Akizungumza kutokea makao makuu ya WHO mjini Geneva, Uswisi, Dkt. Tedros amesema mwaka 2025 umekuwa na mafanikio makubwa pamoja na changamoto nzito kwa afya ya dunia, huku akisisitiza kwamba dunia bado inahitaji uwepo wa WHO.
“Kweli mwaka 2025 umekuwa mwaka wa mafanikio makubwa na changamoto nyingi kwa afya ya dunia na kwa WHO. Mafanikio makubwa zaidi yalikuwa kupitishwa kwa Mkataba wa WHO wa kukabiliana na milipuko ya magonjwa, ambao ni mfano wa nguvu ya ushirikiano wa kimataifa pale nchi zinapochagua kushirikiana badala ya kugawanyika. Pia, mwaka huu WHO imethibitisha nchi 13 kufanikiwa kutokomeza magonjwa, ikatoa miongozo kuhusu tiba mpya kama Lenacapavir kwa kinga dhidi ya VVU na matibabu ya GLP-1 kwa utipwatipwa,na ikachukua hatua dhidi ya majanga 48 katika nchi na maeneo 79, ikiwemo Gaza, Sudan na Ukraine.”
Ulaji wa mara kwa mara wa chakula cha mafuta mengi unaweza kuwa na uzoea kwa watoto.
Akizungumzia changamoto, Dkt. Tedros amesema kupunguzwa kwa misaada ya kimataifa na bajeti kumeathiri sekta ya afya duniani, lakini ameeleza kuwa hali hiyo pia inaleta fursa mpya.
“Lakini ndani ya changamoto hizi pia kuna fursa. Ni fursa kwa nchi kuondokana na utegemezi wa misaada na kujenga mifumo ya afya inayojitegemea, na ni fursa kwa WHO kuwa taasisi imara zaidi na inayojipanga kwa siku zijazo. Dunia bado inahitaji WHO, na WHO itaendelea kushikilia maono yake ya msingi kuhakikisha kiwango cha juu kabisa cha afya kinapatikana kwa wote, si kama upendeleo wa wachache, bali kama haki ya kila mtu.”
Dkt. Tedros amehitimisha ujumbe wake kwa kusema kuwa WHO itaendelea kushirikiana na nchi wanachama ili kukabiliana na changamoto za sasa na zijazo za afya duniani.