Rungu la Baraza la sanaa la Taifa (BASATA) na Bodi ya Filamu nchini limeendelea kuwaponda baadhi ya wasanii ambao wamekiuka Kanuni na sheria katika kazi zao zilizowekwa kwaajili ya kulinda Sheria, Taratibu, Imani, na maadili ya Mtanzania kwa mwaka 2025.
Hatahivyo Taasisi hizo za Kiserikali zimeendelea kutoa pongezi kwa baadhi ya wasanii ambao wamefikia mafanikio makubwa kama Tuzo na kutwaa mataji katika mashindano mbalimbali yaliyofanyika ndani na nje ya nchi kwa mwaka 2025.
Tukianzia na baadhi ya wasanii waliyojikuta matatani dhidi ya Basata na Bodi ya Filamu nchini kutokana na kazi zao kukosa vigezo na kukiuka kanuni na sheria za kazi za sanaa zilizowekwa na Taasisi hizo. Na hii ni Orodha ya wasanii muziki na filamu na kazi zao zilizo waingiza kikaangano.
OSCAR OSCAR, Siku ya Mei 22, 2025, mtangazaji na msanii mpya wa hip hop Oscar Oscar aliitwa Balaza la Sanaa la Taifa (BASATA) baada ya kuachia wimbo wake wa kwanza wa Mniombee iliyotoka Mei 21, 2025, akimshirikisha msanii wa Hip hop Joh Makini.
BASATA walieleza kuwa wimbo huo haukuwa na maadili ya Mtanzania na kumpatia mwongozo msanii huyo na kuagiza wimbo huo upigwe kwenye kumbi za starehe, katika vyombo vya habari kuanzia saa sita usiku. Pia kutopigwa kwenye vyombo vya usifiri wa umma, na kwenye matamasha kama kuna watoto.
Hatahivyo baada ya kikao na baraza hilo, Oscar Oscar alizungumza na wanahabari na kusema kwake ni furaha kuitwa Basata kwani huwezi kuwa msanii mkubwa nchini kama hujawahi kuitwa Basata.
RAPCHA, Siku ya Septemba 11, 2025, Msanii wa muziki wa hip-hop nchini, Cosmas Mfoy maarufu ‘Rapcha’ aliiitikia wito wa Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA). Kwaajili ya mazungumzo kufuatia maudhui ambayo sio ya kimaadili yanayopatikana kwenye video ya wimbo wake mpya ‘Yeeeh’ aliyoachia hivi karibuni.
Kikao hicho kilichoongozwa na Katibu Mtendaji wa Baraza hilo, Dk Kedmon Mapana ambapo msanii huyo aliomba radhi kwa BASATA na Watanzania kwa maudhui ya wimbo huo, huku akichukua hatua ya kuushusha katika majukwaa ya kidijitali.
Aidha, Rapcha alipokea kitabu cha muongozo wa maadili katika kazi za sanaa kilichotolewa na baraza hilo kama mwongozo wa kufuata katika kazi zake zijazo.
Rapcha ameahidi kushirikiana kwa karibu na BASATA na kuwa balozi mzuri wa kuhamasisha maadili bora katika tasnia ya sanaa nchini. Rapcha aliachia video na picha za wimbo wa ‘Yeeeh’ kwenye mitandao ya kijamii kuanzaia Septemba 3, 2025, ambapo kwa mujibu wa BASATA haikuwa na maadili mazuri ya Mtanzania na kupelekea video hiyo kushushwa katika jukwaa la YouTube.
IBRAAH & HARMONIZE
Siku ya Mei 12, 2025, msanii wa Bongo Fleva Ibraah aliitikia wito wa kufika Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) kufuatia mgogoro uliyojitokea baina yake na uongozi wa lebo iliyokuwa ikimsimamia ya Konde Music.
Baraza hilo liliwataka Ibraah na uongozi wa lebo hiyo ambayo ipo chini ya msanii Harmonize wafike BASATA baada ya mvutano wao uliyotokana na chapisho la Ibraah kwenye ukurasa wake wa Instagram akihitaji kujitoa kwenye lebo hiyo lakini anashindwa kutokana na masharti magumu ya mkataba wake.
Uongozi wa lebo hiyo ulimzuia msanii huyo kutoa au kushiriki katika kazi yoyote ya muziki kama ilivyoainishwa kwenye mkataba wake huku akihitajika kuilipa lebo hiyo Sh1 bilioni kama fidia ya kumkuza kimuziki. Kwa takribani siku mbili iIbraah aliitikia wito wa BASATA kufuatia sakata hilo huku Harmonize akishindwa kutokea kwenye baraza hilo.
Hatahivyo sakata hilo liliisha na msanii Ibraah akapewa haki yake ya kuwa msanii huru huku akirudishiwa akaunti na majukwaa yake ya Kidijitali ili kuendelea na shughuli zake kama msanii anayejitegemea.
Siku ya Oktoba 21, 2025, Baraza la Sanaa la Taifa BASATA liliufungia wimbo wa msanii wa Hip hop nchini, Ibrahim Mussa maarufu Roma Mkatoliki ‘Teremsha Bunduki’ kwa kukiuka kanuni ya 25 (6) (b) kwa madai ya wimbo huo kuwa na upotoshaji (c) kuchochea ghasia ya aina au namna yoyote (d) meneno ya uongo, uchochezi.
Kulingana na kanuni za BASATA wimbo wa ‘Teremsha Bunduki’ umepewa Daraja la KK sawa na R yaani wimbo huo hautakiwi kupigwa au kuoneshwa mahali popote nchini.
Wimbo huo ulizuiliwa na Baraza la Sanaa la Taifa, hivyo, na kupigwa marufuku ya kutopigwa kwenye vyombo vya habari au kusambazwa kwenye mitandao ya kijamii mpaka utakapofanyiwa marekebisho.
Atakayekiuka atachukuliwa adhabu za kisheria kama inavyoelezwa katika Kanuni za Baraza za mwaka 2018 kanuni ya 25 (8) kipengele (a) na (b).
Siku ya Desemba 4, 2025, Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) lilimpongeza kwa dhati msanii wa Hip hop nchini, Frida Amani kwa kuteuliwa kuwa balozi wa Hifadhi ya Mazingira chini ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Mazingira (UNEP).
BODI YA FILAMU
WEMA SEPETU, Siku ya Mei 22, 2025 msanii wa maigizo nchini Wema Sepetu alifika Bodi ya Filamu Tanzania ambapo aliitwa kutokana na vazi alilokuwa amevaa kwenye moja ya kumbi ya starehe kudaiwa halina staha.
Kikao hicho kiliongozwa na Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu nchini, Dkt. Gervas ambaye alisisitiza wasanii kujitambua na kujua thamani yao kwenye jamii.
Hatahivyo muigizaji huyo alisema kuitwa kwake na Bodi ya Filamu Tanzania kumemfanya atambue thamani yake. “Labda niseme kwamba mzungumzo baina yangu mimi na Bodi ya Filamu yalikuwa ni mazungumzo ya kirafiki sana, tulikuwa tunakumbushana kwa sababu hata mimi nilikuwa naogopa.
“Lakini hayakuwa yako vile nilivyokua nategemea ni katika kuwekana sawa. Pia nimejisikia vizuri kwa sababu nimetambua thamani yangu na nimeona ni jinsi gani ninavyopendwa kwa sababu ningekuwa nimeachwa tuu nisingeambiwa chochote wala kuitwa au kukanywa,”alisema.
AUNTY EZEKIEL
Msanii wa filamu nchini, Aunty Ezekiel siku ya Julai 10, 2025, aliitwa na Bodi ya Filamu nchini kosa likitajwa ni kuchapisha picha chafu kwenye ukurasa wake wa Instagram.
Hatahivyo muigizaji huyo baada ya kikao na Bodi hiyo alikutana na waandishi wahabari na kukiri kosa na kuomba radhi kwa mashabiki akisema kuna muda kama wasnii huwa wanajisahau na kuweka maudhui ambayo ni kinyume na maadili kitu ambacho hupotosha kizazi kijacho.
Utakumbuka Aunty Ezekiel aliandikiwa wito huo na Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu Tanzania, Dkt Gervas Kasiga Julai 7,2025 akimtaka msanii huyo kuwasili katika ofisi za Bodi hiyo Julai 10,2025.
KAJALA, HEMEDY ‘PHD’, NICOLE
Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu nchini, Dkt. Gervas Kasiga aliwapa onyo waigizaji wa filamu nchini, Aunty Ezekiel, Nicole, Hemedy Suleiman ‘PHD’, na Kajala Masanja akiwataka kubadilisha mwenendo wao na kujitambua kama wanatasnia wenye nafasi kubwa kwenye jamii.
Dkt. Kasiga alitoa onyo hilo Julai 10, 2025, katika ofisi za Bodi ya Filamu Kivukoni, Dar Es Salaam muda mchache mara baada ya kumaliza kikao na muigizaji, Aunty Ezekiel aliyeitwa kupewa onyo baada ya kuchapisa picha chafu mitandaoni.
Akizungumza na waandishi wa habari aliwapa onyo kali wasanii hao kutokana na maudhui ambayo wamekua wakiyaweka kwenye mitandao ya kijamii kuwa kinyume na maadili ya Mtanzania na kuathiri kizazi kijacho.
Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu Tanzania, Dkt. Gervas Kasiga (PhD) alikutana na kufanya mazungumzo na kumpa pongezi mwanatasnia wa filamu na michezo ya kuigiza John Elisha @officiallboneka tarehe 3 Desemba 2025.
John Elisha alifika ofisi za Bodi ya Filamu Tanzania kuitambulisha tuzo ya Mwigizaji Bora wa Mwaka 2025 aliyoipata kupitia tuzo za Tanzania Global Awards tarehe 29 Novemba visiwani Zanzibar. Elisha amepokea tuzo hii kupitia tamthiliya ya Kombolela inayorushwa katika chaneli ya Sinema Zetu ya Azam Tv.
Oktoba 24, 2025, Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu Tanzania, Dkt. Gervas Kasiga (PhD) alikutana na kufanya mazungumzo na Bw. Peter Severini @mchungajipeterseverini —Mtayarishaji na Muongozaji wa filamu nchini Tanzania.
Peter amefika ofisi za Bodi ya Filamu kuitambulisha tuzo ya Filamu Bora ya Mwaka 2025 aliyoipata kupitia filamu yake “KADO”. Tuzo hii imetolewa na Music Video Awards Africa (MVAA) tarehe 11 Oktoba 2025—Lagos, Nigeria na kupokea hongera kutoka kwa Mtendaji wa Baraza hilo.
Peter ni miongoni mwa watayarishaji na waongozaji filamu wanaoaminika nchini Tanzania kutokana na kazi zake kuchaguliwa katika tuzo mbalimbali ndani na nje ya nchi.
Oktoba 23, 2025, Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu Tanzania, Dkt. Gervas Kasiga (PhD) aalikutana na kumpa pongezi mwanatasnia wa filamu na michezo ya kuigiza John Elisha @officialboneka kwa ushindi wa tuzo.
John Elisha alifika ofisi za Bodi ya Filamu Tanzania kuitambulisha tuzo ya Mwigizaji Bora wa Mwaka 2025 aliyoipata kupitia tuzo za East Africa Youth Panel Awards @eastafrican_youthpanel tarehe 19 Oktoba 2025. Elisha alipokea tuzo hii kupitia tamthiliya ya Kombolela inayorushwa katika chaneli ya Sinema Zetu ya Azam Tv.
Oktoba 11, 2025, bodi ya Filamu nchini ilimpongeza muigizaji Stella Mbunge baada ya kuibuka mshindi wa tuzo ya Best MVAA Upcoming Actress of the Year 2025 tuzo zilizoandaliwa na Music Video Africa Awards huko Jijini Lagos nchini Naijeria. Stella Mbuge aliwania tuzo hizo kupitia tamthiliya mbili alizozicheza za “Nuru” na “Jiya”.
Oktoba 13, 2025 Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu Tanzania, Dkt. Gervas Kasiga (PhD) alikutana na kufanya mazungumzo ikiwemo kumpa hongera ya ushindi wa tuzo mwatasania wa filamu na michezo ya kuigiza nchini Agness Suleiman Kahamba ‘Aggybaby’
Hii ni baada Agness Kahamba kupokea Tuzo ya Mwigizaji Bora wa Kike wa Mwaka 2025 kutoka Achievers Awards International ya nchini Naijeria kutokana na kazi zake za sanaa ya uigizaji na shughuli zake za huduma kwa jamii kupitia taasisi yake Tupaze Sauti Foundation (Tanzania).
Desemba 3, 2025, Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu Tanzania, Dkt. Gervas Kasiga alikutana na kufanya mazungumzo na kumpongeza kwa ushindi wa tuzo mwanatasnia wa filamu na michezo ya kuigiza, Mzee Jafari Makatu.
Makatu alifika ofisi za Bodi ya Filamu Tanzania kuitambulisha tuzo ya Mwigizaji Bora wa kiume wa Mwaka 2025 Chaguo la Watazamaji aliyoipata kupitia Tamasha la Tuzo za Filamu Morogoro lililofanyika Mjini Morogoro tarehe 29 Novemba 2025.