
Uingereza, ambayo ni mwandishi mkuu wa azimio hilo kuhusu Somalia, ilisambaza rasimu ya azimio hilo kwa wajumbe wa Baraza.
Akilihutubia Baraza hilo la Usalama, Balozi wa Uingereza katika Umoja wa Mataifa, Archibald Young, amesema kupitishwa kwa azimio hilo kunafuatia uamuzi wa hivi karibuni wa kuongeza muda wa vikwazo dhidi ya kundi la Al-Shabaab. Amesema maamuzi hayo kwa pamoja yanaonesha dhamira endelevu ya Baraza la Usalama kuunga mkono Somalia katika mapambano yake dhidi ya Al-Shabaab.
Balozi Young pia amesema Somalia imepiga hatua kubwa tangu Baraza la Usalama lilipoidhinisha kwa mara ya kwanza kupelekwa kwa ujumbe wa AMISOM mwaka 2007. Ameeleza kuwa ili msaada wa Baraza hilo kwa Somalia uendelee kuwa mahsusi na wenye ufanisi, maamuzi ya Baraza yanapaswa kuendelea kuongozwa na uelewa wa kina wa muktadha wa kitaifa ambako AUSSOM imepelekwa.
Naibu Mwakilishi wa Kudumu wa China katika Umoja wa Mataifa, Sun Lei, amesema pengo la ufadhili linaloikabili AUSSOM kwa sasa haliwezi kuhimilika, huku upungufu wa fedha unaoikabili UNSOS ukiibua wasiwasi. Amesema China inazitaka nchi washirika wa kimataifa, hususan wafadhili wa jadi, kutimiza ahadi zao za awali na kuchukua hatua za haraka kupunguza shinikizo la kifedha linaloikabili AUSSOM.
Kwa upande wake, Balozi wa Marekani, Jeffrey Bartos, amesema Marekani inaendelea kuonesha kutoridhishwa na baadhi ya wajumbe wa Baraza kutumia mchakato wa kuongeza muda wa dhamana kusukuma lugha inayokengeusha mjadala, ikiwemo kuhusu masuala ya kijinsia.