Ripoti hiyo inaeleza kuwa biashara ya kimataifa ya bidhaa za mbao na karatasi imeanza kurejea taratibu, huku ukuaji mdogo ukishuhudiwa katika karibu makundi yote makuu ya bidhaa. Hali hii inajiri baada ya biashara ya bidhaa hizo kushuka kwa jumla ya asilimia 14 mwaka 2023.

Kwa ujumla, mauzo ya nje ya bidhaa za mbao na karatasi duniani yameongezeka kwa kiasi cha dola bilioni 7, sawa na ongezeko la asilimia 1.4, na kufikia dola bilioni 486 mwaka 2024. Hata hivyo, kiwango hiki bado kiko juu kuliko viwango vyote vilivyorekodiwa kabla ya mwaka 2021. Aidha, mauzo ya nje ya bidhaa zisizo za mbao kutoka misituni yameongezeka na kufikia dola bilioni 25, jambo linaloonesha mchango unaoongezeka wa kiuchumi wa sekta ya misitu duniani.

Akizungumza kutoka Rome, Italia, Mkurugenzi Mkuu wa FAO, Qu Dongyu, amesema “Misitu ni chanzo cha maisha kwa mamilioni ya watu duniani kote, na idadi hiyo inatarajiwa kuongezeka kadri misitu inavyoendelea kutoa fursa zaidi za kiuchumi, ikiwemo uzalishaji endelevu wa mbao.”

Miti iliyovunjwa msituni kwa ajili ya mbao

© Unsplash/Ingemar Johnsson

Miti iliyovunjwa msituni kwa ajili ya mbao

Uzalishaji wa bidhaa za mbao waongezeka 

Matokeo ya mwaka 2024 yanaonesha kuimarika taratibu kwa masoko ya bidhaa za misitu katika kanda mbalimbali duniani, hali iliyochochewa na ongezeko la uzalishaji katika makundi mengi ya bidhaa za mbao. Ongezeko hilo limeanzia asilimia 2 kwa mbao ghafi za viwandani, vidonge vya mbao vya nishati (pellet za mbao) na majimaji ya mbao, hadi kati ya asilimia 4 na 5 kwa paneli za mbao, karatasi na kartoni.

Kwa ujumla, ripoti ya FAO inaonesha kuwa licha ya changamoto zilizojitokeza katika miaka ya hivi karibuni, sekta ya bidhaa za misitu duniani inaendelea kuimarika taratibu, huku ikitoa mchango unaoongezeka katika ukuaji wa uchumi na ajira duniani.

Mbao ghafi za viwandani

Uzalishaji wa mbao ghafi za viwandani — yaani mbao zinazokatwa kwa matumizi yasiyo ya nishati — uliongezeka kwa asilimia 2 na kufikia mita za ujazo bilioni 1.96 mwaka 2024. Hata hivyo, biashara ya kimataifa ya mbao hizo ilipungua kwa asilimia 1 na kufikia mita za ujazo milioni 96.

Mbao zilizokatwa

Uzalishaji wa mbao zilizokatwa duniani kwa ujumla umebaki katika kiwango cha karibu sawa, ingawa tofauti zimejitokeza kati ya kanda. Uzalishaji umepungua kwa asilimia 2 barani Amerika Kaskazini, lakini umebaki thabiti barani Ulaya na katika eneo la Asia-Pasifiki. Kwa upande mwingine, Amerika ya Kusini na visiwa vya Karibiani zilirekodi ongezeko la asilimia 2. Biashara ya mbao zilizokatwa haikuonesha mabadiliko makubwa ikilinganishwa na mwaka 2023.

Ukungu unakusanyika kwenye msitu wa mvua wa kitropiki nchini Indonesia

UN Indonesia

Paneli za mbao

Uzalishaji wa paneli za mbao umeendelea kuimarika kwa mwaka wa pili mfululizo, baada ya dalili za kurejea katika hali ya kawaida kuanza kuonekana mwaka 2023. Uzalishaji wa kimataifa umeongezeka kwa asilimia 5 na kufikia mita za ujazo milioni 393, huku ongezeko likiripotiwa katika kanda zote tano za dunia. Biashara ya kimataifa ya paneli hizo nayo iliongezeka kwa asilimia 6 na kufikia mita za ujazo milioni 90.

Majimaji ya mbao na karatasi iliyorejelewa

Uzalishaji wa majimaji ya mbao umeongezeka kwa asilimia 3 na kufikia tani milioni 189 mwaka 2024, huku biashara ya kimataifa ikiongezeka kwa asilimia 2 na kufikia kiwango cha juu zaidi kuwahi kurekodiwa cha tani milioni 73.

Sehemu kubwa ya uzalishaji mpya ilitoka China na  barani Amerika ya Kusini, hususan Brazil, Chile na Uruguay, hali inayoashiria ushindani unaoongezeka wa eneo hilo katika sekta ya majimaji ya mbao. Wakati huo huo, matumizi ya karatasi iliyorejelewa duniani yaliongezeka kwa asilimia 1 na kufikia tani milioni 243.

Peleti za mbao

Peleti za mbao zimeendelea kushuhudia ukuaji mkubwa katika miongo ya hivi karibuni, hususan kutokana na malengo ya matumizi ya nishati jadidifu barani Ulaya, Jamhuri ya Korea na Japan. Baada ya kushuka kidogo mwaka 2023, uzalishaji wa peleti za mbao duniani ulirejea kufikia kiwango cha tani milioni 48 mwaka 2024, sawa na kiwango cha mwaka 2022. Takribani theluthi mbili ya uzalishaji huo — tani milioni 31 — ziliingia katika biashara ya kimataifa.

Bara la Ulaya na Amerika Kaskazini yamebaki kuwa wazalishaji wakuu, yakichangia asilimia 47 na asilimia 28 ya uzalishaji wa dunia mtawalia. Hata hivyo, mchango wa eneo la Asia-Pasifiki uliongezeka kutoka asilimia 14 mwaka 2020 hadi asilimia 22 mwaka 2024. Kwa upande wa matumizi, Ulaya iliongoza kwa kuchangia asilimia 70 ya matumizi ya vidonge vya mbao duniani, ikifuatiwa na Asia-Pasifiki kwa asilimia 28.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *