema hata katika bao la pili, Dalot hakumwekea presha ya kutosha Youri Tielemans kabla ya mpira kupigwa kuelekea kwa Rogers.

“Sitasema wanachezea timu, lakini hawajitumi vya kutosha. Kazi yao ni kuzuia hatari, lakini hawakufanya hivyo,” amesema Keane.

Kwa upande wake, Neville alimkosoa vikali beki chipukizi wa Kifaransa, Yoro, akisema alikuwa mzembe katika kujaribu kumziba Rogers kwenye bao la kwanza. “Yoro alitembea tu, hakutoka haraka kumkabili. Katika nafasi ile, huwezi kumwacha mchezaji kama Rogers apate muda na nafasi,” amesema Neville.

Neville amesema Yoro alipaswa kutoka kwa kasi zaidi kumkabili Rogers nje ya eneo la hatari, akionya kuwa mabeki wakubwa hawaruhusiwi kuteleza wanapokutana na wachezaji hatari. “Alitembea, na hilo lilikuwa kosa kubwa,” amesisitiza.

Kipigo hicho kiliinyima Manchester United nafasi ya kusogea karibu na wapinzani wao Chelsea na Liverpool katika mbio za kuwania nafasi nne za juu kwenye msimamo wa Ligi Kuu England.

United imebakia katika nafasi ya saba ikiwa na pointi zake 26 huku Aston Villa ikizidi kuzifukuzia Man City na Arsenal ikifikisha jumla ya pointi 36 katika nafasi ya tatu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *