Dar es Salaam. Adam Nyaonge, aliyekuwa dereva wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kwa miaka 19, kisha akafukuzwa kazi kwa madai ya kuwasilisha cheti cha elimu ya sekondari kilichoghushiwa, amekwama kisiki mahakamani kupinga uamuzi huo.

Nyaonge alifungua maombi namba 7332 ya 2025 dhidi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, BoT, Tume ya Utumishi wa Umma (PSC) na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), akiomba mapitio ya mahakama ili ifute uamuzi huo.

Hata hivyo, Desemba 24, 2025, baada ya mahakama kupitia mawasilisho ya pande zote mbili, Jaji Awamu Mbagwa wa Mahakama Kuu, Masjala Ndogo Dar es Salaam, aliyatupa maombi ya mapitio akisema hayana mashiko.

Kwa mujibu wa kumbukumbu za shauri hilo, Nyaonge aliajiriwa BoT kuanzia Agosti 25, 2003 hadi Julai 27, 2022, alipopewa mashtaka ya kinidhamu akituhumiwa kughushi cheti cha Kidato cha Nne (CSEE) chenye namba S.578-074.

Katika hati ya mashtaka aliyopewa, inadaiwa cheti hicho alichowasilisha kilikuwa na alama za ufaulu zisizo zake, hivyo kutoa taarifa za uongo ili kupata ajira kutoka kwa mjibu maombi wa pili ambaye ni BoT.

Katika mwenendo wa Kamati ya Nidhamu ya BoT, inaonyeshwa kuwa Nyaonge alipewa muda wa siku 14 kuwasilisha utetezi na alifanya hivyo, akikataa tuhuma zote zilizoelekezwa kwake na kueleza kuwa hakifahamu cheti hicho.

Katika usikilizwaji wa shauri hilo kwenye kamati ya nidhamu, Oktoba 10, 2022, mwombaji alikabidhiwa barua ya kuachishwa kazi. Hakuridhika na uamuzi huo, hivyo akakata rufaa PSC, ambayo ilibatilisha uamuzi huo na kuamuru shauri lisikilizwe upya.

Baada ya shauri hilo kusikilizwa upya, alikutwa na makosa, hivyo akakata tena rufaa PSC ambako, Oktoba 3, 2023, Tume ya Utumishi wa Umma ilibariki uamuzi wa kamati ya nidhamu. Akakata rufaa kwa Rais, lakini nako alikwaa kisiki.

Katika kipindi chote cha usikilizwaji, Nyaonge alishikilia msimamo kuwa hakuwahi kuwasilisha cheti anachodaiwa kuwasilisha na kwamba kile kilichopelekwa Baraza la Mitihani la Tanzania (Necta) kwa uhakiki kinatofautiana na kile kinachodaiwa kughushiwa.

Mwombaji anadai hakuwahi kuorodheshwa miongoni mwa watumishi wa BoT waliobainika kuwa na vyeti vya kughushi na kwamba uchunguzi uliofanyika ulikuwa wa upande mmoja, ukiwa chini ya usimamizi wa mwajiri pekee.

Ni kutokana na madai hayo ndipo alipofungua maombi ya kupatiwa kibali cha mahakama ili afungue maombi ya mapitio. Alifungua maombi hayo dhidi ya wajibu maombi wanne, akipinga kufutwa kwake kazi BoT.

Aliwasilisha hoja tatu. Hoja ya kwanza ni kuwa Rais alimwachisha kazi kwa kuegemea cheti ambacho hajawahi kukimiliki wala kukiwasilisha kwa mwajiri.

Hoja ya pili ni kwamba uamuzi wa PSC ni kinyume cha hati ya mashtaka ya kinidhamu, kwa kuwa cheti kinachodaiwa kughushi kina namba S.578-074 CSEE, huku mlalamikiwa wa kwanza (Rais) na wa tatu (PSC) waliamua kesi yake kwa kuegemea cheti chenye namba S.0578-074 CSEE, ambacho ni cheti halisi kilichowasilishwa na mwombaji.

Majibu ya wajibu maombi

Katika majibu yao, wajibu maombi walieleza kuwa ajira ya mwombaji iliwekewa masharti ya kuwasilisha vyeti halisi vya kitaaluma vinavyoweza kuthibitishwa.

Wamedai mashtaka dhidi yake yalifunguliwa kihalali baada ya uhakiki wa Necta, ambao ulibainisha kuwa cheti alichowasilisha kilikuwa na alama za uongo zisizolingana na rekodi rasmi.

Kwa maoni yao, kuachishwa kazi kwa mwombaji kulitokana na utovu wa nidhamu na kutekelezwa kwa mujibu wa sheria zinazotumika za utumishi wa umma.

Wajibu maombi walieleza kuwa uchunguzi na mchakato wa kinidhamu haukuwa na upendeleo, ulikuwa wa kina na uliendana na kanuni za haki asilia, wakisisitiza kuwa mwombaji alipewa nafasi ya kusikilizwa katika tuhuma zote.

Kwa hiyo, walieleza PSC na Rais walithibitisha kwa usahihi uamuzi wa kamati ya nidhamu, na mwombaji ndiye anayewajibika kwa nyaraka alizoziwasilisha kwa ajili ya kupata ajira na upungufu uliokuwapo katika cheti hicho.

Walalamikiwa walipinga ombi la mwombaji la mapitio ya mahakama, wakidai nafuu inayoombwa ni matumizi mabaya ya mchakato wa mahakama.

Uamuzi wa Jaji Mbagwa

Katika uamuzi alioutoa Desemba 24, 2025 na kupakiwa kwenye tovuti ya Mahakama Desemba 29, 2025, Jaji Mbagwa alianza kwa kujadili hoja ya mwombaji kuwa hakuwahi kuwasilisha kwa mwajiri cheti chenye namba S.578-074.

Wajibu maombi walijibu kuwa kumbukumbu zote za ajira, kikiwamo cheti kilichowasilishwa wakati mwombaji anaajiriwa, zilikuwa chini ya hifadhi ya wajibu maombi na kwamba mwombaji anajua aliwasilisha cheti chenye alama zilizoongezwa.

Hivyo, kamati ya nidhamu ilifanya mwenendo wake kwa kuegemea taarifa zilizohakikiwa kutoka Necta na Ofisi ya Rasilimali Watu ya BoT.

Jaji amesema ni kanuni ya msingi kuwa mtumishi wa umma ni lazima awe na sifa za kielimu kwa nafasi aliyoajiriwa au anayoishikilia, kama inavyosisitizwa chini ya Kanuni ya 12 ya Kanuni za Utumishi wa Umma za mwaka 2022.

“Uwasilishaji wa vyeti vya kughushi vya kitaaluma ni utovu wa nidhamu mkubwa na uvunjaji wa uaminifu,” amesema Jaji Mbagwa na kuongeza:

“Kutokana na kumbukumbu, ni dhahiri kwamba mwombaji alipewa fursa ya kusikilizwa kikamilifu kwa nidhamu na fursa ya kuwasilisha utetezi wake, hivyo kukidhi kanuni ya kupewa haki ya kusikilizwa au kutoadhibiwa bila kupewa nafasi ya kujitetea.”

Amesema: “Kwa maoni yangu, madai ya mwombaji kwamba hakuwasilisha cheti cha kughushi hayaonyeshi kuwepo kwa ukiukwaji wa utaratibu anaouomba uingiliwe na mahakama.”

Kuhusu hoja ya pili, amesema madai ya tofauti kati ya hati ya mashtaka na uamuzi, mahakama ilishaweka msimamo kuwa makosa madogo kama ya namba au nukuu (citation) hayawezi kuharamisha mwenendo wa shauri la nidhamu.

“Hasa pale ambapo maudhui ya mashtaka yalikuwa bayana na mlalamikiwa alipewa nafasi ya kujitetea,” amesema.

Jaji amesema hoja ya msingi katika kamati ya nidhamu ilikuwa ni uwasilishaji wa cheti cha kughushi, na hoja hiyo imebaki bila kupingwa.

Akizungumzia hoja ya tatu, amesema kuwasilisha cheti cha kitaaluma kilichoghushiwa si tu ukiukwaji mkubwa wa maadili ya utumishi wa umma bali pia ni kosa la jinai.

“Kamati ya nidhamu, Tume (PSC) na Rais walitumia mamlaka yao ya kisheria na kikatiba ndani ya mipaka ya sheria. Kanuni za haki asilia zilizingatiwa, na uamuzi ulikuwa wa busara, sawia na halali,” amesema.

Jaji amesema kumbukumbu zinathibitisha kuwa mwombaji alisikilizwa kwa haki, ikiwamo kusikilizwa na kamati ya nidhamu, kupata mashtaka aliyokuwa akikabiliwa nayo, fursa ya kujitetea na kukata rufaa PSC na kwa Rais.

Mbagwa amesema katika maombi ya mapitio ya mahakama, wajibu wa mahakama ni kupima uhalali wa kisheria, busara na usahihi wa taratibu, si kuchambua ushahidi uliowasilishwa mbele ya chombo chenye mamlaka.

“Baada ya kuchunguza kwa makini ukweli, ushahidi na mawasilisho ya pande zote mbili, mahakama hii imeridhika kuwa uamuzi wa kumfuta kazi ulifanywa ndani ya mamlaka ya kisheria na ulizingatia kikamilifu kanuni za haki asilia,” amesema.

Ni kwa msingi huo, ameyatupa maombi ya Nyaonge akisema hayana sifa.

Katika maombi hayo, mawasilisho ya mwombaji yaliwasilishwa na Wakili Benedict Chang’ambwe, wakati wajibu maombi yaliwasilishwa na Wakili wa Serikali, Hemed Mkomwa, ambao jaji amesema waliisaidia mahakama kufikia uamuzi wa haki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *