
Huko Kimara Bonyokwa jijini Dar es Salaam, Tanzania, kikundi cha vijana kutoka Chuo cha Sayansi na Teknolojia cha Paradigms kimebuni suluhu bunifu ya kuchakata taka za plastiki na kuzibadili kuwa nishati safi ya kupikia ya gesi. Sabrina Saidi amezungumza na kiongozi wa mradi huo, Mhandisi wa Kemikali Amasha Kyando, pamoja na mmoja wa vijana wanaoshiriki katika mradi huo, kuhusu namna ubunifu huo unavyosaidia kulinda mazingira na kukuza matumizi ya nishati safi.
Sababu za kuanzisha mradi wa nishati safi
Akieleza kilichowasukuma kuanzisha mradi huo, Mhandisi Amasha Kyando anataja sababu kuu mbili. Mosi, ni ongezeko kubwa la taka za plastiki katika mazingira, hasa ya mijini. Kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2018, kiasi kikubwa cha taka hizo huzagaa bila kufanyiwa urejeshwaji au kuchakatwa, hali inayochangia uchafuzi wa mazingira.
Sababu ya pili ni msukumo wa kitaifa wa matumizi ya nishati safi ya kupikia, unaoendelezwa na Serikali ya Tanzania. Anasema sera na juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania zimewapa vijana hao fursa ya kuona namna wanavyoweza kuchangia ajenda ya taifa kwa kutumia taaluma zao.
Kwa nini nishati safi ya kupikia ya gesi na sio nyingine?
Akifafanua chaguo la gesi, Amasha anasema kila mbunifu huangalia tatizo lililopo katika jamii na njia bora ya kulitafutia suluhu.
“Tumeangalia changamoto ya uwepo wa plastiki kwa wingi katika mazingira yetu, na tumeona namna ya kuzibadilisha hizo plastiki ni kuwa nishati ya safi ya gesi ili kuweza kutatua hii changamoto ya ongezeko la taka za plastiki kwenye mazingira yetu.”
Mchakato wa kubadili plastiki kuwa gesi
Kwa mujibu wa Mhandisi Amasha, mchakato wa kuchakata taka za palstiki na kuzalisha gesi hupitia hatua sita muhimu.
- Hatua ya kwanza ni ukusanyaji wa taka za plastiki kutoka maeneo mbalimbali ikiwemo jalalani, majumbani na maeneo mengine ya kutupa taka.
- Baada ya kukusanywa, plastiki hizo hupangwa kwa makundi kulingana na aina zake, ikiwemo PET, HDPE, LDPE, PP, Nylon, PVC na nyinginezo.
Majina ya hizo aina za plastiki yameandikwa kwenye plastiki mbalimbali mfano chupa za maji na nyinginezo.
- Hizo plastiki tajwa hupangwa kwa makundi baada ya kukusanywa na kisha kuanza kufanyiwa kazi. Amasha anaeleza kwamba aina hizo kuu za plastiki ndizo ambazo hupatikana kwa urahisi katika mazingira ya kila siku ukilinganisha na aina nyingine.
- Kisha plastiki huanza kuchaguliwa kulingana na aina, hapa huchagua aina mojawapo kutoka katika yale makundi, mfano PET, ni aina ya plastiki ambayo hujumuisha plastiki zitokanazo na chupa za maji na juisi ingawa sio zote huwa ni aina hii ya plastiki.
- Baada ya kuchagua aina ya plastiki, kisha kusafishwa kwa kuondoa uchafu kama mchanga na maji, kabla ya kukatwa katika vipande vidogo vidogo vinavyojulikana kama plastic pallets. Vipande hivyo huwekwa kwenye mashine maalum ya uchakataji inayojulikana kitaalamu kama minupyrolysis reactor, ambapo huchakatwa kwa kutumia joto na kichocheo cha kemikali (catalyst).
- Na baada ya hapo jiko la gesi litawashwa ili kusaidia hiyo mashine ya kuchakata plastiki kupata joto na kuwezesha plastiki kuzalisha gesi na kupitia mchakato huo, plastiki huzalisha gesi ambayo hupitia hatua mbalimbali za uchujaji kabla ya kutumika moja kwa moja kwa kupikia.
Mchango wa mradi katika kuwawezesha vijana
Kuhusu uwepo wa idadi ya vijana na mabadiliko yoyote chanya katika jamii, Amasha anaeleza,
“Vijana wapo, wasichana kwa wavulana na kwa sasa hivi vijana hawa wanajitolea kufanya kazi kwenye huu mradi, kwa sababu mradi bado haujaanza kuzalisha hadi kufikia hatua ya kuuza, na kama tunavyofahamu gesi ikianza kuuzwa ni lazima ipite kuthibitishwa na mamlaka mbalimbali, kama Shirika la Viwango Tanzania (TBS) ili iweze kufaa kuingia kwenye matumizi. Lakini hatua nzuri ambayo tumefikia ni kwamba tumeshakwenda Shirika la Maendeleo ya Viwanda Vidogo Tanzania (SIDO), tumeshapeleka barua na wamekubali kuja kututembelea na pia wametupa barua ili kuweza kuchukua sampuli za gesi ili tupeleke TBS, kwa ajili ya kupimwa na kuthibisha ubora ili iweze kuwa tayari kwa matumizi.”
Ushirikiano na UNEP Tanzania
Mradi huu pia umeanza kupata mwitikio mzuri kutoka kwa wadau wa mazingira, ikiwemo Shirika la Umoja wa Mataifa la Mazingira (UNEP). Ushirikiano huo ulianza baada ya vijana hao kushiriki katika maonesho ya Siku ya Mazingira Duniani yaliyofanyika jijini Dar es Salaam.
Amasha anaeleza kuwa ubunifu wao uliwavutia UNEP, hali iliyosababisha kualikwa katika ofisi za shirika hilo jijini Dar es Salaam, na kuwasilisha kwa kina wazo la mradi. Baada ya mazungumzo na Mkuu wa UNEP Tanzania, Bi. Clara Makenya, waliombwa kuandaa nyaraka za mradi ikiwemo muhtasari wa kibiashara unaoonesha uwezo wa mradi huo katika kutengeneza ajira na kuleta faida kwa jamii na taifa kwa ujumla.
Matumizi mengine ya gesi hiyo
Mbali na kupikia, Amasha anaeleza kuwa gesi inayozalishwa kupitia uchakataji wa plastiki inaweza pia kutumika kuendesha mitambo ya umeme na mashine za kusaga nafaka, hivyo kuongeza wigo wa matumizi yake katika shughuli za kiuchumi.
Changamoto zinazowakabili katika kutekeleza mradi
Licha ya mafanikio yaliyofikiwa, mradi huu bado unakabiliwa na changamoto kadhaa, ikiwemo ukosefu wa wafadhili na mlezi wa kudumu wa mradi, pamoja na changamoto ya mtaji. Amasha anasema kwa sasa analazimika kutumia sehemu ya kipato chake binafsi ili kuendeleza shughuli za mradi huo.
Vijana wanaoshiriki mradi, nao wana lipi la kusema?
Mmoja wa vijana wanaoshiriki mradi huo, Ng’eni H. Ng’eni, Mhandisi wa Ujenzi, anaeleza kwamba kabla ya kujiunga katika mradi huu, amekuwa akijishughulisha na shughuli hiyo hiyo ya uhandisi ujenzi, lakini pia ni msaidizi wa mafunzo chuoni hapo na anashiriki kwa karibu katika utekelezaji wa mradi wa uchakataji wa taka za plastiki.
Ng’eni anasema “kilichonivutia zaidi hadi kujiunga kwenye mradi huu ni kuona jinsi taka za plastiki zinachakatwa na kutengeneza nishati safi kwa sababu zinaenda kusafisha mazingira.”
Ng’eni anahitimisha kwa kusema kuwa anajisikia faraja kuwepo katika mradi huu, kwa sababu anahusika katika kutunza mazingira na kuyaweka safi.