
Dar es Salaam. Unaweza kusema yajayo yanafurahisha kuhusu kurudiana kwa mastaa wawili waliowahi kuwa ‘couple’ ya nguvu hapa Bongo, Harmonize na Kajala. Hii ni baada ya wawili hao kuonekana pamoja usiku wa kuamkia leo Desemba 26, 2025.
Wawili hao walionekana pamoja wakati Harmonize alipokuwa kwenye show visiwani Zanzibar ambapo alifuchua rasmi kurudiana na Kajala jambo ambalo liliibua shangwe kwa mashabiki waliohudhuria katika show hiyo. Na baada ya muda Konde alimpandisha jukwaani kumtambulisha Kajala huku akimwagia sifa kwa kumtaja kuwa ndiye mwanamke mzuri kushinda wote.
“Mtu ninayempenda yupo hapa kwa ajili ya kunisapoti, wewe ni mzuri sana, wewe ni mwanamke mzuri ambaye sijawahi kumwona kwenye maisha yangu, watu wameshakuona naomba ukapumzike, na hii ndio ilikuwa zawadi yangu ya Krismass kwenu,” amesema Konde boy.
Utakumbuka uhusiano wa wawili hao ulianza mapema mwaka 2021 na baada ya hapo waliachana lakini huo haukuwa mwisho wao walirudiana tena mwaka 2022 ambapo walirudi kwa kishindo na Harmonize kumvisha pete Kajala.
Tukio ambalo lilifanyika Juni 25, 2022 katika hoteli ya Serena na kulipa jina la ‘Late Lunch’ huku likihudhuriwa na watu wa karibu wa wasanii hao ukiwamo uongozi wa lebo ya Konde Gang, Mkurugenzi wa TVE, Francis Ciza ‘Majizzo’, Aunty Ezekiel, Martin Kadinda na wengineo.
Wawili hao walichumbiana ikiwa ni takribani mwaka mmoja tangu walipotengana baada ya mwanamuziki huyo kumfungulia mashtaka Kajala na binti yake Paula akiwatuhumu kuvujisha picha zake za utupu.
Aidha, licha ya kurudiana kwao penzi hilo lilivunjika tena miaka miwili iliyopita na kila mmoja akafuata njia yake. Lakini sasa wameibua tena mjadala kutokana na mabusu waliyopigana katika show ya Konde iliyofanyika Zanzibar. Huku kukiwa na tetesi kuwa wawili hao walirudiana tangu mwezi Mei mwaka huu.