Kwa mujibu wa ofisi hiyo, raia wanatishiwa na mamlaka za kijeshi pamoja na makundi yenye silaha yanayopinga jeshi, kuhusu ushiriki wao katika uchaguzi huo.
Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa, Volker Türk, amesema “mamlaka za kijeshi zinapaswa kusitisha matumizi ya vurugu za kikatili kuwalazimisha watu kupiga kura, na kusitisha kuwakamata wale wanaoonyesha maoni tofauti.”
Kamishna Türk amesema uchaguzi huo “unafanyika katika mazingira ya vurugu na ukandamizaji, bila hali ya kuwezesha uhuru wa kujieleza, kushirikiana au kukusanyika kwa amani.”
Hali ilivyo
Ofisi ya haki za binadamu imeeleza katika taarifa yake ripoti zinaeleza kuwa watu kadhaa wamekamatwa chini ya kile kinachoitwa “sheria ya ulinzi wa uchaguzi” kwa kutumia haki yao ya uhuru wa kujieleza. Baadhi yao wamehukumiwa adhabu kali, wakiwemo vijana watatu wa Hlaingthaya, eneo la Yangon, waliopewa hukumu ya vifungo vya kati ya miaka 42 na 49 gerezani kwa kubandika mabango ya kupinga uchaguzi.
Watu wengine waliokamatwa ni pamoja na watu mashuhuri kama mwongozaji wa filamu Mike Tee, mwigizaji Kyaw Win Htut na mchekeshaji Ohn Daing, waliohukumiwa vifungo vya miaka saba kwa kukosoa filamu ya propaganda inayounga mkono uchaguzi.
Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Haki za Binadamu pia imepokea taarifa kutoka kwa watu waliokimbia makazi yao, wakiwemo wanaoishi katika eneo la Mandalay, waliotishiwa kushambuliwa au kunyang’anywa nyumba zao endapo hawatarudi kupiga kura. Türk amesema “kuwalazimisha watu waliokimbia kurejea katika mazingira hatarishi ni ukiukwaji wa haki za binadamu.”
Pia kumekuwepo na vitisho kutoka kwa makundi yenye silaha yanayopinga jeshi, ikiwemo utekaji wa walimu wanawake tisa na mashambulizi ya mabomu yaliyowajeruhi wafanyakazi wa uchaguzi.